Watoto walivyo hatarini kwenye viwanja vya soka

Katika viwanja vya michezo nchini, mchezo wa mpira wa miguu una nafasi ya pekee katika nyoyo za Watanzania.

Wakati wa mechi kubwa, hususani zile zinazohusisha timu za Simba na Yanga, viwanja vya mpira hujaa maelfu ya mashabiki.

Pamoja na shangwe na vigelegele vinavyosikika, kuna kundi moja linalokabiliwa na hatari nyingi zaidi, kundi la watoto.

 Licha ya uwepo wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inayoweka wazi haki na usalama wa mtoto, bado hali halisi viwanjani inaonesha kuwa usimamizi wa sheria hii ni changamoto kubwa.

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, kupitia Kifungu cha 5, inasema; “Ni wajibu wa mzazi, mlezi, jamii, na serikali kuhakikisha kuwa mtoto anapata ulinzi wa kutosha dhidi ya vitendo vya kikatili au vya kumdhuru kimwili au kisaikolojia.”

Aidha, Kifungu cha 10 cha sheria hiyo kinatamka kuwa; “Kila mtoto ana haki ya kupata huduma bora za afya na matibabu ili kuhakikisha ukuaji mzuri wa kimwili na kiakili.”

 Hata hivyo, picha halisi katika viwanja vya michezo nchini, hususani wakati wa matamasha na mechi kubwa, inaonyesha uzembe katika usimamizi wa sheria hizi.

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na matukio kadhaa ya kusikitisha ambayo yamezua maswali mengi kuhusu usalama wa watoto viwanjani.

 Mwaka 2021, mtoto wa miaka saba alifariki dunia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa mechi ya Taifa Stars dhidi ya Uganda.

Tukio hili lilifungua macho ya wengi kuhusu hali ya usalama viwanjani, hususani kwa watoto. Pamoja na jitihada za serikali na wadau wa michezo, hali bado ni tete.

Tamasha la Yanga la mwaka 2023 kutokana na wingi wa watu geti lilivunjwa pia mwaka huu 2024 katika matamasha  ikiwepo tamasha la Yanga la mwaka 2023 na mwaka huu kwa matamasha yote mawili ya Simba na la Yanga.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa wazazi wengi huwaleta watoto wao kwenye mechi kubwa kama sehemu ya kuwafunza mapenzi ya timu wakiwa bado wadogo.

Ramadhani Salum, mkazi wa Yombo, ni mmoja wa wazazi walioamua kumleta mtoto wake wa miezi 10 kwenye tamasha la Yanga.

“Nimekuja na mtoto wangu kwa sababu anaipenda Yanga pia namrithisha mapema ili asione cha ajabu akikua na atakuwa na kumbukumbu ya kufika katika uwanja huu tangu akiwa mdogo,” anasema Salum.

Hali kadhalika, Khadija Kazi, mkazi wa Mbagala, alimleta mjukuu wake wa miezi 18 na wengine wa miaka saba na 13 uwanjani.

“Hivi ninavyokwambia wengine wapo njiani wanakuja tena na mtoto wetu mdogo wa miezi nane ikicheza Yanga hatuwezi kukaa nyumbani tunakuja ukoo mzima,” anasema Khadija.

Hata hivyo, nia hii nzuri ya wazazi kuwaleta watoto wao kushuhudia mechi kubwa inakuja na changamoto zake nyingi.

Japo Agosti 08, Philimon Jackson anasema hakupata taabu kuingia na vijana wake wawili kutokana na kuwekwa utaratibu uliopunguza msongamano, lakini changamoto kwa wenye watoto huwa wakati wa kutoka.

“Muda huo inabidi mzazi kuwa makini vinginevyo utamuumiza mtoto, mfano mimi huwa nasubiri watu wanapungua kabisa ndio nashuka na wanangu, najali sana usalama wao kwa kuwa pale kwenye ngazi ni pembamba na wanafungua mlango mmoja,” anasema Jackson.

