MSIMU wa mashindano wa 2024/25 umeanza nchini Tanzania, kwa mashindano ya ndani na ya nje.
Kuanza kwa msimu ni kuanza kwa biashara zote zinazoambatana na mpira, ikiwemo ya viwanja vya kuchezea.
Na kama kuna uwanja umeanza kwa kishindo basi ni Azam Complex, uwanja wa nyumbani wa Azam FC, uliopo pale Chamazi.
Kwa siku tatu tu, Ijumaa ya Agosti 16, Jumamosi ya Agosti 17 na Jumapili ya Agosti 18 uwanja huo umefanya biashara kubwa kutokana na kutumika kwenye mechi za CAF za klabu.
Katika siku hizo tatu uwanja huo umetumika kwa mechi nne za CAF ikiwemo ya kwao wenyewe.
Ijumaa ya Agosti 16, Azam Complex ilihodhi mechi mbili za CAF, moja ikiwa ya Ligi ya Mabingwa na nyingine ya Kombe la Shirikisho. Timu zilizocheza zote kutoka nje ya Tanzania.
Kwanza kulikuwa na mchezo kati ya Arta Solar 7 ya Djibouti iliyowakaribisha Dekedaha FC kutoka Mogadishu, Somalia. Mchezo huo ulioanza saa 10 alasiri ulishuhudia wenyeji wakichapwa mabao 2-0.
Halafu ukaja mchezo mwingine wa Kombe la Shirikisho ulioanza saa tatu usiku, ukiwakutanisha Horseed FC ya Somalia na Rukinza FC ya Burundi.
Mchezo huo uliisha kwa sare tasa, yaani bila kufungana.
Jumamosi ya Agosti 17 kukawa na mchezo mmoja wa Vital’O ya Burundi dhidi ya Yanga ya Tanzania.
Wageni waliokuwa nyumbani, Yanga walishinda 4-0 dhidi ya wenyeji waliokuwa ugenini. Na Jumapili ya Agosti 18, wenye uwanja wao, Azam FC wakiwakaribisha APR kutoka Burundi.
Mchezo huu tuachane nao kwa sababu ni Azam wenyewe ndiyo walitumia uwanja kwa hiyo ni sawa na stori ya kuku wa bwana heri.
Tuangalie mechi zingine hizo tatu ambazo ziliichezwa Ijumaa na Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Azam FC iliyotolewa mwaka 2020 kuhusu gharama za kikosi uwnaja, Azam FC imevuna kiasi kikubwa hadi sasa kwa msimu huu.
Kwa timu za nje ya Tanzania, kukodi uwanja huo kwa ajili ya kuchezea mechi ni Dola elfu tano ambazo ni zaidi ya Sh12 milioni. Kwa mechi tatu tu, Azam Complex imeingiza jumla ya Dola elfu kumi na tano, ambazo ni takribani Sh40 milioni.
Bahati iliyoje kwa Azam Complex kwani katika mechi za mkondo wa pili, uwanja huo utaingiza tena kiasi kama hicho kwani timu zote hizo zitaendelea kutumia uwanja huo huo.
Unaweza kudhani kuna kitu kitachapungua kutokana na mchezo wa Yanga na Vita’O kwani timu za ndani ya Tanzania gharama yake kidogo imepungua ni Sh5.6 milioni.
Hata hivyo hiyo haitabadili kitu kwani Coastal Union nao watatumia uwanja huo, hivyo kufidia pengo la Yanga. Kwa hiyo badala ya ile milioni 40 kama mechi za mkondo wa kwanza, uwanja huo utaingiza takribani milioni 30.
Kwa hiyo hamna hamna, kwa mechi raundi ya awali tu, Azam Complex itakuwa imeingiza si chini ya Sh70 milioni.
Kubwa zaidi timu zote zilizocheza katika raundi ya ya kwanza ya awali, zitaendelea kuutumia uwnaja huo huo kwa mechi za raundi ya pili ya awali kwa zile zitakazofuzu.
Maana yake tena kuna takribani milioni 70 Azam Complex itaingiza. Na hii ni mwanzo tu wa msimu, maana yake huko mbele kutakuwa na mechi zaidi na zaidi za ndani na nje ya nchi.
Ama kwa hakika uwnaja wa Azam Complex ni kitega uchumi kinachoendelea kuimarika.
Soko la Azam Complex kimataifa lilianza mwaka 2020 wakati wa mlipuko wa Uviko 19 pale nchi zingi zilipoendelea kuwafungia watu ndani na kupataza kufanyika kwa shughuli za michezo huko Tanzania milango kuwa wazi.
Timu nyingi za kutoka nje ya Tanzania zikachagua kuchezea mechi zake uwanjani hapo na ndipo milango ikafunguka.
Septemba 16 2021, Azam Complex iliikusanya Afrika na kuileta Chamazi.
Siku hiyo timu sita kutoka mataifa matano tofauti barani zilifanya mazoezi kujiandaa na mechi za CAF, kwenye uwanja huo. Azam FC (Tanzania), Horseed SC (Somalia), Biashara United (Tanzania), Dikhil FC (Djibouti), Le Messager de Ngozi (Burundi) na US Gendermarie (Niger).
Gharama za kukodi uwanja wa Azam Complex kwa ajili ya mazoezi kwa timu kutoka nje ya Tanzania ni Dola elfu moja.
Uwanja wa mpira ni biashara kubwa sana, hasa kama menejimenti yake inajua kuandaa matukio.
Kuna mechi za mpira, kuna matamasha ya muziki, kuna mapambano ya masumbwi€haya yote yanaweza kuwa vyanzo vizuri sana vya mapato kwa mpira.