Waziri Gwajima atoa neno kauli ya RPC Dodoma binti aliyebakwa, kulawitiwa

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuwa watulivu kuhusu mwenendo wa washtakiwa wa kesi ya ‘waliotumwa na afande’, huku akiahidi haki itatendeka.

Agosti 4, 2024 ilisambaa video katika mitandao ya kijamii ikionyesha vijana watano wakidaiwa kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile binti anayedaiwa kuishi Yombo, Dar es Salaam,  huku wakimtaka kumwomba samahani ‘afande’.

Msingi wa kauli ya Waziri Gwajima ni kutokana na taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya aliyoitoa jana Agosti 18, 2024 alipozungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo.

Kamanda Mallya alisema: “Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”

“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo” alisema kamanda huyo.

Akijibu katika habari hiyo iliyochapishwa katika ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, Waziri Gwajima amesema; “Ndugu wananchi, nimepokea ‘Tags’ nyingi za maoni na maswali kuhusu taarifa iliyotolewa na RPC Mkoa wa Dodoma juu ya mwenendo wa shauri la ‘Binti wa Yombo’ (reja taarifa za awali).

“Ndugu wananchi, nimepokea hisia zenu, maoni na maswali yenu ambayo mmeelekeza kwangu. Nimewasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye tayari naye amepokea na anafanyia kazi, hivyo tumpe nafasi atatoa taarifa yake,” amesema Gwajima.

Waziri Gwajima ameongeza kuwa ni Dhahiri alichofanyiwa ‘Binti wa Yombo’ ni kitu kibaya kisicho cha utu, hivyo anastahili haki yake kwa mapana yote.

“Ndugu wananchi, nawasihi tujipe muda na kuamini kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na itaonekana bayana na si vinginevyo,”amesema Waziri Gwajima.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Agosti 9, 2024 na msemaji wake, David Misime ilieleza video hiyo ilianza kusambaa Agosti 2, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti msichana mmoja wakidai kuagizwa na afande.

Amewataja waliokamatwa kwa kosa la kumlawiti na kumbaka binti huyo ni Clinton Damas maarufu kama Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.

Misime alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa ya Dodoma na Pwani, huku jeshi hilo likiendelea kuwasaka watuhumiwa wawili ambao hawajapatikana mpaka sasa.

Related Posts