Yohana Wagalo anayependa kwenda uwanjani kwenye dabi na kijana wake tangu akiwa na miaka miwili hadi sasa minne anasema kuanzia kwenye kuingia kijana wake huyo anakuwa mabegani.

“Huwa nahakikisha anakula kabisa nje ya uwanja, tukiingia ndani anakuwa full (ameshiba) anajisaidia kabisa, tukikaa tumekaa, ambacho namnunulia ni maji tu,” anasema Wagalo.

Sadick Said anayependa kwenda uwanjani na vijana wake wawili wa miaka 4 na 10 anasema anazingatia ulinzi na usalama wa watoto wake.

“Nao wanapenda mpira, siwezi kuondoka nikawaacha, hivyo huwa nazingatia sana usalama wao, namkatia tiketi mkubwa ili asipate tabu, tukitoka nyumbani wanakuwa wamekula na kushiba.

“Changamoto ni pale ikitokea kuna msongamano wa kuingia, kupambana na watoto wawili si kazi ndogo, labda tungepewa kipaumbele kama ilivyo kwenye maeneo mengine yanayotoa huduma,”

Pascal Msafiri (7), Muhsini Omary (8) na Majid Ali (9) wakazi wa Vetenari wamedai kuwa wamefika uwanjani kwa ruhusa za wazazi na walezi kwenda uwanjani licha ya kutofanikiwa kuingia kwa sababu ya kukosa watu wa kupita nao getini.

“Kila mmoja amemuaga mzazi wake na tuliwaambia tutarudi mapema saa 11 jioni kwani huwa tunakuja uwanjani mara kwa mara wenyewe na wanaturuhusu kufanya hivi,”anasema Pascal kwa niaba ya wenzie.

Mtoto mwingine Rahma Kassim (2) ambaye alikuwa na mzazi wake alipoulizwa kama amekula mchana alijibu hapana na huo ulikuwa ni muda wa saa 8 mchana.

Mtoto mwingine, Furaha Bright (13) anasema huwa anapenda kwenda uwanjani kutokana na amsha amsha ya wazazi wake.

“Nikishafika uwanjani,  baada ya saa moja nachoka kwa kelele na wakati mwingine kuna msongamano na njaa inauma hakuna chakula,” anasema.

Changamoto Zinazowakabili watoto viwanjani

Msongamano wa watu ni moja ya changamoto kubwa zinazowakabili watoto katika viwanja vya michezo. Wakati wa kuingia na kutoka uwanjani, kuna hatari ya kukanyagana au hata kubanwa kwenye msongamano.

 Jesca Daud (11), mwanafunzi wa darasa la tano, anaeleza changamoto anayopitia anapopelekwa uwanjani na mama yake kwenye mechi za dabi.

“Kama leo, tumekuja saa 5 asubuhi kusubiri mechi ya usiku. Napenda Simba hivyo huwa nafurahia kuja,” anasema Jesca.

Hata hivyo, anasema changamoto kubwa ni pale anapochelewa kulala baada ya kutoka uwanjani usiku, jambo linalomuathiri kwenye masomo yake siku inayofuata.

Athari za kisaikolojia na kimwili ni kubwa zaidi kwa watoto wanapokuwa katika mazingira yasiyo salama.

Daktari Bingwa wa Masikio kutoka Hospitali ya Aga Khan, Ali Jaffer, anaeleza kuwa kelele nyingi viwanjani zinaweza kuathiri misuli ya sikio la mtoto na kusababisha matatizo ya usikivu.

“Athari hizi haziwezi kuonekana kwa kipindi kifupi, lakini zinaweza kujitokeza baadaye maishani,” anasema Dk. Jaffer.

Anashauri wazazi kutumia vifaa vya kuzuia kelele (earplugs) kwa watoto wao wanapowapeleka viwanjani.

