R4 za Samia kutumika kusuluhisha migogoro ya kibiashara

Dar es Salaam. Taasisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara Tanzania (TIArb) imesema itatumia falsafa ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan katika utatuzi wa migogoro katika sekta ya ujenzi na uwekezaji kimataifa nje ya Mahakama.

Alipoingia madarakani Machi, mwaka 2021, Rais Samia alikuja na falsafa ya R4 zikiwa ni kifupisho cha maneno ya Kiingereza; Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga upya), akilenga kuleta maridhiano miongoni mwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 19, 2024 kwenye uzinduzi kongamano la wiki ya utoaji elimu hiyo, Makamu wa Rais wa TIArb, Aderickson Njunwa amesema elimu hiyo itatolewa kwa kushirikiana na wabobevu wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kama mdau mkuu.

“Tutatoa elimu kwa Watanzania wote kusuluhisha migogoro kwa njia mbadala ya Mahakama, na safari hii tutawaelimisha katika sekta ya ujenzi na uwekezaji wa kimataifa.

“Tumekuwa wadau wakubwa wa Mahakama, tumeona tutumie falsafa ya R4 ambayo hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiitumia kuwaelimisha Watanzania na kuwajengea uwezo,” amesema.

Njunwa ameeleza kuwa katika kongamano hilo la saba kufanyika tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, mbali na kuwakutanisha wabobevu kutoka Afrika Kusini na Pakistan, pia linalenga kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani na watendaji wa Serikali katika eneo hilo.

“Teknolojia inazidi kukua na mifumo ya usuluhishaji imekuwa ikibadilika na tutaelimisha namna bora ya kusuluhisha migogoro hiyo nje ya Mahakama na kujadili changamoto zinazojitokeza, ili kuboresha mazingira kwa ujumla,” amesema Njunwa.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara Dar es Salaam, Abdallah Gonzi ametaja kukosea kuandika mikataba na utekelezaji usio kuwa sahihi ni miongoni mwa maeneo makuu yanayoleta msigano mkubwa kiasi cha kushamiri migogoro mingi.

“Uandishi usiokuwa sahihi wa mkataba huwa unazaa migogoro mbele ya safari, tatizo lingine mkataba unaweza kuwa umeandikwa vizuri, lakini jinsi ya kuusimamia kiutekelezaji watu huwa wanashindwa,” amesema.

Amesema msingi wa makubaliano yeyote ni msingi wa kilichoandikwa kwenye mkataba na kama ukiandikwa vizuri hata msigano ukitokea wanarudi kuangalia katika maandishi.

Amesema Mahakama jukumu lake ni kupokea na kutatua migogoro na jambo hilo ni la kikatiba na kisheria pia ndani ya chombo hicho huwa wanaendeleza utaratibu wa migogoro itatuliwe kwa njia ya suluhu ya pande zote

“Kusuluhisha migogoro ni jambo la kikatiba na sheria inahimiza ndio maana hata kesi ikifunguliwa mahakamani, kuna utaratibu wa kesi zote wa kesi zote za madai kupitia katika suluhu na tuna kitengo mahususi cha usuluhishi migogoro,” amesema.

Wiki hiyo itakayokuwa mahususi katika utoaji wa elimu ya sekta ya ujenzi na uwekezaji wa Kimataifa,  imeanza leo Agosti 19, 2024 na wataalamu hao watakuwa wanatoa elimu kupitia vyombo vya habari na watafanya mikutano miwili ambayo Waziri wa Katiba na Sheria atakuwa mgeni rasmi.

Related Posts