Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimehoji maswali 11 kutokana na kauli ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC), Theropista Mallya kuhusu uchunguzi wa tukio la kubakwa na kulawitiwa kwa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa maswali ambayo kituo hicho imejiuliza na kuhitaji majibu ni kuwa afande anayetajwa ni wa jeshi gani na kipi kinaendelea juu yake.
Tukio hilo linadaiwa kutendwa na vijana watano wanaodaiwa kutumwa na afande kutekeleza kitendo hicho. Kipande cha video, kilichosambaa mitandaoni kikionesha tukio hilo, kiliibua mijadala mikali maeneo mbalimbali.
Agosti 9, 2024, Jeshi la Polisi lilieleza kuwashikilia vijana wanne kati ya watano ambao ni Clinton Damas maarufu kama Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.
Polisi walisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa ya Dodoma na Pwani, huku jeshi hilo likiendelea kuwasaka watuhumiwa wawili ambao hawajapatikana hadi sasa.
Jana Jumapili, Agosti 18, 2024, Mwananchi lilimtafuta Kamanda Mallya kujua nini kinaendelea juu ya watuhumiwa hao ambapo alisema katika uchunguzi Jeshi la Polisi lilibaini vijana hao waliotuhumiwa kwa madai ya kutumwa, walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa.
“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”
“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo” alisema kamanda huyo.
Kauli hiyo ya Kamanda Mallya imeibua mijadala maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni wakitaka haki itendeke. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura amefanya mabadiliko madogo ya makamanda kwa kumpeleka George Katabazi kuwa RPC wa Dodoma, huku Mallya akipelekwa Makao Makuu, Dodoma.
Wakati hayo yakiendelea na mijadala kuhusu hilo, LHRC limeitisha mkutano na waandishi wa habari, makao makuu ya ofisi hiyo Kijitonyama, Dar es Salaam na kueleza kusikitishwa na kauli hiyo, huku wanajiuliza maswali mengi kuhusu Jeshi la Polisi tangu kuibuka kwa tukio hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga amesema pamoja na maswali hayo ni pamoja na zipi ni taarifa sahihi kutoka kwa jeshi hilo, za makao makuu, Wizara ya Mambo ya Ndani au makamanda wa Polisi wa mikoa wa Dar es Salaam na Dodoma.
Pili, watuhumiwa hao ni maofisa wa jeshi lipi. Tatu, watuhumiwa katika tukio hilo walikuwa watano, je huyo mwingine ni nani na yupo wapi. Nne, binti alilazimishwa kumuomba msamaha ‘afande’ je afande ni nani.
Tano, wanajiuliza kama mwathirika yupo salama katika mikono ya wanaomhukumu kuwa ni kama alikuwa anajiuza.
Swali la sita, binti huyo kuwa katika mikono ya polisi hakutaathiri upatikanaji wa haki na ushahidi na je mtu kuwa kama anajiuza inahalalisha kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa.
Saba, vipi binti huyo kuwa mikononi mwa polisi, je hakutaathiri upatikanaji wa haki na ushahidi. Nane, je kwa vitendo hivi, Jeshi la Polisi linasimamia maslahi ya nani?
Swali la tisa, Je, kuwa mlevi na mvuta bangi ni kinga ya uhalifu? Kumi, kwa kutajwa afande bila kusema ni afande wa jeshi gani, je polisi hawana mgogoro wa maslahi na shauri hili?
Swali la 11, LHRC wamehoji taarifa ya Polisi ya Agosti 9 ilisema upelelezi umekamilika na leo Agosti 19, je lini shauri hilo litapelekwa mahakamani?
Anna katika tamko lao hilo, amesema LHRC inawakumbusha kuwa kitemdo alichofanyiwa mwathirika ni cha kinyama, kikatili, kinyume na haki za binadamu na sheria za nchi na anyefumbia macho vitendo hivyo ni adui wa haki na utu.
“Pia LHRC inapenda kusisitiza yaliyotokea katika tukio hilo yalionyesha dhahiri hayakuridhiwa na binti huyo alishurutishwa, kutishiwa na kuteswa,” amesema Anna.
Wamelitaka Jeshi la Polisi kuacha kulinda na kutetea uhalifu, kwani kauli ya Kamanda Mallya ni wazi inatetea uhalifu uliofanyika.
Vilevile, imetaka Jeshi hilo kutoa nafasi kwa binti mhusika kupata huduma, ikiwemo ya ushauri nasihi kutoka kwa chombo ambacho hakina maslahi na shauri hilo.
Tukio lenyewe lolivyokuwa
Tukio la msichana huyo lilianza kwa kusambaa kwa picha jongefu katika mitandao ya kijamii Agosti 2, 2024 likionyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Katika kipande hicho cha video, binti huyo alishurutishwa kumwomba radhi mtu aliyetajwa kuwa Afande na alisikika akifanya hivyo.