Pia, mazingira ya usafi viwanjani yanaacha mengi ya kutamaniwa. Uchunguzi wetu ulibaini kuwa mara nyingi, viwanja vya michezo havina huduma bora za vyoo, hali inayosababisha wazazi wengi kuwa na hofu kuhusu afya ya watoto wao.

Ashura Juma, mkazi wa Keko, anasema kuwa huwa hawaruhusu mtoto wake kutumia vyoo vya uwanjani kwa sababu ya hali duni ya usafi. “Siwezi kuruhusu mwanangu ajisaidie kwenye vyoo hivyo. Kwa hali ilivyo ni rahisi kupata magonjwa,” anasema Ashura.

Athari za Afya kwa Watoto

Daktari wa Watoto, Suleiman Kimatta, anaonya kuwa watoto wanaoletwa kwenye viwanja vya michezo wanakabiliwa na hatari ya kupata magonjwa yanayoenezwa kwa urahisi kwenye mikusanyiko mikubwa kama vile homa, mafua, na magonjwa ya njia ya mkojo. “Watoto wadogo kinga zao si imara kama za watu wazima, hivyo ni rahisi kwao kuambukizwa magonjwa ya njia ya hewa kutokana na msongamano uliopo kwenye viwanja,” anasema Dk. Kimatta.

Pia, anaongeza kuwa watoto wanaokaa kwa muda mrefu bila kula au kunywa maji wanaweza kuathiriwa kiafya, hususani wanapolazimishwa kutojisaidia kwa muda mrefu. “Watoto wanahitaji chakula cha mara kwa mara na maji ya kutosha. Kukaa kwa muda mrefu bila vyakula na vinywaji ni hatari kwa afya yao,” anaongeza Dk. Kimatta.

Muongozo wa watoto viwanjani

Meneja wa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Milinde Maona, amekiri kuwa kuna changamoto kubwa kwa watoto na wazee wanapoingia viwanjani, hususani kwenye mechi kubwa.

“Tunaendelea kufanya tathmini na tumeshaliona hili. Hatuna budi kuweka muongozo maalum kwa ajili ya kundi hili,” anasema Maona.

Muongozo huo unatarajiwa kubainisha umri wa watoto wanaoruhusiwa kuingia viwanjani na jinsi ya kuwashughulikia watoto walio chini ya umri wa miaka minne.

Maona anasema kuwa kuna uwezekano wa kuandaa geti maalumu kwa ajili ya watoto na wazee, ili kupunguza msongamano na hatari za ajali viwanjani.

Hata hivyo, anakiri kuwa ni vigumu kuweka jukwaa maalum kwa watoto katika uwanja wa Mkapa kutokana na changamoto za idadi kubwa ya mashabiki.

“Kuna wakati mashabiki wanaweza kuzidi hata idadi ya viti vilivyopo. Ni vigumu kuandaa jukwaa maalumu la watoto kwasababu hatuwezi kudhibiti idadi yao. Hata hivyo, tunapendekeza watoto wa chini ya miaka minne wasiletwe uwanjani kwenye mechi hizi kubwa,” anasema Maona.

Mazingira ya Usafi na Huduma za Chakula

Suala la usafi na huduma za chakula ni changamoto nyingine kubwa kwa watoto viwanjani.

Wakati wa mechi kubwa kama ile ya nusu fainali ya Ngao kati ya Simba na Yanga, Uwanja wa Benjamin Mkapa ulikuwa na hali mbaya ya usafi, hususani kwenye vyoo.

Mwananchi ilishuhudia vyoo vikiwa na maji yaliyotapakaa, hali iliyowalazimu wazazi kuwazuia watoto wao kutumia vyoo, hivyo na badala yake kutumia njia mbadala zisizo salama kama kujisaidia kwenye chupa.

Kuhusu hili Maona, anakiri kuwa usafi wa vyoo ni changamoto kubwa, hususani wakati wa mechi kubwa.

