ACHA niwe mkweli tu kwamba tangu mwanzo niliamini binafsi timu yetu ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya 33 ya Olimpiki huko Paris, Ufaransa iliyomalizika Jumapili ya wiki iliyopita ilikuwa dhaifu sana, kiasi haikuwa na uwezo wowote. Sio tu wa kushinda medali, bali hata ile chembe ya kutia kishindo cha maana kwenye michezo hiyo mikubwa kuliko yote duniani.
Nasema hivi kwa kuwa nimekuwa karibu na michezo ya Olimpiki kwa kipindi kirefu kiasi cha kujua vyema dira na mwelekeo wake katika jukwaa la ushindani. Nilianza kuifuatilia michezo hii kwa karibu nikiwa bado shuleni mwaka 1968 wakati huo kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki michezo iliyofanyika Mexico City.
Pamoja na kuwa wanagenzi, lakini Tanzania ilivuma sana katika michezo hiyo, sio kwa kunyakua medali, bali kwa sababu mmoja wa wanamichezo wake, John Stephen Akhwari, mbali ya kumaliza wa mwisho kabisa mbio za marathoni alijinyakulia sifa lukuki baada ya kujikongoja huku mguu ukiwa umefugwa bandeji kumalizia mbio hizo, ambaoo aliwasili eneo la kumalizia wakati watu wote wamekwishaondoka uwanjani. Kitendo hicho hadi leo kimempatia sifa kubwa mzee huyu na kumfanya kuingia katika historia kwa kuelezwa kuwa huo ndio moyo halisi wa ushindani wa michezo ya Olimpiki.
Miaka minne baadaye, 1972 nilikuwa tayari ni Mtangazaji wa Michezo wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kukatokea wazo kwamba nami niwemo katika timu ya Tanzania iliyokwenda Munich, Ujerumani kwa michezo ya mwaka huo ya Olimpiki. Nilifurahi sana. Lakini, kwa sababu ambazo baadaye wakuu wangu hawakuweza kuziweka wazi safari yangu hiyo ilivunjika.
Hata hivyo, michezo hiyo ya Munich ikawa maarufu sana mwaka huo, sio kwa matokeo ya viwanjani, bali kwa mauaji ya kigaidi ya wanamichezo 11 wa Israel yaliyofanywa na kikundi kilichojulikana kama Black September.
Michezo iliyofuata ilikuwa ya miaka minne baadaye. Ni kipindi hiki cha kati ya miaka ya 1970 na 1980 ambacho wadadisi wa historia ya michezo Tanzania wanakiita kipindi cha dhahabu.
Wanamichezo wa Tanzania walitamba katika majukwaa na viwanja mbalimbali vya michezo. Iwe katika kandanda, ngumi, riadha, netiboli, mpira wa mikono, kikapu na kadhalika.
Nilipata bahati ya kuandamana na baadhi ya timu hizi hasa katika mashindano na nchi nyingine barani Afrika ambapo ubora wa wanamichezo wa Tanzania ulikuwa bayana. Wakiingia popote walikuwa wakiheshimiwa. Wakifahamika kwa uwezo mkubwa na ubora wao wa kushindana.
Kifungua mimba cha mafanikio hayo ni mwaka 1973 katika michezo ya Afrika (All Africa Games) iliyofanyika Lagos, Nigeria, ambapo kilitokea kile ambacho hakuna mnajimu yeyote angeweza kukibashiri. Mfalme wa mbio za kati katika riadha duniani alikuwa Kipchoge Keino wa Kenya. Huyu jamaa alitisha kwa maana halisi ya kutisha. Olimpiki zake za kwanza kushiriki zilikuwa zile zilizofanyika Tokyo, Japan 1964 ambapo aliambulia patupu, licha ya kutoa upinzani wa nguvu akiingia fainali ya mbio zote alizoshiriki. Baada ya hapo Kipchoge akawa moto wa kuotea mbali akishinda kila mbio alizoshiriki.
Akanyakua medali ya dhahabu katika Olimpiki za Mexico City 1968 na vilevile kunyakua medali nyingine ya dhahabu Olimpiki za Munich 1972. Hii ni pamoja na kutamba karibu katika mbio nyinginezo duniani ikiwa ni pamoja na michezo yote aliyoshiriki ya Jumuiya ya Madola.
Sasa mwaka huo wa 1973 Keino aliwasili Lagos katika michezo ya Afrika akiwa anajiamini kupindukia. Alijua ataondoka huko akiwa ametia kibindoni medali nyingine ya dhahabu. Hivyo ndivyo alivyojua hadi pale alipopatiwa kile ambacho mzee huyu wa miaka 84 sasa, bado anakielezea ulikuwa ni mshtuko mkubwa kuwahi kutokea maishani mwake.
