Michezo ya majeshi kuanza kutimua vumbi Septemba 6 Morogoro

Mkoa wa Morogoro unategemea kuwa mwenyeji wa mashindano ya michezo ya majeshi itakayoaanza Septemba 6 na kumalizika Septemba 15 ambapo zaidi ya wanamichezo 1300 watashiriki katika michezo hiyo ya aina saba itakayoratibiwa na Baraza la michezo ya majeshi BAMATA.

Akizungumzia maandalizi ya michezo hiyo mwenye wa Baraza la michezo ya majeshi BAMATA Brigedia Jenerali Saidi Hamisi Saidi amesema baraza hilo limefikia uamuzi wa kuleta mashindano hayo mkoani Morogoro kwa kutambua kuwa mkoa huo umekuwa ukitoa vipani vingi katika michezo mbalimbali hivyo itakuwa fursa kwa wananchi kuona vipaji hivyo kutoka kwenye majeshi.

Brigedia Jenerali Said amesema michezo hiyo pia itasaidia kuyaweka majeshi hayo pamoja sio tu katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi lakini pia katika ustawi wa nchi.

“Kupitia michezo hii ambayo itafanyika katika viwanja vya wazi wananchi wataweza kuyaona majeshi yao yakionesha vipaji na kwa kuwa michezo ni furaha, afya na ajira basi wananchi wanaruhusiwa kufika kwenye maeneo yatakayofanyika michezo hii Ili waje wapate burudani ya bure kabisa,” amesema Brigedia Said.

Naye katibu wa Baraza la michezo ya majeshi Tanzania BAMATA Kanali Martin Msumari ameitaja michezo itakayochezwa katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira ya kikapu, mpira wa pete, mpira wa wavu, handball, riadha na Shabaha.

Kanali Msumari amesema michezo hiyo itapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa bongo hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo hiyo.

“Michezo yote itafanyika kwenye viwanja vya wazi lakini mchezo mmoja wa kulenga shabaha ndio utafanyika kwenye viwanja maalumu kwa kuwa wanamichezo watatumia silaha za moto,” amesema Msumari.

Naye mwenyekiti wa kanda ya zimamoto na uokoaji Naibu Kamishna Puyo Nzalanyamisi amewataka waandishi wa mkoa wa Morogoro kuyageuza michezo hiyo kama fursa ya kiuchumi kwa kuuza bidhaa mbalimbalimbali kwenye maeneo yatakayofanyika kwenye michezo hiyo.

“Michezo hiyo itakusanya wanamichezo wengi hivyo wananchi wanaweza kuuza maji, vyakula na hata wenye nyumba za kulala wageni wao ni fursa kwao ya kibiashara.

Akizungumza na Baraza hilo la michezo ya majeshi BAMATA mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema michezo hiyo ina malengo mapana ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa lakini pia itakuwa ni jukwaa la kubaini vipaji vilivyopo kwenye majeshi.

Malima amesema kuwa Serikali ya mkoa iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha michezo hiyo kwa kutambua kuwa michezo ndio kitu pekee kinachowaunganisha watu bila kuangalia tofauti.

Related Posts