Dar es Salaam. Maswali tata yamegubika kutokana na mwenendo wa uchunguzi wa tukio la kubakwa na kulawitiwa kwa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam, baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theropista Mallya kufafanua kuhusu hatua za uchunguzi huo.
Maelezo ya kamanda huyo yaliyoibua maswali ni kuhusu vijana hao kutotumwa na afande, lakini aliwataja walikuwa kama walevi na wavuta bangi, huku binti akidaiwa kama alikuwa akijiuza ‘kahaba.’
“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”
“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo,” alisema Kamanda Mallya.
Ufafanuzi wa Kamanda Mallya alioutoa katika mazungumzo yake na Mwananchi jana Jumapili Agosti 18, 2024 lililotaka kujua kinachoendelea kwa watuhumiwa hao. Ufafanuzi huo umehojiwa na wadau wakiuliza, ukahaba wa binti huyo unahalalisha kubakwa au kulawitiwa?
Maswali hayo yameibuliwa leo Jumatatu, Agosti 19, 2024 na Wakili Peter Madeleka alipozungumza na Mwananchi baada ya majibu ya polisi.
Licha ya madai ya polisi kuwa binti huyo alikuwa anafanya biashara ya ngono ‘Ukahaba’, Madeleka amehoji jambo hilo linahalalisha kubakwa au kulawitiwa?
Swali lingine lililoibuliwa na wakili huyo ni ukahaba alionao binti huyo unamnyima haki ya uraia, kulindwa na kuhakikishwa usalama wake na vyombo vya dola?
Kadhalika, amehoji kilichoelezwa na Kamanda Mallya kuwa waliohusika ni walevi na wavuta bangi Je, sifa hizo zinawapa uhalali wa kutenda tukio hilo na hawaruhusiwi kukamatwa?
Kwa mtazamo wa jumla, wakili huyo amesema kilichozungumzwa na jeshi hilo hakina mashiko ya kisheria na ni uthibitisho aliyezungumza hastahili kuendelea kuwa kiongozi ndani ya Jeshi la Polisi.
“Ni kauli ya kibaguzi kwamba anayefanya biashara ya ngono anastahili kubakwa na kulawitiwa,” amesema Madeleka.
Watu maarufu nao hawakuwa nyuma kutoa maoni kuhusu kauli hiyo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), Msanii wa Muziki wa HipHop, Frida Amani ameandika: “Yaani tuone mtu akibakwa halafu tuambiwe aliyebakwa alikuwa anajiuza?
“Kwa nini tutafute njia ya kuonyesha alichofanyiwa ni sawa jamani! Hii leo imeniuma sana,” ameandika Frida.
Maoni hayo yanayofanana na yaliyoandikwa na mjasiriamali na mwanaharakati wa haki za binadamu, Carol Ndosi aliyeandika tukio lililofanywa kwa binti huyo la kinyama.
“Wanaojaribu kulirahisisha na kuwatengenezea njia wale vijana na waliomtuma wasiwajibishwe, ni wanyama zaidi. Tujuane kama Taifa,” ameandika.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi ameandika Polisi haina mamlaka ya kuchambua ushahidi na kuhitimisha bila kuwapeleka mahakamani.
“Polisi imegeuka Mahakama inaamua kesi yenyewe, polisi haina mamlaka ya kuchambua ushahidi na kuhitimisha bila kupeleka mahakamani. Polisi is gaslighting us makusudi kabisa, mnatuchochea,” ameandika.
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Tito Magoti ameandika kulinda wahalifu sababu ya ushirika wao na Serikali ni kuutomasa utawala wa sheria.
“Jeshi la polisi kwa mara nyingine mmetukosea sana. Ni ‘kahaba,’ so what? Nyie ni Mahakama? Priority ni victimisation ya victim? Mna maslahi gani na ule uhalifu? Hamfai na mnalithibitisha hilo,” ameandika.
Maoni mengine yalimlenga moja kwa moja Kamanda Mallya, kama ilivyoandikwa na miriamah187 kupitia mtandao wa Instagram, ”Bahati nzuri wewe ni mama umezaa katika uzao wako una binti, kama huna wamo wa ndugu zako, tusema Amina Mwenyezi Mungu kama anasikia na kuona video inajieleza.”
Ameongeza video hiyo inajieleza, lakini haki inapindishwa bila huruma, jambo alilodai linatiwa woga.
“Kuna siku watu wataamka ipo siku. Siku zote maumivu yakikomaa unaingiza ujasiri, ipo siku,” ameandika.
Naye Mtangazaji wa redio, Dina Marios ameandika katika katika ukurasa wake wa Instagram akisema: “Jeshi la Polisi mjitathimini kwenye hili. Hivi mnatuonaje?”
“Kwenye hili kuna mtu analindwa, haiwezekani kwa akili zenu timamu mje na hizi “kama kama”
na binti mlisema mnae nyinyi na yupo mahali salama…yeye ndio kawaambia kuwa alikuwa anajiuza? hizi “kama” zimetokea wapi?
Alichoandika Dk Gwajima
Katika mtandao wa Instagram, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema tayari ameshawasilisha maoni ya wananchi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.
Amewataka wananchi wampe muda Masauni afanyie kazi maoni hayo, kisha atatoa taarifa.
Majibu yake hayo, amesema yametokana na kupokea maoni mengi ya wananchi wakionyesha hisia zao juu ya mwenendo wa upelelezi wa tukio hilo.
“Ndugu wananchi, ni dhahiri kuwa alichofanyiwa ‘Binti wa Yombo’ ni kitu kibaya kisicho cha utu, hivyo anastahili haki yake kwa mapana yote,” ameandika.
Hata hivyo, amewataka wananchi waendelee kujipa muda, kwani haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na itaonekana bayana na si vinginevyo.
Tukio hilo lilianza kwa kusambaa picha jongefu katika mitandao ya kijamii Agosti 2, mwaka huu likionyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Katika kipande hicho cha video, binti huyo alishurutishwa kumwomba radhi mtu aliyetajwa kuwa Afande na alisikika akifanya hivyo.
BaadayeAgosti 9, mwaka huu, Jeshi la Polis kupitia Msemaji wake, David Misime lilitangaza kuwakamata vijana wanne waliohusika na ubakaji huo na wengine wanne kwa kosa la kusambaza video hiyo.
Lakini, jana Kamanda Mallya amesema upepelezi wa tukio hilo umekamilika na wakati wowote jalada litafika kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.