Shetani wa Buswita alivyoibuka tena kwenye usajili wa  2024/25

Dirisha la usajili kwa Tanzania limefungwa Agosti 15 na kuhitimisha mwezi mmoja na nusu wa pilikapilika za kuwania wachezaji zilizotawalia na visa na mikasa.

Klabu ya Simba ya Dar es Salaam ndiyo iliyoongoza kwa mikasa, ikianza na ule wa Lameck Lawi wa Coastal Union, Valentino Mashaka wa Geita Gold, Yusuf Kagoma wa Singida Black Stars na Awesu Awesu wa KMC.

Wachezaji hawa wote walilalamikiwa na vilabu vyao kwamba walisaini Simba wakiwa bado na mikataba nao.

Hali hii ya wachezaji kusaini mikataba na vilabu zaidi ya kimoja haijaanza leo.

Ipo kwa miaka na miaka lakini haikujulikana chanzo chake hadi mwaka 2017 pale Pius Buswita alipoitangazia dunia chanzo cha mikasa ya aina hii.

Mwaka huo, Pius Buswita akitokea Mbao FC ya Mwanza, alisaini mkataba na Yanga na Simba zote Dar es Salaam.

Sakata lake lilipofika kwenye vyombo vya sheria, mchezaji huyo alikiri kufanya kosa hilo kwa nguvu za shetani.

Kupitia wakala wake, Medi Mtabora, Buswita alisema kwamba shetani alimpitia ndiyo maana akasaini Simba na Yanga!

Hapo ndipo tukajua kwamba kumbe wachezaji husaini na vilabu zaidi ya kimoja kwa sababu ya shetani.

Na shetani aliyempitia Buswita ndiyo huyo aliyewapitia akina Awesu Awesu na aliwapitia wengi sana kabla yake na kuwafanya wasaini vilabu zaidi ya kimoja ndani ya dirisha moja la usajili na kusababisha migogoro.

Wafuatao ni baadhi ya wachezaji nyota waliowahi kupitiwa na shetani huyo na kugonga vichwa vya habari.

Nyota wa kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu AFCON 1980, Mtemi Ramadhani, aliwahi kupitiwa na shetani huyu mwaka huo,

Yeye aliweka rekodi kwa kusaini vilabu vinne ndani ya dirisha moja la usajili.

Kiungo huyo fundi alisaini na vilabu vya Waziri Mkuu SC ya Dodoma, Pan African FC, Yanga SC na Simba SC za Dar es Salaam.

Mbaya zaidi alisaini muda mfupi kabla ya Taifa Stars kwenda kwenye fainali za AFCON za Nigeria.

Akiwa huko aling’ara sana na huku nyumbani taarifa zikavuja kwamba amesaini vilabu vinne.

Siku Taifa Stars inarudi nyumbani baada ya mashindano, viongozi wa vilabu vile vinne walifika uwanja wa ndege kumuwahi na kuleta patashika kubwa kiasi cha kutwangana makonde.

FAT chini ya Mwenyekiti wake Said El Maamry, ikaamuru kwamba Mtemi achague timu anayoipenda, akachagua Simba.

Yanga hawakukubali, wakakata rufaa BMT iliyotengua uamuzi wa FAT na kumfungia mwaka mmoja.

2. MOHAMED MWAMEJA, HUSSEIN MARSHA NA KENNETH MKAPA.

Mwaka 1993, Mohamed Mwameja wa Coastal Union ya Tanga, Hussein Marsha wa Pamba ya Mwanza na Kenneth Mkapa wa Yanga walipitiwa na shetani wa Buswita na kusaini Yanga na Simba.

FAT chini ya mwenyekiti Muhidin Ndolanga na katibu Geras Lubega, ilikuwa inaelekea kuwafungia.

Bahati njema kwao ilikuwa Yanga kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati huko Uganda.

Waliporudi, walienda Ikulu kwa Rais Ali Hassan Mwinyi kumkabidhi kombe la ubingwa.

Katika hotuba yake ya kupokea Kombe, Rais Mwinyi akawaombea msamaha wachezaji hao akitumia msemo wa Kiswahili ‘kosa moja haliachi mke’.

FAT wakapokea maombi ya Rais na kuwasamehe.

Mwaka 1995, klabu ya Sporting Lisbon ilipanga kumuuza Luis Figo kwa Juventus. Mwenyewe hakupenda kwenda huko hivyo akasaini ili tu kuiridhisha klabu yake halafu akasaini Parma klabu aliyoitaka yeye.

Mgogoro huu ukasababisha afungiwe miaka miwili Italia, ndo akatimkia Barcelona!

4. CHARLES BONIFACE MKWASSA

Mwaka 1979, Yanga ilimsaini kiungo fundi aliyeisaidia klabu ya Mseto ya Morogoro kushinda ubingwa wa ligi ya taifa mwaka 1975, Charles Boniface Mkwasa.

Nyota huyo ambaye baada ya ubingwa alihamia Tumbaku ya Morogoro pia, akatua Jangwani kuleta matumaini mapya kwa Yanga iliyoyumba tangu mpasuko wa 1976 uliozaa Pan African.

