KATIBU Mkuu wa Warriors Queens ya Zanzibar, Neema Othman Machano amesema sababu ya kujiondoa kwenye mashindano ya Cecafa kwa wanawake ngazi ya klabu ni changamoto ya kifedha ikiwemo usafiri.
Michuano hiyo ya kuwania nafasi ya kuuwakilisha Ukanda wa Cecafa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake ilianza juzi ambapo Tanzania ilitarajiwa kuwakilishwa na timu mbili, moja ya Bara Simba Queens ambayo iko tayari nchini humo na Warriors iliyojiondoa ikitokea Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, katibu huyo alisema walishindwa kusafiri kwenda nchini Ethiopia ambako yanafanyika mashindano hayo baada ya kukosa baadhi ya tiketi za ndege.
Neema aliongeza kuwa, kama viongozi walilifahamisha Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) baada ya kukwama, lakini nalo lilikwama jambo lililowafanya wasitishe safari hiyo.
“Kuna baadhi ya tiketi tulipata kama tano hivi na tukajitahidi kupambana, lakini ikashindikina, tukaona tusitishe tu tukarudi kwa viongozi wa ZFF nao wakashindwa,” alisema Neema.
Mwanaspoti lilimtafuta Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Suleiman Mahmoud Jabir juu ya kuzungumzia suala hilo ambapo alisema anaomba aachwe kwa sasa kwani anauguza. “Niwaombe ndugu zangu niko kwenye wakati mgumu wa kumuuguza mzazi wangu sitaweza kuzungumzia hilo,” alisema kiongozi huyo.