STEVE NYERERE ATAKA HATUA KALI KWA WANAODHALILISHA WATOTO WA KIKE – MWANAHARAKATI MZALENDO

Msanii maarufu Steven Nyerere ametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wa kike, akisisitiza kuwa haki na utu wa binadamu lazima vilindwe kwa gharama yoyote.

Kupitia ujumbe aliouandika, Steven Nyerere alieleza kutoridhishwa kwake na majibu mepesi yanayotolewa kuhusiana na matukio ya udhalilishaji wa watoto wa kike. Alisisitiza kuwa ni muhimu kutoa adhabu kali itakayokuwa fundisho kwa wengine, akieleza kuwa haikubaliki kamwe kuona mtoto wa kike anafanywa kama wa majaribio bila idhini yake.

“Haikubaliki kuona mtoto wa kike anakuwa wa majaribio bila idhini yake kamwe. Haiwezekani, lazima ipatikane adhabu ambayo itakuwa mfano kwa wengine. Haki isimame kwenye utu wa mtu, na dhamira kwenye taifa hili ni kulinda utu wa mtu kwa gharama yoyote ile,” aliandika Nyerere kwa msisitizo.

Aidha, Steven Nyerere alitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa za kuwajengea watoto wa kike heshima, uhuru, na fursa za kujikwamua kimaisha. Alisema kuwa Rais Samia amefanya mengi kumjengea mtoto wa kike ujasiri na kujiamini, hivyo ni muhimu kulinda thamani yao kwa uangalifu mkubwa.

Nyerere aliomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika wote wa vitendo vya udhalilishaji, akisisitiza kuwa watangazwe hadharani na kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine. “Mtoto wa kike thamani yake haielezeki, basi ilindwe kwa gharama yoyote ile,” alihitimisha Steven Nyerere kwa uchungu.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts