Dabo asaka dawa ya APR

KAULI ya Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo kuhusu wapinzani wake APR imeonekana kuwa na maswali mengi juu ya kitakachoenda kutokea katika mchezo wa marudiano jijini Kigali nchini Rwanda.

Juzi Jumapili Azam iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APR ya Rwanda katika mchezo wa kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, mfungaji akiwa Jhonier Blanco raia wa Colombia dakika ya 56 kwa mkwaju wa penalti baada ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufanyiwa madhambi na beki wa APR, Claude Niyomugabo.

Baada ya mchezo huo, Dabo alibainisha wazi kwamba wapinzani wake APR walikuja tofauti na alivyowasoma hapo awali hivyo ni kama ilikuwa sapraizi kwake licha ya kwamba walifanikiwa kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani na sasa wanajipanga kuhakikisha wanaenda Rwanda kutafuta matokeo zaidi na sio kujilinda.

“Tunahitaji kufanya kazi zaidi ya moja katika mchezo wa marudiano, kwanza ni kuhakikisha tunalinda bao letu lakini pia tusiwape nafasi ya kutushambulia mara kwa mara langoni kwetu kwa sababu tunatambua watatushambulia kuanzia mwanzoni,” alisema Dabo.

Azam imeanza vyema hatua ya awali ya michuano hiyo ikiwa nyumbani, lakini ina kibarua cha kulinda ushindi huo watakaporudiana Agosti Jumamosi ijayo Agosti 24, 2024 kwenye Uwanja wa Amahoro uliopo Kigali Rwanda ili kutinga hatua inayofuata ambapo mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya JKU ya Zanzibar iliyochapwa mabao 6-0 na Pyramids ya Misri.

Kuhusu mchezo wa juzi, Dabo ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Tulipoteza nafasi nyingi kipindi cha kwanza kwa sababu wachezaji walikuwa wanacheza kwa presha zaidi, ila nilikaa nao na kuwaelekeza watulie na wasiwe na wasiwasi, nashukuru tulipata bao ambalo tuliweza pia kulilinda hadi mwisho wa mchezo.”

APR iliyocheza dhidi ya Azam, ilikuwa hapa nchini kwa takribani wiki tatu ikishiriki michuano ya Kagame iliyoanza Julai 9, 2024 na kumalizika Julai 21, 2024 ambapo timu hiyo ilikuwa Kundi C ikimaliza kinara mbele ya SC Villa, Singida Black Stars na Al Merriekh Bentiu, huku mechi zake zote hatua ya makundi ikicheza Azam Complex, kabla ya baadaye kuhamia Uwanja wa KMC Complex kucheza nusu fainali na fainali ilipopoteza kwa penalti 10-9 dhidi ya Red Arrows ya Zambia waliokuwa mabingwa.

Katika kipindi chote cha michuano hiyo ya Kagame, Azam ilikuwa katika maandalizi ya msimu mpya ikianzia kambi Zanzibar kabla ya kutimkia Morocco ambapo ikiwa huko ilikuwa ikifahamu inakwenda kukutana na timu gani hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ratiba kuweka hadharani tangu Julai 11, 2024, siku mbili baada ya kuanza kwa Kagame Cup.

APR katika michuano ya Kagame kuanzia hatua ya makundi hadi fainali, ilicheza mechi tano ambazo ilitarajiwa kuwa zinatosha kwa Dabo kuwasoma vizuri wapinzani wake hao bila ya kuona kitu kipya juzi walipokutana.

Mbali na michuano ya Kagame, pia APR ilicheza dhidi ya Simba katika Tamasha la Simba Day, Agosti 3, mwaka huu, jumla zikiwa ni mechi sita timu hiyo imecheza katika ardhi ya Tanzania siku chache kabla ya kukutana na Azam.

Ikumbukwe kwamba, Azam FC imerejea kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, ambapo kurejea kwao ni mara ya pili kufuatia kufanya hivyo mara ya kwanza mwaka 2015.

Mwaka 2015, timu hiyo ilishiriki michuano hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014 bila kupoteza mchezo wowote ambapo katika michezo 26 ya ligi iliyocheza, ilishinda 18 na kutoka sare minane chini ya Kocha Mcameroon, Joseph Omog.

Related Posts