Dar es Salaam. Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeshauri umuhimu wa Watanzania kujijengea utaratibu wa kila asubuhi kuanza na kifungua kinywa kabla ya kuwahi kwenye majukumu yao, ili kupata nguvu ya kukabiliana na kazi zilizo mbele yao.
Imesema bila kufanya hivyo hakuna mtu anayeweza kufanya kazi yeyote kwa ufanisi na kupata tija inayotakiwa kama ana lishe duni.
Hayo yamesemwa na Ofisa Lishe Mtafiti Mwanadamizi wa TFNC, Maria Ngilisho leo Jumatatu Agosti 19, 2024 wakati akizungumza kwenye mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) ikiwa na mada: “Kwanini ni muhimu kuanza siku kwa kupata mlo kamili asubuhi?
Katika maelezo yake, Ngilisho amesemas: “Mfano kama unapata lishe pungufu, hasa kwenye vyakula vinavyotupatia nguvu au nishati, ina maana unakuwa na nguvu kidogo ya kufanya kazi na chakula kikiwa duni unaweza kuwa na upungufu wa vitamini na madini.”
Amesema mtu akiwa na upungufu wa madini ya chuma yanayosaidia kutengeneza chembe hai za damu zinazobeba virutubishi na hewa ya oksijeni, akifanya kazi kidogo anaishiwa nguvu.
“Tunafanya kazi bila kuwa na tija kama tunakuwa na lishe duni, mathalani Tanzania tunaamka asubuhi kuwahi kwenye majukumu yetu, ni vizuri kuanza siku yako kwa kupata kifungua kinywa au mlo wa asubuhi,” amesema Ngilisho.
Amesema mlo wa asubuhi unampunguzia mtu uwezekano wa kupata uzito unaozidi, kwani hatokula vyakula bila kuzingatia mpangilio unaotakiwa.
“Mtu akiwa na njaa anashawishika zaidi kula vyakula bila kuzingatia mpangilio, kwa kula kwa kudonoadonoa mara mafuta ili kutuliza njaa inayojitokeza,” amesema.
Amesema mtu akiwa na njaa anakosa utulivu na kuna baadhi wanajikuta wakiingia kwenye tabia hatarishi iwe kwa mtu mzima au mtoto.
“Mtu mzima anaweza kujikuta anafanya kazi ambazo hakustahili kuzifanya na zinaweza zikawa za kumdhalilisha au kumshusha hadhi yake na utu. Kwa watoto wadogo wanaishiwa kurubuniwa na kuishia kwenye hali ambayo si ya kiusalama,” amesema.
Awali, Mwandishi wa habari za afya, Gazeti la Mwananchi, Baraka Loshilaa akichokoza mada hiyo amesema watu kula kwa kuzingatia mlo kamili ni njia sahihi ya kuimarisha kinga ya mwili, itakayosaidia kukabiliana na magonjwa nyemelezi.
Amesema mlo kamili ni mchanganyiko wa makundi yote ya chakula katika kiwango sahihi kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu na kurutubisha kwa ajili ya ukuaji.
Katika maelezo yake, Loshilaa amesema:“Wataalamu wanashauri katika sahani yako ya kila siku, nusu yake lazima iwe mbogamboga, lakini waliowengi unakuta kiwango cha mboga ni kidogo na kutokuheshimu utaratibu wa mlo.
“Nafaka ambayo haijakobolewa kama ulezi, mtama na mchele wa kahawia, inashauriwa katika sahani uwepo kiwango cha robo, lakini watu hawazingatii,” amesema.
Amesema kundi la protini linapaswa kuwa robo kama samaki, nyama ya kuku, maharage na njugu na mafuta yatokanayo na mimea kama mizeituni, soya kwa sababu ni salama kwa afya.
Baraka amesema kutumia mlo kamili kama inavyoshauriwa na wataalamu, unajiweka njia salama ya kuepukana na magonjwa kama kisukari yanayowakabili zaidi wazee na watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Malembo Farm, Lucas Malembo amesema kula mlo kamili si kwa watu wenye vipato vikubwa pekee.
“Watu wanadhani kula mlo kamili ni mpaka wawe na vipato vikubwa, hapana. Kila mtu katika eneo lake anaweza kula makundi mbalimbali ya chakula,” amesema.
“Kweli tunahitaji hizo protini, lakini ziwe bora. Tuna shida nyama namna inavyoandaliwa kuanzia machinjioni inaakisi ubora? Mbogamboga namna zinavyosafirishwa, kuhifadhiwa hata ukivitumia kama mlo kamili je ni salama?” amehoji.
Malembo amehoji tatizo la lishe Tanzania linachangiwa na mambo yapi, hususan kwenye uzalishaji wa chakula, kipato au uelewa.
Amesema takwimu za Serikali zinaonyesha Tanzania inajitosheleza kwa chakula, lakini kuna idadi kubwa ya watu wenye udumavu ikiwa ni matokeo ya kukosa lishe bora, hivyo ameomba mjadala juu ya sababu ya changamoto hiyo na suluhisho.