Mshtakiwa aiomba akutanishwe na mkewe wajadili mtoto wao kutokwenda shule

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kusafirisha kilo 3050 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine, Najim Mohamed (52), ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imkutanishe na mkewe ili wajadiliane kuhusu mtoto wao mdogo ambaye hajahudhuria shule tangu Machi 2024.

Mohamed amedai mtoto wao huyo anasoma darasa la sita na tangu Machi 2024 hadi sasa hajaenda shule.

Bila kutaja sababu ya mtoto wao kutokuhudhuria masomo, mshtakiwa huyo ameomba Mahakama imkutanishe na mkewe ambao wote wapo rumande wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Mbali na Najim, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mkewe Maryam Najim Mohamedi (50) pamoja na mfanyakazi wa ndani wa kiume, Juma Abbas (37).

Mshtakiwa huyo amewasilisha ombi hilo leo Jumatatu Agosti 19, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mohamed amefikia hatua hiyo, baada ya wakili wa Serikali, Frank Rimoy kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea.

Rimoy baada ya kueleza hayo, Hakimu Lyamuya amemuuliza mshtakiwa iwapo ana jambo lolote kuhusiana na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka kwa kuwa washtakiwa hawana wakili wa kumtetea.

Mshtakiwa huyo amedai ana jambo moja na kwamba anaomba kuliwasilisha mahakamani hapo. “Mheshimiwa hakimu nina jambo, nataka niongee na mwenza wangu, tujadiliane namna mtoto wetu kwenda shule.

“Nimepata taarifa, mtoto wetu mdogo anayesoma darasa la sita hajaenda shuleni tangu Machi mwaka huu hadi sasa, hivyo naomba Mahakama itupe nafasi ya kuonana ili tuzungumze jambo hili hata kwa njia video,” amedai Mohamed, ambaye yupo Gereza la Mahabusu Ukonga.

Mshtakiwa huyo amekwenda mbali zaidi na kudai majadiliano hayo hayatakuwa ya faragha na kama itawezekana wafanye kwa njia ya video conference kati yake na mkewe ambaye yupo Gereza la Mahabusu Segerea.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza ombi la mshtakiwa huyo, amemueleza tarahe ijayo, Mahakama hiyo itawaelekeza wataalamu wa Tehema ili waunganishe televisheni ziwe tatu na mshtakiwa aliyopo Segerea na Ukonga waonane na kujadiliana.

“Septemba 2, 2024, tutaunganisha screen tatu kwa ajili ya mawasiliano kwa njia ya video conference baina ya Mahakama, mshtakiwa aliyepo Gereza la Segerea na Ukonga ili mjadiliana jambo hilo, halitakuwa faragha,” amesema Hakimu Lyamula.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hadi Septemba 2, 2024 itakapotajwa.  Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video, huku washtakiwa hao wakiwa rumande.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanadaiwa Desemba 15, 2023, eneo la Kibugumo Shule lililopo Wilaya ya Kigamboni, washtakiwa hao walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 882.71.

Shtaka la pili, wanadaiwa siku na eneo hilo, walisafirisha dawa za kulevya aina ya methamphetamine zenye uzito wa kilo 2,167.29.

Related Posts