Wataka maboresho miundombinu ya kiuchumi dira ya maendeleo 2050

Musoma. Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuandaa dira ya Taifa ya Maendeleo kwa mwaka 2050, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wameiomba izingatie uboreshaji wa miundombinu ya kiuchumi mkoani humo.

Wametaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na ya ujenzi wa viwanda, uboreshaji wa bandari na mazingira ya uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Wamesema hatua hiyo itaongeza ajira na pia kushusha bei za bidhaa za viwandani zikiwamo za ujenzi, kilimo na biashara.

Wakitoa maoni yao mjini Musoma leo Jumatatu Agosti 19, 2024 kwa ajili ya uandaaji wa dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, wakazi hao wamesema suala la kuimarika kwa uchumi wa mtu mmojammoja na jamii kwa ujumla, lina umuhimu mkubwa katika ustawi wa Taifa.

Chrisant Nyakitita amesema uwepo wa viwanda una faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa na rasilimali zilizopo mkoani humo.

“Mkoa wetu una wakulima, sasa ili mazao yaweze kuwa na tija zaidi ni vema yakaongezwa thamani kwa kuchakatwa hapahapa kwa sasa hilo halifanyiki  kwa sababu hatuna viwanda ndio maana tumeshuhudia mazao kama nyanya, mbogamboga zikiharibika kutokana na kukosekana kwa viwanda,” amesema

Amesema bidhaa ikichakatwa  inakuwa na  faida ikiwamo kupata soko ndani na nje ya nchi, tofauti na ikiuzwa ghafi.

Ernest Ojung’a amesema mbali na kuongeza thamani ya bidhaa na uhakika wa soko lakini viwanda pia ni chanzo kikuu cha ajira, hivyo uwepo wake  ni suluhisho mojawapo la tatizo la ajira mkoani Mara na nchini.

” Serikali imeboresha elimu, wasomi wanaingia mtaani kila kukicha lakini chanzo kikuu cha ajira ni Serikali ambayo pia kwa sasa  nafasi ni kama hakuna, hivyo uwepo wa viwanda utasaidia kupunguza wimbi la wasomi walioko mtaani bila ajira,” amesema Ojung’a

Christina Ndengo amesema ujenzi wa reli ya kisasa unatakiwa kwenda  sambamba na uboreshaji wa bandari ya Musoma ili kurahisisha suala zima la usafirishaji wa bidhaa za viwanda.

Amesema bidhaa nyingi zimekuwa zikiuzwa bei ghali mkoani humo kutokana na gharama kubwa za usafiri wanazotumia wafanyabiashara kuzifikisha kwa mlaji.

 “Kuna vituo vya kutolea huduma za afya takriban kila kata, shule za msingi karibia kila kijiji lakini hakuna watumishi wa kutosha, kata na vijiji vingi havina watendaji hebu hili lifanyiwe kazi kwa sababu tuna wataalamu ambao wanatokana na vyuo vyetu,” amesema Loti Mayamba.

Sagini ajivunia mafanikio

Naibu Waziri wa Sheria na Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini amesema Serikali imejitahidi kufanya mapinduzi chanya katika mambo mengi nchini katika kipindi cha miaka 25 iliyopita ingawa changamoto bado zipo.

Ametolea mfano miundombinu, amesema miaka ya nyuma wakazi wa mkoa huo walikuwa wakilazimika kutumia zaidi ya saa 14 kwenda Mwanza huku kwa safari ya kwenda Dar es Salaam walilazimika kupitia nchini Kenya, mambo ambayo kwa sasa hayapo kwani miundombinu ya barabara imeboreshwa kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema suala la uzalendo ni muhimu ikiwa ni pamoja na kutokomeza rushwa pamoja na kusimamia maadili.

Amesema fursa za utalii zilizopo mkoani Mara zitumike  kuwavutia.

“Kuna haja ya kuwa na uwanja wa ndege wa kisasa, mkoa huu una vivutio vingi hivyo kukiwa na usafiri wa haraka kama huo utachangia kuongeza idadi ya watalii,” amesema Mtambi.

Amesema suala la uboreshaji zaidi wa huduma za kijamii ni jambo la muhimu katika safari ya nchi kuelekea mwaka 2050.

Related Posts