Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mkutano wa saa tatu kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ulikuwa mzuri.
Blinken anatazamiwa kusafiri kesho Jumanne kwenda Cairo, Misri ambako mazungumzo ya kusitisha mapigano yanatarajiwa kuanza tena wiki hii.
Soma Pia: Kamala Harris aashiria mabadiliko makubwa kwenye sera ya Marekani kuhusu Gaza.
Mkutano huo umefanyika wakati katika Ukanda wa Gaza wanajeshi wa Israel wakiendelea na mashambulizi zaidi katika mji wa Khan Younis.
Waandamanaji walikaa nje ya bunge la Israel mjini Jerusalem leo wakati Blinken alipokutana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Waandamanaji hao wanaitaka serikali yao ifikie makubaliano ya kuwarejesha mateka nyumbani.
Mwandamanaji mmoja aliyeshika bango lililosema, sitarajii chochote kutoka kwenye mkutano huu, kwa sababu waziri mkuu wetu anazuia mpango wa mateka kurejea nyumbani, alipoulizwa na waandishi wa Habari kwa nini anasema hivyo alijibu.
“Ninasikitika sana kusema hivi kwa sababu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anafanya juhudi nyingi kuufanikisha mpango wa kuwarudisha mateka, lakini serikali yetu inafanya kila kitu kuepuka hilo, kwa sababu tumo kwenye hali mbaya ya kisiasa hapa Israel.”
Wapatanishi, ikiwa ni pamoja na Marekani, wameonyesha matumaini mapya kuwa mpango wa kusitisha mapigano unakaribia kufikiwa. Lakini Hamas wameeleza kutoridhika na baadhi ya mapendekezo ya hivi karibuni ya Israel, imesema yapo maeneo ambayo haiko tayari kuyakubali.
Soma Pia: Vita vyaendelea Gaza, mchakato wa mazungumzo wakwama
Wakati huo huo, wapiganaji wa Kipalestina kutoka kwenye matawi ya Hamas na Islamic Jihad leo Jumatatu wamethibitihsa kuhusika na shambulio la bomu la jana jioni katika mji wa Tel Aviv, wakiita kuwa ni ”operesheni ya kujitoa mhanga.” Makundi hayo yametishia kufanya mashambulizi zaidi nchini Israel wakati vita vya Gaza vinapoendelea.
Shambulio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alipowasili mjini Tel Aviv kushinikiza kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza huku hofu ikiongezeka ya vita hivyo kuenea katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.
Kwingineko shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa limefuta safari zake za ndege kwenda na kutoka Tel Aviv, Tehran, Beirut, Amman na Erbil katika eneo la Kurdistan la Iraq kutokana na hali ya sintofahamu inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati hadi Jumatatu ijayo.
Vyanzo: RTRE/DPA/AFP