“Tunajitahidi kufanya usafi mara kwa mara, lakini bado changamoto ni kubwa kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaotumia vyoo kwa wakati mmoja,” anasema Maona.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ukarabati wa vyoo, lakini bado mazingira hayako rafiki kwa watoto.

Ashura Juma, mzazi anayekwenda na binti yake wa miaka sita uwanjani, anasema: “Kwa hali ilivyo siwezi kumruhusu mwanangu ajisaidie kwenye vyoo vya uwanjani.Huwa namwambia ajisaidie kwenye chupa kisha namwaga na nikitoka naye nyumbani nataka awe amejisaidia kabisa,” anasema Ashura.

Huu ni utaratibu ambao wazazi wengi wamejiwekea kwa sababu ya hofu ya watoto wao kupata magonjwa.

Tiketi za watoto na udanganyifu

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo anasema utaratibu wa kuwa na tiketi maalumu kwa ajili ya watoto kwa hapa nchini bado ni mgumu.

“Tuliwahi kujaribu kuweka utaratibu huo lakini tukakutana na changamoto ya udanganyifu kwa kuwa hakukuwa na mfumo uliobaini tiketi ya mtoto na mkubwa,” anasema Kasongo.

Anasema wapo ambao walikuwa wananunua tiketi za watoto hivyo ili kuwa ngumu kumbaini ni mtoto kweli hivyo kutokana na usumbufu waliamua kuondoa utaratibu huo.

Kutokana na hali hiyo kuleta usumbufu utaratibu wa sasa ni watoto kuingia bure huu wakiangalia utaratibu mzuri wa wao kuwa na tiketi zao.

Uwanja huo unaingiza mashabiki 60,000 wakiwa wamekaa lakini inapotokea mechi kubwa mashabiki wanapitiliza kwa kuwa wapo wanaoingia na watoto ambao hawalipi na kutokuingizwa kwenye idadi ya mashabiki walioingia siku husika.

Utaratibu wa watoto Old Trafford

Utaratibu wa watoto kuingia uwanjani hata kwenye uwanja maarufu wa soka Old Trafford wa Manchester United, wana utaratibu wao wa jinsi ya kuhakikisha watoto wanaingia uwanjani na kuwa salama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye mtandao wao inasema:” Kila mtoto ambaye anaingia uwanjani ni lazima awe na tiketi maalumu ya mtoto, lakini pia hatushauri sana watoto wadogo sana waje uwanjani lakini kama itakuwa kuna ulazima ni vyema utaratibu huu ukafuatwa.

“Kama ni lazima kuja na mtoto lazima awe na Headphone ambazo zimezuia sauti kubwa kuingia kwenye masikio yao, lakini pia lazima mzazi atafute siti ambayo ipo umbali wa zaidi ya mita 20 kuanzia kwenye siti ya kwanza ili kumlinda mtoto asipigwe na mpira ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa.

“Tunashauri mzazi anayekuja na mtoto uwanjani, basi ajitahidi kuwahi na kumzungusha mtoto sehemu kubwa za uwanja ili azifahamu na baada ya mchezo tunashauri,wazazi walio na watoto wawe wa mwisho kutoka uwanjani.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa kila mzazi anatakiwa kuwa na jukumu la kumlinda mtoto wake kwa nguvu kubwa na kama kutakuwa na tofauti basi aombe msaada wa walinzi uwanjani.

“Kwa ushauri kama kuna mzazi anahisi mtoto wake anaweza kupotea basi ni vyema akaje naye uwanjani akiwa na nguo yenye mifuko na amwekee kadi maalum yenye taarifa muhimu mfukoni ili walinzi wakimkuta wapate urahisi wa kumpata mzazi.

Kuhusu mtoto kwenda mwenyewe

“Kwa mujibu wa taarifa ya Old Trafford hakuna mtoto chini ya miaka 16 anayeweza kukata tikei mwenyewe bila usaidizi wa mzazi wake, hivyo mtoto lazima awe na msimamizi ambaye ni miaka 16 na zaidi.”

Related Posts