Shinyanga. Watu wawili wamefariki dunia na wengine 46 kujeruhiwa baada ya basi la Happy Nation na daladala ya Kampuni ya LBS kugongana eneo la Savannah Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa ya vifo hivyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mkoani humo, Julius Mtatiro, akisema ajali hiyo ilihusisha magari yote yaliyokuwa yakitokea Mkoa wa Mwanza.
Amesema ajali hiyo imetokea jana Jumatatu saa 12:30 jioni huku jitihada za kunusuru maisha ya majeruhi hao wakiwamo watoto wanne zikiendelea.
Mtatiro amesema majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwawaza na Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga.
“Ni kweli Agosti 19, 2024 ajali hiyo imetokea hapa Shinyanga Mjini eneo maarufu kama ‘Savannah’ karibu na Kiwanda cha Jambo mkoani Shinyanga.
“Magari hayo yamepata ajali eneo ambalo kuna vibao vya kuendesha garı kwa spidi 50 lakini inaonekana wao walikuwa mbio zaidi,” amesema Mtatiro.
Amesema abiria wengine 46 wanaendelea na matibabu na miongoni mwao majeruhi watano hali zao siyo nzuri huku wakiwa chini ya uangalizi wa wahudumu wa afya.
“Tunapambana kuwatibu hao ambao wamepata majeraha wakiwamo watoto wanne. Wito wangu kwa watu wanaotumia vyombo vya moto barabarani wawe makini na wazingatie sheria za barabarani,” amesema
Abiria wa daladala, Godfrey Mfungo amesema ajali hiyo imetokea muda mfupi baada ya gari waliyokuwamo kusimama eneo hilo kubeba abiria ndipo basi lilipofika na kuligonga.
Ajali hiyo imetokea zikiwa zimepita siku nne tangu ajali nyingine iliyohusisha malori mawili itokee Agosti 15, 2024, eneo la Manzese mjini Kahama mkoani humo na kusababisha vifo vitatu huku wengine watatu wakirejuhiwa.