MRATIBU wa Simba Queens, Selemani Makanya amesema viongozi wa timu hiyo iliyopo Ethiopia kushiriki fainali za michuano ya Klabu Bingwa kwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kusaka tiketi ya kucheza Klabu Bingwa ya Afrika, wamejiandaa kumburuza straika, Aisha Mnunka kwa Shirikisho la Soka (TFF) kwa utoro.
Mnunka anadaiwa hajaripoti hadi sasa katika klabu hiyo kama ambavyo Mwanaspoti liliwajulisha awali kwamba ametoroka na kutokuwa sehemu ya msafara wa timu hiyo iliyopo Addis Ababa kushiriki michuano hiyo ya Cecafa ambapo leo itatupa karata ya kwanza dhidi ya FAD ya Djibouti Uwanja wa Aveve Bikila.
Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizinasa ni kwamba nyota huyo aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), amefichwa na timu mpya jijini Dar es Salaam (jina tunalo), kitu kilichowatibua mabosi wa Msimbazi wanaelezwa wameshaandika barua ya kuipeleka TFF kumshtaki mchezaji huyo.
Makanya alisema wamewaandikia barua TFF ya kutaarifu utoro wa mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba Queens ambao ni mabingwa wa Tanzania kwa msimu uliopita.
Aliongeza, Aisha Mnunka ni mtoro kazini kwani alitakiwa kuripoti Simba mara baada ya majukumu ya timu ya taifa, lakini hakufanya hivyo na hakuna mawasiliano yoyote hadi sasa kitu kinachowatibulia katika mipango ya kusaka tiketi ya CAF.
Makanya alisisitiza kuwa, nyota huyo hakutoa taarifa yoyote kuhusu utoro wake na uongozi umefanya jitihada zote za kumtafuta bila mafanikio na hata katika simu hapatikani kwa kuwa amebadilisha namba.
“Aisha Mnunka bado ni mchezaji wa Simba, ana mkataba wa mwaka mzima, lakini hatuna taarifa rasmi, baada ya kurejea kikosi cha timu ya taifa alitakiwa kuripoti kambini lakini hakuripoti na hakuna taarifa yoyote aliyotoa kwa viongozi kama anaumwa au la hivyo tumepeleka malalamiko TFF,” alisema Makanya.