Kipchoge hakutaka kujua wala kusikiliza majina ya washidani wenzake katika fainali ya mbio za mita 1500 kwenye michezo hiyo. Alikuwa na haraka tu ya kubeba kile alichoona ni haki yake, medali ya dhahabu.
Wala hakutaka kumsalimia au angalau kumtazama tu, kijana mwembamba, mrefu wa kadri, maji ya kunde aliyekuwa amevaa fulani yenye michirizi ya bendera ya Tanzania kifuani. Alichojua alikuwa ni kijana mdogo tu kwake.
Naam kijana huyo alikuwa ni Filbert Bayi wakati huo akiwa na umri wa miaka 20. Nilimfahamu Bayi mwaka mmoja hivi kabla ya mashindano hayo ya Lagos. Jumamosi moja mnamo 1972 nilikwenda Kibaha Secondary kwenye kambi ya wanariadha wa taifa kurekodi kinachoendelea huko.
Nilipofika uwanjani pale nilistushwa na mbio za kasi mno ambazo nilikiri kimoyomoyo kwamba sijawahi kuona binadamu akikimbia kasi hivyo, tena hayo yakiwa ni mazoezi tu. Alipotulia kijana yule nilimfuata, nikajitambulisha kwake, “Mimi ni Tido Mhando wa RTD”.
Naye akanijibu kwa sauti ya upole, lakini yenye kujiamini sana; “Nakufahamu nami ni Filbert Bayi.” Na huo ukawa mwanzo wa uhusiano mkubwa baina yangu na mwanariadha huyo bora zaidi ya wote kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Sasa miezi kadhaa baadaye katika fainali zile za mita 1500 kule Lagos Nigeria, Bayi akakutana na Keino. Duh! Akiwa bado hajajua kinachoendelea bunduki ikalia kuashiria kuanza kwa mbio hizo za fainali za mita 1500. Bayi akaamua kuchomoka kama mshale kama vile nilivyomuona siku ile mazoezini Kibaha. Akajisemea kimoyomoyo, liwalo na liwe mwenye uwezo wa kunifuata anifuate.
Mwanzoni Kipchoge alidhani kijana yule wa Kitanzania alikuwa akifanya utani, lakini hadi kengele ya kuashiria mzunguuko wa mwisho wa mbio hizo ilipopigwa Bayi alikuwa tayari mbali sana, na wala hakuonyesha dalili za kuchoka.
Keino akaanza kuhaha. Uwanja wa Lagos ukalipuka kwa mayowe. Kijana mbichi wa Kitanzania, Filbert Bayi amemwangusha mbabe wa riadha duniani, Kipchoge Keino. Dunia ikashtuka, kulikoni?
Keino akatangaza kujiuzulu na kustaafu riadha kabisa. Kwake Bayi huu ukawa mwanzo mpya na maisha mapya ya umaarufu mkubwa duniani kuwahi kumpata mwanamichezo yeyote wa Kitanzania.
Na huu ukawa mwanzo wa kile kipindi cha dhahabu cha wanamichezo wa Tanzania, kwani miezi michache tu baadaye nilibahatika kuandamana na timu ya taifa ya Tanzania ya kandanda (Taifa Stars) kwenda Uganda kushiriki mashidano makubwa ya soka siku hizo kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati zikiwemo Malawi, Zambia, Uganda, Kenya na Tanzania. Ni mashindano ya Kombe la Chalenji.
Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza nje ya Tanzania halafu ikawa ni kwenda Uganda ikiongozwa wakati huo na Idd Amin Dada. Wakati wote wa mashindano hayo, kiongozi huyo wa kijeshi alikuwa hakosi kuja uwanjani Nakivubo na zaidi akipendelea pia kupitia katika sehemu yetu ya kutangazia mimi na mwenzangu Hayati Mshindo Mkeyenge.
Zaidi alitutania kwa Kiswahili. Kwa kukufahamisha tu hiki ndicho kilikuwa kipindi cha chokochoko baina ya Tanzania na Uganda ambapo miezi michache baadaye vita halisi vya Kagera baina ya Tanzania na Uganda vikaanza.
Sasa ni nini kilitokea uwanjani Nakivubo? Jibu langu ni kwamba kikosi cha kina Sunday Manara, Abdallah ‘King’ Kibaden, Mohamed Bakari ‘Tall’, Gibson Sembuli, Adam Sabu, Omar Zimbwe, Mweri Simba, Maulid Dilunga, Willy Mwaijibe, Hassan Gobbos na wengine wengi acha tu. Haikuwa masihara. Tulifika fainali na baadaye kufungwa kwa tabu na wenyeji Uganda, mbele ya Idd Amin kwa mabao 2-1.
