TANZANIA KUANDAA MKUTANO WA MAONESHO YA 11 YA PETROLI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amehudhuria kikao cha maandalizi ya Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25), yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 5 hadi 7, 2025, katika Ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku tatu utafanyika chini ya kauli mbiu “Unlocking Investment in Future Energy: The Role of Petroleum Resources in the Energy Mix for Sustainable Development in East Africa” ambapo pamoja na mijadala na maonesho, kutakuwa na safari za kutembelea maeneo ya kijiolojia na vivutio vya utalii katika nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Mkutano huo utawajumuisha wadau zaidi ya 1,000 kutoka mataifa mbalimbali, watakaokuja kujadili masuala ya uwekezaji katika nishati safi na mchango wa rasilimali za petroli katika maendeleo endelevu ya nishati kwa kanda ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Biteko alisema, “Kama nchi, tumepata fursa ya kuandaa mkutano huu wa kimataifa, na Serikali imepanga kufanya hivyo kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuandaa mkutano wenye tija kwa nchi na kutoa nafasi kwa Watanzania kufaidika na uwepo wa mkutano huu.”

Alitoa wito kwa wahudhuriaji wa kikao hicho kutumia fursa ya mkutano wa EAPCE’25 kutangaza biashara, huduma, na utaalamu wao, pamoja na kujenga mitandao na washirika kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, alieleza kuwa mkutano wa EAPCE’25 utahusisha pia maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali, hivyo kutoa fursa kwa wadau kuchangamkia nafasi hiyo. Aliongeza kuwa udhamini wa mkutano huo utatoa nafasi kubwa ya kujitangaza ndani na nje ya nchi, kwa kuzingatia ukubwa wa tukio hilo.

Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya awali kuelekea Mkutano wa EAPCE’25, ambao unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya nishati na uwekezaji katika kanda ya Afrika Mashariki.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts