Kibaha. Mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Waliul Asr Education Center wilayani Kibaha, mkoani Pwani, aliyesombwa na maji kwenye mto unaokatiza shuleni hapo umepatikana.
Mwanafunzi huyo, Amar Mwazoa alisombwa na maji Aprili 22, 2024 ikidaiwa chanzo ni tatizo la msuli wakati akiogelea.
mwenzake, Ally Mwinyi, akizungumzia tukio hilo amesema walikuwa wameenda kufanya usafi kwenye uwanja wa michezo, walipofika kwenye daraja Mwazoa alimwambia waogelee.
“Aliniambia twende tuoge kwanza, akasema ana ujuzi wa kuogelea hivyo tuingie kama nitashindwa atanisaidia,” amesema Mwinyi.
Amesema waliingia kwenye maji kwa kujitupa na kuanza kuogelea, Mwazoa akiwa nyuma yake lakini baada ya muda alimwambia msuli wa mguu umekaza.
Mwinyi amesema maji yalimzidi hivyo aliamua kutoka, huku mwenzake akiendelea kuogelea.
“Nilipokuwa nje nilimsikia tena akisema msuli wa mguu unakaza, hivyo anahitaji kusaidiwa. Nilijaribu kufanya hivyo lakini nilishindwa ndipo nilipowakimbilia wanafunzi wenzangu nikawapa taarifa, baadaye kufikisha taarifa kwa uongozi wa shule,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 28, 2024 akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), baba mdogo wa mwanafunzi huyo, Jumaa Mwazoa amesema mwili wa kijana wao umekutwa ukiwa umenasa kwenye shina la mti ndani ya mto na kwamba, taratibu za mazishi zinaendelea.
“Tumeshauleta mwili hapa Tumbi tunaendelea na taratibu ili twende Tanga kwa maziko,” amesema.
Jumaa amesema amepewa jukumu la kusimamia mambo yote na kupeleka mwili wa marehemu Tanga.
“Kaka hatakuja huku, nilimficha kifo cha mwanaye kutokana na mazingira ya kazi yake. Nilisubiri kumjulisha baadaye lakini kuna mtu alimweleza na kusababisha gari alililokuwa akiendesha kugongwa na lingine,” amesema
Amesema mwili umepatikana baada ya watu waliouona kupiga simu kwa uongozi wa shule.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkoani, Shaban Rashid, amesema alipata taarifa kuhusu kusombwa na maji mwanafunzi huyo kutoka kwa uongozi wa shule.
“Leo nimepigiwa simu kujulishwa kuwa mwanafunzi aliyesombwa na maji amepatikana akiwa amekufa, nimefika kushuhudia nimewakuta ndugu na uongozi wa shule,” amesema.
Amesema juhudi zinapaswa kuchukuliwa na shule kuweka tahadhari juu ya mazingira yanayoizunguka ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi na wananchi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya Waliul Asr Education Center, Aaliya Rajani, amesema baada ya tukio hilo walifanya jitihada za kumtafuta mwanafunzi huyo wakishirikiana na mamlaka mbalimbali bila mafanikio.
Amesema hatua wanazochukua ni kugharimia masuala mbalimbali ikiwemo kusafirisha mwili wa marehemu na ndugu wachache.
Katika eneo la mto huo kuna daraja linalokadiriwa kuwa na urefu wa mita tatu na wakati wa mvua husafirisha maji mengi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amekiri kupokea taarifa kuhusu mwanafunzi kusombwa na maji.