Januari 1974 ukawa mwaka mwingine uliokuwa umejaa msisimko mwingi wa kimichezo, lakini jambo moja kubwa likatokea. Huo ulikuwa mwaka wa michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, Newzealand. Niliongozana na kikosi cha Tanzania cha wanamichezo kiasi cha 35 hivi. Kwa jinsi ilivyokuwa wanamichezo wote waliandaliwa vizuri na mwishowe wote tukapewa sare nzuri na kila kitu kingine muhimu kwa safari hii.
Kwenye sherehe ya ufunguzi vijana wa timu ya Tanzania walipendeza, hivyo kuwapa kiburi na jeuri ya kutaka kushinda. Michezo ya Madola inafanana sana na ile ya Olimpiki. Katika timu hii kulikuwepo wapanda baiskeli, mabondia, vinyoya (badminton), table tennis, riadha na kadhalika. Lakini pamoja na kuwepo kwa michezo mingi dunia nzima mwaka huo ilikuwa inasubiri kwa hamu mchezo mmoja, mbio za fainali za mita 1500.
Baada ya kumshinda Keino kule Lagos watu walitaka kuona kama Bayi ataweza pia kuwamudu wanariadha wengine wawili maarufu duniani Wakati huo John Walker wa New Zealand na Ben Jipcho wa Kenya. Walker ndiye aliyekuwa akishikilia rekodi ya dunia ya mbio hizo wakati huo.
Kwa ajili ya umaarufu wake mchezo huo wa mbio za mita 1500 ukawekwa kuwa wa mwisho kwenye ratiba ya michezo. Ilikuwa Jumamosi ya kijua cha wastani katika Uwanja wa Michezo wa Queen Elizabeth, Christchurch ulipofurika. Na baada ya michezo mingine michache ya riadha iliyobakia kumalizika wakati uliokuwa ukisubiriwa ukafika.
Nilimuona Bayi akiingia uwanjani kwa kujiamini. Alitupa matumaini makubwa, ingawa Watanzania wote tuliokuwepo hapo tulikuwa na hofu mno. Nilifuatana na mwandishi wa habari mwenzangu Steven Rweikiza kutoka magazeti ya Daily News, lakini tulikuwa kimya.
Macho yote yalikuwa kwenye kundi la wanariadha wanane waliojipanga uwanjani. Newzealand walimshangilia sana mwanariadha wao, Walker, mtoto wa nyumbani.
Mara bunduki ikalia na kama kawaida yake Bayi akafyatuka kama risasi. Ni kama aliyekuwa anasema mwenye uwezo anifuate. Naam Walker na Jipcho wakaanza kumkimbiza. Hofu ikaniingia. Nilifumba macho. Nikitetemeka. Nilipofungua macho Bayi alikuwa bado akiongoza, ila wawili wale wakiwa wanapambana wao kwa wao na huku wakimfukuza Bayi. Nilifumba tena macho. Uwanja ulikuwa unalipuka kwa mayowe. Nilipofungua (macho) Bayi alikuwa anakaribia kumaliza ila Walker naye alikuwa anamkaribia sana, vivyo hivyo Jipcho. Kila mtu uwanjani alisimama mara lahaula Bayi akawa amemaliza muda wa dakika 3:32:2 aliotumia ukawa ni rekodi mpya ya dunia. Amemshinda Walker tena nyumbani kwao na kuivunja rekodi yake iliyokuwepo kwa muda wa miaka saba.
Ulikuwa wakati wa fahari kubwa kwetu Watanzania tuliokuwepo uwanjani pale. Ghafla nilimuona Bayi akija mahali nilipokuwa na kuwakimbia waandishi wengine wa habari waliokuwa wanamfuata. Alitaka kuzungumza nami kwanza. Tukakumbatiana. Machozi ya furaha yakanitoka wakati Bayi akivishwa medali yake ya dhahabu. Bendera ya Tanzania ikapandishwa na wimbo wa taifa wa Tanzania kupingwa.
Umati wa Watanzania kwa maelfu ambao haujawahi kutokea walikuja kutupokea uwanja wa ndege wakati tuliporejea nyumbani. Wengine kwa maelfu walijipanga barabarani. Ni miaka 50 kamili sasa tangu historia hii kuandikwa, lakini hakuna kijana mwingine yeyote wa Kitanźania hadi leo aliyeweza kufanya kile ambacho Bayi alikifanya mwaka 1974.
Tatizo ni nini? Wakati kule Kenya ya Jipcho, vijana wanazivunja rekodi za dunia kama wanachezea gololi. Nchini New Zealand, mzee Walker mwenye umri wa miaka 72 sasa ametunukiwa heshima ya juu ya taifa. Sasa ni Sir John Walker.
Katika makala ifuatayo nitaeleza kuhusu Mwalimu Nyerere na Olimpiki za 1976 Montreal, Canada. Itaendelea…Usikose!