KIPA wa Ken Gold, Castory Mhagama amesema wanaoibeza timu hiyo kwa kutokuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu, wasubiri kwani ligi ndio imeanza na matokeo yatazungumza.
Mhagama anayecheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, amekuwa na rekodi ya kipekee baada ya kuipandisha timu hiyo ya mkoani Mbeya akiipa ubingwa wa Championship msimu uliopita.
Kipa huyo ndiye alicheza mechi zote za Championship, ambapo katika michezo yote walipoteza mechi mbili, sare saba wakishinda michezo 21 na kumaliza kinara kwenye ligi kwa pointi 70.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mhagama alisema baada ya kufikia malengo yao ya kupandisha timu, kwa sasa kazi iliyobaki ni kupambania timu hiyo kufanya vizuri Ligi Kuu.
Kuhusu uzoefu wao, alisema kila mmoja anao mwanzo wa katika maisha, hivyo walichonacho wataongeza na kile kilicholetwa na baadhi ya wenzao waliotua kikosini.
“Hata walio na uzoefu hawakuanza nao, kila kitu na mwanzo wake hivyo hata sisi tutafikia huko walipo wengine, kimsingi ni kupambania timu kuhakikisha tunafanya viozuri.”
Kocha mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema pamoja na usajili wa wachezaji wengi chipukizi, wamekuwa na muda mzuri wa maandalizi kwa kutengeneza muunganiko, hivyo anaamini watafanya vizuri.
“Tumewaandaa vijana kubadilika kuondoa dhana ya Championship ili kucheza Ligi Kuu, tumetengeneza muunganiko mzuri na vijana watafanya vizuri,” alisema Elias.