Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), limesema watoto wengi nchini Tanzania wanakwenda shuleni wakiwa na njaa.
Mbali na hilo, Daktari wa binadamu, Edger Rutaigwa amesema lishe bora ni sehemu ya kinga ya magonjwa mbalimbali ya binadamu, akisisitiza lishe mbaya ndio chanzo cha maradhi mengi.
Wamesema hayo leo Jumatatu Agosti 19, 2024 wakati wakizungumza kwenye mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), ikiwa na mada: “Kwanini ni muhimu kuanza siku kwa kupata mlo kamili asubuhi?
Mtaalamu wa Lishe wa FAO, Stella Kimambo amesema hali hiyo inasababisha watoto wakifika shuleni kuanza kununua biskuti, ubuyu, mihogo na vinginevyo, hivyo hukosa mlo kamili.
“Aina hiyo ya ulaji huwafanya kukosa uelewa wa kutosha, kwani nyakati za asubuhi ubongo huhitaji sukari ya kutosha kwenye damu na kumuwezesha mtu kufikiria, kwa hiyo tunapaswa kuangalia huu mlo wa asubuhi,” amesema.
Stella amesema mlo wa asubuhi huhusishwa na magonjwa sugu kwa sababu mtu anapoacha kula asubuhi, mchana hula kila anachokutana nacho.
Amesema watu wengi kwa mujibu wa tafiti wanaruka mlo kamili wa asubuhi, huku kundi la vijana likiongoza kwa kutopenda kula kutokana na kipato kuwa kidogo, hivyo kupanga muda wa kula.
“Sababu ya kuruka huu mlo wa asubuhi upo kwa vijana wa chuo kikuu au wanaosoma shule za sekondari za kutwa kutokana na mawazo ya kuwahi darasani,” amesema.
Jambo lingine linalochangia vijana kuruka mlo wa asubuhi ni kutopenda kupika, hivyo kukimbilia vyakula vilivyoandaliwa, jambo ambalo huwaingiza kwenye majaribu.
Alichokisema Dk Dk Rutaigwa
Daktari wa binadamu, Edger Rutaigwa amesema lishe bora ni sehemu ya kinga ya magonjwa mbalimbali ya binadamu, akisisitiza lishe mbaya ndio chanzo cha maradhi mengi.
“Lishe bora ni sehemu ya kinga, kutokana na lishe tunaepukana na magonjwa mengi na tunahimizwa kinga ni bora kuliko tiba,” amesema Dk Rutaigwa.
Amesema mtu anapopata mlo bora asubuhi, hupata nguvu ya kufanya shughuli za siku nzima na kuwa na fikra bora.
Mtaalamu huyo wa afya amesisitiza mlo kamili hupunguza ulaji usiozingatia utaratibu, hususan ulaji wa vyakula vya viwandani au vyenye mafuta mengi.
“Pia kwa watu wa mazoezi mlo wa asubuhi unawasaidia kufidia nguvu aliyoitumia kwenye mazoezi ya kujenga mwili,” amesema.
Amesema mtu akikosa mlo wa asubuhi hubadilika kuwa na hasira za haraka kutokana na njaa.
“Mtu anaweza kukukanyaga kidogo tu kwenye daladala unaonyesha utofauti ambao hautarajiwi, ofisini umeombwa kitu unatoa jibu ambalo haliendani kwasabaabu hujapata mko bora,” amesema.
Dk Rutaigwa amesema katika hali hiyo mtu akifanikiwa kudhibiti hasira zake, basi ataonekana asiye mchangamfu, hata akitumwa huaenda kwa kujivutavuta kwa sababu umekosa mlo wa asubuhi.
Kuhusu muonekano wa mtu, Dk Rutaigwa amesema mtu anapopata mlo bora asubuhi uso wake hung’aa.
“Kwa mlo mbaya unaonekana umekosa nuru, lakini kwa mlo bora asubuhi kisayansi ngozi inangaa, hivyo ukikosa mlo wa asubuhi unashindwa kungaa,” amesema.
Jambo lingine aliloshauri mtaalamu huyo ni unywaji wa maji ya kutosha, kwani watu wengi anaokutana nao hutumia maji kidogo.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Maria Samlongo amesema kukosa elimu ya uandaaji wa mlo kamili ni sababu ya maeneo mengi yenye uzalishaji wa vyakula vingi nchini kukumbwa na janga la udumavu.
“Tunashida kubwa kwenye uandaaji, tumekariri familia inachakula cha kutosha ikiwa na mahindi na maharage basi, lakini tunasahau makundi mengine muhimu ambayo tunaweza kuyapata hata kwenye mlo wa asubuhi,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kifungua kinywa cha asubuhi kinachozingatia makundi yote matano ya vyakula, ili kumfanya mtu awe na nguvu ya kumuwezesha kufanya kazi kwa kufikiri sahihi na kulijenga Taifa.
“Hata watoto wadogo kama hawajapata mlo wa asubuhi ataingia kwenye muhangaiko ambao utamfanya asitulie na kuzingatia masomo kikamilifu na kubaki akiwaza chakula alichokiacha nyumbani,” amesema.
Katika maelezo yake amesema katika mwili wa binadamu kiungo kinachotegemea nguvu ni ubongo ambao ni karibu asimilia 20 nishati yote inayoingia mwilini.
Kwa upande wake, Ofisa Lishe Mtafiti Mwanadamizi wa TFNC, Maria Ngilisho amesema Tanzania bado haina takwimu zinazoonyesha mwenendo wa kupata mlo wa asubuhi na kushauri umuhimu wa watafiti kufanyia kazi.
“Watafiti tunapaswa kufanya kazi ili kuona taarifa mbalimbali na kutoa ushauri na kufanya afua zinazoweza kufanya hali ikaboreka, takwimu zilizopo ni chache na ni tafiti ndogondogo zilizofanywa,” amesema Ngilisho.
Amesema tafiti hizo zilizofanywa kwa silimia kubwa zinaonyesha watoto wengi wanaenda shuleni wakiwa hawajapata mlo wa asubuhi kutokana na sababu mbalimbali.
“Utafiti huo ni wazi unaonyesha hata wazazi wanatoka nyumbani kwenda katika shughuli za kila siku bila kupata kifungua kinywa na tukifika kule tumezoea kunywa supu, maharage na chapati ambavyo si vyakula bora,” amesema Maria.
Amesema kitamaduni Tanzania inaundwa na jamii mbalimbali na kila moja ina mlo wa kifungua kinywa cha asubuhi ya asili, lakini imekuwa ikipotea kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na maeneo ya kuishi.
“Mathalani jamii ya kifugaji wengi wanapata mlo wa asubuhi ambao ni mzito na kunywa maziwa mengi kama wakiona watatumia siku zima kuchunga mifugo, ili uwapeleke hadi jioni,” amesema Ngilisho.
Naye Mtaalamu wa Lishe, Janeth Mnzava amesema muda sahihi wa kupata kifungua kinywa kamili unaanzia tangu unapoamka kwa kuzingatia ubora wa chakula kinachotakiwa kuliwa.
“Tafiti mbalimbali zinaonyesha hivyo kuanzia pale mtu anapoamka na nchi mbalimbali zina muda wao, lakini kwa hapa Tanzania ni kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa 4 asubuhi, ni muda unaruhusu kutumia kwa kifungua kinywa,” amesema.