Mabosi wa Fountain Gate, bado wanahaha kunusuru usajili ili kuanza msimu mpya, lakini kama unataka kumjua staa aliyezuia usajili ni Rodrigo Figueiredo Calvalho.
Fountain Gate imeshindwa kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, kutokana na madai ya kusitishiwa mkataba kwa Rodrigo, raia wa Brazil.
Mshambuliaji huyo ambaye aliitumikia timu hiyo kwa kipindi kifupi wakati ikiitwa Singida Fountain Gate kabla ya kusitishiwa mkataba na kwenda kufungua kesi Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).
Timu hiyo ilikuwa na kesi nyingi za madai Fifa, lakini zimemalizwa na kubaki ikipambana na Rodrigo ambaye licha ya Fountain Gate kudai imeshamlipa, kuna hatua moja inatakiwa kukamilika.
Fifa inataka hata kama klabu imemalizana kumlipa mchezaji anayedai ni lazima nyota husika au wakili wake athibitishe kuwa amepokea malipo ndipo kifungo husika kiondolewe.
Rodrigo ameshindwa kuthibitisha kupokea malipo ikielezwa kuwa anailipizia timu yake hiyo ya zamani ambayo wakati inaachana naye mmoja wa viongozi wake walipishana kwa maneno.
Endapo Fountain Gate ingekuwa na mawasiliano mazuri na mchezaji huyo lilikuwa ni suala dogo la kumpa taarifa, kisha angeijulisha Fifa kuwa ameshalipwa stahiki zake na klabu hiyo kuendelea na usajili.
Hata hivyo, kitu pekee kinachoinusuru Fountain Gate ni nyaraka za uthibitisho kuwa ilishamaliza kumlipa Rodrigo, kabla ya dirisha la usajili kufungwa, jambo ambalo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), litaisaidia timu hiyo kwenye mawasiliano na Fifa kuipa nafasi maalumu ya kukamilisha usajili.
Singida imebaki na wachezaji watano pekee kwenye timu iliyokuwa Singida Fountain Gate ambapo licha ya kufanya usajili haitawaingiza kwenye mfumo wachezaji.