Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mpaka sasa wagonjwa 4,232 wenye maambukizi ya homa ya nyani (Monkey pox) wameripotiwa ndani ya Bara la Afrika, sawa na asilimia 4.3 ya wagonjwa wote duniani.
Mpaka sasa watu 99,176 wamethibitika kuwa na ugonjwa huo katika nchi 116 duniani, Bara la Amerika ya Kaskazini na Kusini likiongoza kuwa na wagonjwa 62,904 sawa na asilimia 63.4.
Bara la Ulaya linashika nafasi ya pili likiwa na wagonjwa 27,529 na asilimia 27.8 ya wagonjwa wote duniani. Idadi ya waliopoteza maisha mpaka sasa ni watu 208 pekee, sawa na asilimia 0.2.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu Agosti 19, 2024 na Waziri wa Afya wa Tanzania, Jenista Mhagama akisema bado Tanzania haijapata maambukizi ya ugonjwa huo.
Waziri Jenista kupitia taarifa yake aliyoinukuu kutoka kwa WHO, amesema hadi sasa watu 208 sawa na asilimia 0.2 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
“Hadi sasa hakuna mgonjwa aliyethibitika kuwa na maambukizi ya Mpox nchini. Wizara ya Afya inaendelea kuchukua hatua zifuatazo kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini,” ameeeleza waziri huyo katika taarifa hiyo.
Pamoja na kutoripotiwa kwa ugonjwa huo Tanzania, Waziri Jenista ametaja hatua zinazochukuliwa na wizara kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini, ikiwemo kuimarisha njia za uchunguzi kwa wasafiri kupitia huduma za afya mipakani.
Maeneo yaliyotajwa ni bandari, nchi kavu na viwanja vya ndege lengo ili kubaini wasafiri wenye viashiria na dalili za ugonjwa huo na kuchukua hatua stahiki.
Pia kufuatilia ndani ya jamii mtu yeyote mwenye viashiria au dalili za ugonjwa huo, ili kumhudumia haraka na kupunguza kusambaa kwa maambukizi endapo ugonjwa utaingia nchini.
“Kwa kushirikiana na timu za afya za mikoa, halmashauri, watoa huduma ngazi ya jamii na katika vituo vya kutolea huduma za afya, tumeimarisha utayari katika vituo vya kutolea huduma za afya, maabara za uchunguzi, upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba ili kutoa huduma stahiki endapo ugonjwa utaingia nchini.
“Pia kutoa elimu kwa njia mbalimbali, ikiwemo televisheni, radio na vipeperushi katika mitandao ya kijamii na kuujulisha umma juu ya mwenendo wa ugonjwa huu, ili kuchukua hatua stahiki,” imeandikwa kwenye taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, pale mtu anapoona dalili za homa inayoambatana na vipele kwenye sehemu za mwili, kuchoka na kuvimba mtoki anapaswa kuwahi kwa mtoa huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi.
Jambo lingine la kuzingatia ni utoa taarifa za watu wenye viashiria au dalili za ugonjwa huo kwa kupiga bure namba 199 kwa ajili ya kupata huduma.
“Epuka kugusana kwa njia ya kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana, kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox au kugusa majimaji ya mgonjwa wa Mpox, nawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
“Katika hili nitoe wito kwa maeneo ya umma, kaya na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule, vyuo na vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha kunakuwa na vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni ili kurahisisha unawaji wa mikono,” imesisitiza taarifa hiyo.
Hatua nyingine ni kusafisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mtu mwenye dalili za Mpox pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara kwa kutumia sabuni au klorini (mfano Jiki).
Jambo la kuzingatiwa pia ni kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama ambao wanaweza kuwa na maambukizi, vaa barakoa kwa tahadhari iwapo itabidi kukaa na kuzungumza kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox.