Ripoti: Wanaolawitiwa, kubakwa waongezeka nchini

Dar es Salaam. Matukio ya ubakaji na ulawiti yanayoripotiwa kwenye vituo vya polisi nchini Tanzania,   yameongezeka kutoka 23 kwa siku mwaka 2022 hadi 31 mwaka 2023, Takwimu za Msingi Tanzania – 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zimeonyesha.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, ulawiti umeongezeka zaidi ya mara mbili mwaka 2023 hadi kufikia matukio 2,488 ikilinganishwa na kesi 1,205 zilizoripotiwa mwaka 2020. Idadi hii pia ni sawa na ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na 2022.

Kwa uhalisia wa takwimu hizo, matukio sita hadi saba ya ulawiti huripotiwa katika vituo vya polisi nchini kwa siku, ubakaji ukionekana kuwa na matukio 23 hadi 24 kwa wiki.

Wakati hali ikiwa hivyo, upande wa ubakaji matukio yalikuwa 6,827 mwaka 2023 na kuongezeka hadi kufikia 8,691 mwaka jana.

Kifungu cha 136(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kimeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kubaka na kifungu cha 132(2) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa yeyote anayekutwa na hatia ya kujaribu kubaka.

Aidha, kifungu cha 154 kimeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kulawiti.

Kinachopaswa kufanyika kudhibiti

Akizungumzia matukio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesema utamaduni wa ubakaji unalelelewa kwenye familia.

“Linapotokea suala la mtoto kubakwa kama limetokea kwenye familia, familia yenyewe itafanya kila inaloweza kuhakikisha suala hilo linazimwa kwa sababu linaleta aibu,hata binti akilalamika jamii itamtafutia jina baya au anachokizungumza ataonekana yeye ndiye mwenye kosa,”amesema.

Rebecca amesema matukio ya ubakaji yanapotokea jamii huanza kutengeneza mazingira ya mhusika kubebeshwa makosa ya namna alivyovaa, alikuwa wapi wakati tukio linatendeka.

Mawazo ya kumtafutia makosa mwathirika, Gyumi amesema tabia hiyo ndiyo inakoleza matukio ya ubakaji kwenye jamii.

“Kwa sababu tumekuwa tukimaliza mambo nyumbani au yanapofikishwa kwenye vyombo vya mamuzi uwajibikaji tunaotegemea ufanyike vyombo vyetu vinaangalia kwanza aliyetenda kosa ni nani kama ni mlala hoi sheria inafuata mkondo wake kama ni mtu ana madaraka, nguvu ya hela au ushawishi itafanyika namna kesi isifike mwisho,”ameeleza.

Jambo lingine analotaja Rebeca kuongeza matukio hayo ni uwepo wa mfumo unaoamini watu wenye mamlaka na nguvu, wanaweza kuamua kuhusu miili ya wengine jambo ambalo linakoleza matukio hayo.

Mbali na hayo, amesema ipo sheria ya ubakaji na ulawiti kwani licha ya uwepo wa ushahidi na mtu kushitakiwa baada ya muda wahusika au mhusika huonekana akiwa uraiani.

Rebeca amesema ili kudhibiti matukio hayo ni lazima wananchi wajiulize ni aina gani ya jamii wanayoitaka kuijenga.

“Tunajenga jamii ya namna gani kama watoto wetu tangu wakiwa wadogo wanalawitiwa na kubakwa wakiwa wakubwa wataona hayo ndio maisha wanayopaswa kuyaishi na wengine maumivu waliyoyapitia badaye wanakuja kuwa makatili kwenye jamii,”amesema.

Mwanaharakati huyo akitolea mfano binti aliyebakwa na kulawitiwa na watu wanaodai walitumwa na afande, amesema anatafutiwa jina baya ili aonekane yeye ndiyo mkosaji.

Jambo lingine analoshauri ni kuchunguza mifumo ya utoaji wa haki kuhusu uwajibikaji wake kwenye sheria walizokasimishwa kuzisimamia kwani changamoto kubwa iliyopo sasa ni utekelezaji wa sheria.

“Tunatakiwa kuimarisha usimamizi wa sheria, hata mifumo ya dhamana watu wanalalamika kwa sababu imekuwa kichaka cha watu wanaotuhumiwa na makosa ya ulawiti na ubakaji kutumia kurudi kwenye jamii na kesi kuisha, pia sheria za ubakaji na ulawiti zinapaswa kuongezwa ukali kwa sababu haziwatishi watu,”amesema.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema ili kutatua changamoto hiyo ni lazima kufahamu wanaofanyiwa vitendo vya ulawiti na ubakaji wanakuwa kwenye mazingira gani.

Dk Bisimba amesema wakati mwingine unyama huo hufanywa na ndugu wa karibu au jirani hivyo ni muhimu wazazi wakaimarisha ulinzi kwa watoto wao.

 “Tuangalie mazingira waliyopo na kuja na njia ya kutatua changamoto hizi, suala la kusema mtoto ametumwa na jirani je tunamjua huyo jirani binadamu wamebadilika hata hawa ndugu ambao wanakaa nyumbani hawana kazi ni muhimu kuwa nao makini,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben amesema matukio ya ulawiti na ubakaji yanafanyika ndani ya jamii hivyo ni muhimu jamii kuwajibikaji.

“Ni muhimu Watanzania kukumbushwa uwajibikaji, zipo tunu za taifa mojawapo ikiwemo utu kwas ababu kinachofanyika ni kudhalilisha utu wa mtu na Taifa kwa ujumla wake,” amesema.

Katika hoja hiyo, Rose Omuga amesema jamii ina wajibu wa kuyafuatilia matukio ya ubakaji na ulawiti yanapofikishwa katika vyombo vya maamuzi hadi mwisho wake utakapojulikana.

Amesema elimu zaidi inahitajika kwenye jamii na kuimarisha ulinzi wa watoto na wasimamizi wa sheria kusimamia matukio hayo wanaohusika wawajibishwe.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vina nafasi kubwa ya kushughulikia haya, kesi za wabakaji zifike mwisho sababu wapo wanaotuhumiwa na kukamatwa lakini baadaye wanaonekana barabarani,”amesema.

Rose amesema miaka ya nyuma ndani ya jamii kulikuwa na ujamaa kuhusu malezi lakini sasa suala hilo limetoweka lakini wazazi na walimu shuleni wanapaswa kujenga ukaribu na watoto.

Julai 2022 Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya kufungua jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika hospitali ya CCBRT,  alisema tatizo la fistula kwa watoto linasababishwa na vitendo vya ubakaji, huku akitoa rai kwa jamii kuripoti matukio hayo ili kuwaepusha watoto na matatizo hayo

Alisema hospitali ya CCBRT inapokea watoto wenye umri mdogo wakiwa na tatizo la fistula, jambo ambalo linasababisha na vitendo vya ubakaji, ndoa za utotoni na mimba za mapema

”Nilikuwa nanong’ona na Mkurugenzi wa CCBRT Brenda Msangi hapa, akaniambia inasikitisha. Wana cases (matukio) wanazozipokea, mtoto wa miaka 11, 12, analetwa hapa ana tatizo la fistula. Na hii inatokana na watoto kubakwa

“Wale wanaotubakia watoto wanazalisha tatizo hilo. Lakini pia kuna vitoto vidogo kabisa, miaka minne, mitano, sita, wanapokelewa hapa wana tatizo la fistula. Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania, tuone tatizo hili la ubakaji na kulikomesha,” alisema Rais Samia.

Related Posts