Jubilee yaja na kampeni elimu ya bima ya afya kwa Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Kutokana na uelewa duni wa wananchi kuhusu bima ya afya, Kampuni ya Bima ya Afya ya Jubilee imekuja na kampeni yenye lengo la kuongeza elimu na umuhimu wa matumizi ya bima.

Bima hiyo imezinduliwa leo Jumatatu Agosti 19, 2024 na ina kauli mbiu ‘Kuna kuishi na Kuishi Huru’ itakayoshirikisha nchi tatu za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Maisha ya Jubilee, Hellen Mzena amesema uelewa wa masuala ya bima nchini ni chini asilimia moja, hivyo watatumia kampeni hiyo kutoa elimu kwa Watanzania.

“Tumekuja na kampeni hii kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kukabiliana na changamoto za kiafya na za kimaisha bila shida yoyote,” amesema Hellen.

Pia, amesema kutokana uzoefu wa miaka 87 kwa Afrika Mashariki tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo, wanajua namna ya kumhudumia mteja na wamejikita kidijitali, kwani kwa sasa huduma nyingi zinapatikana kwa njia hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya Afya ya Jubilee, Dk Harold Adamson amesema kampeni walioanzisha itasaidia kutua mizigo ya kifedha na kiafya kwa Watanzania na itawapa fursa ya kujiunga na bima za afya ya kampuni yao.

“Masuala ya bima ya afya yameonekana kuwa ni kwa matajiri, watu wenye kipato fulani au waajiriwa pekee, lakini tunakuja mbele yenu kuwapatia fursa kupitia kampeni hii yenye lengo la kuwafikia Watanzania wote kwa vipato tofauti watakaoweza kufikiwa na kampeni hii,” amesema Dk Adamson.

Amesema wametumia neno la ‘Ishi Huru’ kwa kutafsiriwa kwa maana mbalimbali na Jubilee wametafsiri katika mawazo ya nini kitakachotokea endapo mtu atakapougua, mtoto atakaposhindwa kwenda shule kwa kukosekana ada na kujua wapi watu watawekeza na kuongeza kipato chao.

Hivyo, kupitia kampeni hiyo watu wengi watatambua na kupata uelewa wa afya na bima ya maisha.

Kuhusu changamoto zinazojitokeza katika masuala ya bima za afya, amesema wamekuwa na mazingira mazuri ya ufanyaji wa kazi na kuwa wabunifu baada ya kuwepo sera ya bima ya afya kwa wote na kuamaua kutengeneza bidhaa mbalimbali ili kuwafikia watu wa chini.

“Tumekuwa na bima ya afya ambayo mtu anaweza kulipia Sh300 kwa siku… hiyo ilitusaidia kuweza kumfikia mpaka mwananchi yule wa chini,” amesema.

Related Posts