Dar es Salaam. Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2o25 ilianza rasmi Ijumaa iliyopita kwa mchezo baina ya Pamba Jiji na Tanzania Prisons uliochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mchezo huo ulimalizika kwa timu hizo kugawana pointi moja moja baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya sare tasa.
Msimu mpya umeanza huku ukiwa na namba ndogo ya makocha wazawa ambao wanahudumu katika nafasi ya ukocha mkuu kwenye timu zao kulinganisha na ile ya wageni,
Kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi hiyo msimu huu, ni sita tu ambazo zina makocha wazawa na 10 zilizobakia zinaongozwa na makocha wa kigeni,
Timu zenye makocha wazawa ni Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Mashujaa, JKT Tanzania, KenGold na Fountain Gate.
Tanzania Prisons inanolewa na Mbwana Makata, Mecky Maxime (Dodoma Jiji), Mohammed Abdallah ‘Baresi’ (Mashujaa FC), Mohammed Muya (Fountain Gate), Fikiri Elias (KenGold) na Ahmad Ally wa JKT Tanzania.
Makocha 10 wa kigeni na timu wanazozinoa kwenye mabano ni Miguel Gamondi (Yanga), Youssouf Dabo (Azam), Fadlu Davids (Simba), David Ouma (Coastal Union), Abdihamid Moalin (KMC), Patrick Aussems (Singida Black Stars), Mwinyi Zahera (Namungo), Goran Kopunovic (Pamba), Francis Kimanzi (Tabora United) na Paul Nkata (Kagera Sugar).
Licha ya namba ndogo ya makocha wazawa katika Ligi Kuu msimu huu, bado wana nafasi ya kuthibitisha kuwa timu zilizowaamini na kuwapa fursa ya kuzinoa msimu huu hazijakosea na zilifanya hivyuo kwa vile wamestahili.
Wanapaswa kutumia vyema nafasi ambazo wamepata kufanya mambo makubwa na yenye thamani ya hali ya juu ili kukuza majina yao wenyewe lakini pia kubadilisha fikra hasi ambazo wadau wa mpira wa miguu Tanzania wamekuwa nayo juu yao hadi kupelekea viongozi wa klabu nyingi kujenga imani na kuwapa kipaumbele makocha wa kigeni na sio wazawa.
Yapo mambo ambayo wanapaswa kuyafanya na pia kuna wanayotakiwa kujiepusha nayo ili thamani zao ziweze kupanda na kupunguza au kuondoa ulazima wa viongozi wa timu zetu kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kusaka makocha nje ya hapa nyumbani.
Nidhamu ni jambo la msingi ambalo sio tu makocha wanapaswa kuwa nalo bali pia wanapaswa kulionyesha kwa muda wote ndani na nje ya timu.
Kwa kiasi kikubwa, nidhamu ndio itafanya kocha aheshimike au asiheshimike katika kazi yake.
Nidhamu inaweza kupimwa katika namna tofauti kama vile ya kuenda na muda katika utekelezaji wa program na shughuli za timu, mtindo wa uvaaji na hata uzungumzaji wake.
Kocha anayejiheshimu ni rahisi kufikisha ujumbe kwa wachezaji wake na maofisa wengine kwenye timu na ukapokelewa na kufanyiwa kazi kwa haraka kwa vile tayari anakuwa na mamlaka ya kuwawajibisha wakikosea kwa yeye mwenyewe kujitumia kama mfano bora mbele yao.
Lakini ikiwa kocha anashindwa kujiheshimu, ni vigumu kwake kuwawajibisha walio chini yake kwani anapoteza mamlaka mbele yao kwa vile yeye mwenyewe ameshapoteza haiba ya kiuongozi.
Kocha hapaswi kuwa mfano mbaya wa utovu wa nidhamu kwani ataigharimu timu kwa kukumbana na adhabu ambazo zitamfanya ashindwe kuipa timu huduma ya kiufundi kwenye mechi ya kimashindano lakini pia hasara ya fedha kutokana na faini ya fedha ambayo yeye mwenyewe au timu italipa.
Kingine ambacho makocha wazawa ambao wamepata fursa ya kuzinoa timu za Ligi Kuu msimu huu wanapaswa kukifanya ni kujiimarisha na kujiendeleza kimbinu mara kwa mara.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia na nyakati pia yamepelekea mchezo wa soka kukumbana na mabadiliko ya mara kwa mara ya kimbinu na kiufundi ambayo kocha anapaswa kwenda nayo sambamba ili timu yake iweze kumudu ushindani na kufanya vizuri vinginevyo atajikuta anajiweka katika hatari ya kuangusha pointi mara kwa mara jambo linaloweza kumfanya akumbane na janga la kutimuliwa.
Mbinu bora ambazo kocha atazitoa kwa wachezaji wake na kisha akawafanikiwa katika kuwawezesha wazitafsiri vyema ndani ya kiwanja zitawafanya wawe bora na hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuipa timu matokeo mazuri.
Na ukiondoa faida kwa timu, wachezaji wakizielewa vyema mbinu inafungua mlango wa kuzalisha makocha bora wa siku za usoni ambao nao watazalisha na kuibua vipaji vingi.
Hakuna kocha anayeibuka tu kutoka kusikojulikana, ni lazima atengenezwe kuanzia pale anapokuwa mchezaji ili iwe rahisi kufanyia kazo kitu alicho na uzoefu nacho.
Tumeona juhudi mbalimbali zikichukuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuhakikisha ubora wa makocha wazawa unaongezeka lengo hasa likiwa ni kuwawezesha kupambana katika soko la kiushindani na makocha wa kigeni.
Ili ziwe na matunda chanya zaidi ni muhimu makocha wenyewe wakaonyesha utayari na uungaji mkono kwa kujitahidi kujiweka katika hadhi ya juu ambayo itashawishi watu kurudisha imani kwao tofauti na hali halisi ilivyo hivi sasa ambapo wadau wengi wa mpira wa miguu wamekuwa na mitazamo hasi juu ya makocha wazawa.
Ni vyema msimu huu wa ligi ukatumika na makocha wazawa kufanya mageuzi na kuteka imani ya viongozi wa klabu kwao.