Licha ya Coastal Union kufumuliwa mabao 3-0 katika mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na Bravos do Marquis ya Angola, kocha mkuu wa kikosi hicho, Mkenya David Ouma amesema bado hajakata tamaa na matokeo hayo akijipanga kupindua meza mchezo wa marudiano.
Coastal iliyorejea katika michuano ya kimataifa tangu mwaka 1989 ilikumbana na kipigo hicho ikiwa ugenini na kujiweka katika nafasi finyu ya kusonga mbele kwa raundi ya pili, kwani mchezo ujao wa marudiano itahitaji ishinde si chini ya mabao manne ili iwang’oe Waangola hao.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, kocha Ouma alisema, ni kweli matokeo ya juzi ni mabaya kwa timu hiyo iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, lakini bado anaona wana nafasi ya kusawazisha makosa watakaporudiana kwani wamegundua kilichowagharimu ugenini.
Ouma alisema timu yake iliangushwa na eneo la kiungo na mabeki wa kati ambao kwa kiasi kikubwa walikosa maelewano mazuri na kwamba wanaenda kufanyia kazi kabla ya kurudiana na Bravo wikiendi hii, jijini Dar.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa marudiano ingawa kama wao wameweza kushinda kwao kwa nini sisi tusishinde pia kwetu, kila kitu kinawezekana japo tunapaswa kuongeza umakini zaidi kuanzia katika kuzuia na kushambulia,” alisema Ouma.
Aliongeza, sababu nyingine iliyowafanya kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao ni kushindwa kuwasoma vyema wapinzani wao, hali ambayo ilikuwa ngumu kukabiliana nao japo amechukua kama funzo la kujirekebisha katika mchezo wa marudiano.
“Ilituchukua muda sana kuwasoma wapinzani wetu kwa maana ya kuwajua wachezaji wao hatari, udhaifu, ubora na aina pia ya uchezaji, ila kama ambavyo nimesema hapo mwanzoni sisi kama benchi la ufundi tunaamini tutapindua matokeo nyumbani.”
Simba na Coastal ni timu ambazo zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu baada ya kumalizia nafasi ya tatu na nne msimu uliopita huku Yanga na Azam FC zikiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mara ya mwisho kwa Coastal kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza ambapo michuano hiyo iliunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004.
Timu hiyo kwa sasa inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao 4-0, katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Agosti 24, kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, na endapo itafuzu itakutana na FC Lupopo ya DR Congo hatua inayofuata.