Mwaka 1982, Simba ilimfuata na kumrubuni ahamie kwao, naye akakubali na kusaini Simba SC kwa jina la Charles Boniface alilokuwa pia akitumia Yanga, Tumbaku na Mseto.

Lakini Yanga wakamfuata na kumshawishi abaki, na baada ya kukubaliana naye, akasaini kuendelea kuichezea Yanga, safari hii akitumia jina la Charles Boniface Mkwasa.

Lakini hii mbele ya FAT ya El Maamry ilidunda na Mkwasa alifungiwa msimu mzima kabla ya kumaliza adhabu yake na kuendelea kucheza Jangwani.

Akiwa mchezaji wa Pamba ya Mwanza mwanzoni mwa miaka ya 1980, beki Yussuf Ismail Bana alisaini Simba katika fomu za usajili akitumia jina la Yussuf Ismail.

Lakini baadaye Yanga wakamfuata na kumrubuni asaini kwao, akasaini Jangwani na kutumia jina la Yussuf Bana.

Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) chini ya Mwenyekiti wake wa enzi hizo, Said Hamad El Maamry wakamuidhinisha kuchezea Yanga.

Chini ya El Maamry, FAT ilikuwa na utaratibu wa kumuuliza mchezaji, “katika timu hizi mbili ulizosaini, unaipenda ipi?’

Timu atayoitaja ndiyo atakayoidhinishwa kuitumikia.

Mwaka 2012 mashindano ya Kagame yalifanyika Dar es Salaam Tanzania na moja ya timu zilizoshiriki ilikuwa APR ya Rwanda.

Timu hiyo ya jeshi ilikuja na mchezaji wake mwenye asili ya DRC, Mbuyu Twitte, ambaye alichukua uraia wa Rwanda.

Twitte aling’ara sana na baada ya mashindano, Yanga na Simba zikaingia vitani kumwania.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, akasafiri hadi Rwanda na kuonana na viongozi wa APR na kumalizana nao, kisha akaongea na mchezaji.

Akakubaliana naye kila kitu na kumpatia dola 30,000 za Marekani kama pesa za kusaini mkataba.

Baada ya hayo yote, akapiga naye picha na kuisambaza Tanzania kwamba amemaliza na Twitte ni mchezaji halali wa Simba.

Kumbe Rage alikosea. Twitte hakuwa mchezaji wa APR bali FC Lupopo ya Lubumbashi DRC, aliyekuwa kwa mkopo APR.

Yanga walipojua hilo, wakaenda DRC kuonana na klabu yake na kukubaliana nayo.

Mchezaji akawa hana namna zaidi ya kukubali mahitaji ya klabu yake inayommiliki, siyo ile ya mkopo.

Akasaini Yanga na siku anafika uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere, alipewa jezi namba 4 yenye jina la Rage.

Hapa Yanga walikuwa wanalipa kisasi cha mwaka 2004 walichofanyiwa na Simba, kama itakavyosimuliwa katika mkasa unaofuata.

Mwaka 2004, mlinzi mahiri wa Simba, Victor Costa Nampoka ‘Nyumba’, alisaini Yanga na kujiunga na timu hiyo kwenye Kombe la Mapinduzi Zanzibar.

Aliyefanikisha umafia huu alikuwa katibu mkuu wa Yanga, Jamal Malinzi.

Kwa mbwembwe na bashasha za ‘kihaya’, Malinzi alitamba sana kwamba amewanyoosha Simba.

Baada ya mashindano, Costa akarudi Dar es Salaam na kusaini tena Simba SC.

Siku anaenda mazoezini kwa mara ya kwanza baada ya kurudi Simba, alivalishwa jezi namba 4 yenye jina la Malinzi.

Jamal Malinzi alikuwa katibu mkuu wa Yanga na ndiye aliyemrubuni mchezaji huyo.

Lakini baada ya Zacharia Hans Pope wa Simba kufanikiwa kumrudisha nyumba kibabe mchezaji huyo, ikawa zamu ya Simba kumcheka Malinzi na ndipo jina lake likaandikwa kwenye jezi.

Makoye alikuwa mchezaji mpya kwenye kikosi cha Yanga aliyesajiliwa kutoka Kagera Stars mwaka 2000.

Simba SC wakamfuata na kumrubuni asaini kwao. Makoye, ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika sekondari ya Makongo, alichukua fedha za Simba akasaini.

Hata hivyo, siku hiyohiyo Yanga walimnasa na kumchukua hadi kwa viongozi wa Simba kurudisha fedha alizochukua aendelee kuchezea Yanga.

Simba waligoma kuchukua fedha na kwa sababu wakati huo FAT ilikuwa haitambui mikataba ya klabu na mchezaji zaidi ya fomu za usajili, ambazo zilikuwa hazijatoka, Makoye aliendelea kuchezea Yanga, ingawa baadaye alichezea Simba alipotemwa Yanga.

Related Posts