Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha adhabu ya kifo aliyohukumiwa Kalisto Mpangwe baada ya kukutwa na hatia ya kumuua baba yake mzazi.
Sasa anatakiwa kupelekwe hospitali ya wagonjwa wa akili akafanyiwe uchunguzi wa kiafya kujua kama ana matatizo ya akili.
Mahakama hiyo imesema baada ya uchunguzi huo, ripoti ya mganga mkuu iwasilishwe kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kesi hiyo ianze upya kusikilizwa mbele ya Jaji mwingine na wakati huo huo, Kalisto atabaki rumande.
Kalisto anadaiwa kumuua baba yake mzazi Mpangwe Sakali, Julai 4, 2019 katika Kijiji cha Imalampaka Wilaya ya Urambo Mkoa wa Tabora, baada ya kuzuka mzozo baina yao.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, baba yake alikuwa akichukizwa na tabia ya Kalisto kuvuta bangi.
Mahakama ya Rufani imefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali, Alice Thomas, aliyedai huenda Kalisto ana ugonjwa wa akili kwa sababu awali kabla ya kumuua baba yake, aliwahi kutishia kutaka kukata tumbo la dada yake aliyekuwa mjamzito.
Wakili huyo pia ameiambua Mahakama kuwa, sababu nyingine ni Kalisto hakuomba toba na alijionyesha hajutii hata kidogo kosa la kumuua baba yake na aliona ni kitu cha kawaida.
Uamuzi huo ulitolewa Agosti 16, 2024 na jopo la majaji watatu ambao ni Shaban Lila, Patricia Fikirini na Panterine Kente.
Jaji Kente akitoa ufafanuzi huo, alisema wameingia kwenye viatu vya Mahakama Kuu ili kufanya kile kilichopaswa kufanywa na Mahakama hiyo kwa kuamuru Kalisto apelekwe hospitali ili kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kwa mujibu wa kifungu cha 220 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na taarifa yake kuwasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tabora.
Kalisto alifikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na alisomewa shtaka na kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Ilidaiwa siku ya tukio kabla ya kuua, Kalisto alikuwa na mzozo wa muda mrefu na baba yake juu ya tabia yake (Kalisto) ya kuvuta bangi.
Siku ya tukio saa moja asubuhi, Kalisto alikwenda nyumbani kwa baba yake na kumuuliza kwa nini alitaka kumuua siku za nyuma.
Ilielezwa kuwa mahakamani hapo kuwa, hali hiyo ilizua mzozo baina yao na Kalisto akafikia hatua ya kumuua baba yake, kisha kukimbia kabla ya kukamatwa siku iliyofuata.
Baada ya kukamatwa alikiri kutenda kosa hilo na kufunguliwa mashtaka na hatimaye kutiwa hatiani kwa mauaji.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Kalisto aliwakilishwa na Wakili Saikon Nokoren huku Jamhuri ambayo ni mjibu rufaa ikiwakilishwa na Wakili Alice Thomas.
Katika sababu zake za rufaa, Kalisto amedai upande wa mashtaka haukuthibitisha bila shaka na Jaji kushindwa kuzingatia ushahidi kwenye rekodi, upande wa mashtaka haukuthibitisha ubaya uliofikiriwa hapo awali kwa upande wake.
Wakili Nokoren aliunganisha sababu hizo za rufaa kwa pamoja ili kufikia matokeo kwamba kosa la mauaji halikuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Akirejelea utetezi wa Kalisto wakili alidai kuwa marehemu alitaka kumshambulia, hivyo mtoto wake alilipiza kisasi kwa kujihami kwa kuwa alikerwa na maneno ya baba yake kuwa alistahili kuuawa kwa sababu alikuwa kijana asiyefaa kwa sababu anavuta bangi.
Wakili huyo aliielekeza Mahakama kwenye uamuzi wake mbalimbali kuhusu maana au kukataa uovu uliofikiriwa katika kesi za mauaji.
Majaji hao walieleza kuwa, jambo linaloonekana kuhitaji kuzingatiwa ni uwezo wa kiakili wa Kalisto wakati wa kutekelezwa kwa kosa aliloshtakiwa nalo la mauaji.
Kuhusu hoja hiyo, Wakili Alice alisema hakubaliani na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya awali, kwa kuwa mienendo ya mrufani kabla na baada ya tukio la mauaji, Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alipaswa kuizingatia.
Wakili Alice alidai uwezekano wa Kalisto kupata ugonjwa wa akili linaweza kuwepo kutokana na ukweli kwamba kabla ya tukio hilo aliwahi kutishia kukata tumbo la dada yake ambaye alikuwa mjamzito.
Wakili alieleza ushahidi mwingine unaoelekea kuashiria kuwa Kalisto alikuwa na matatizo ya akili ni ukosefu wa toba na kujionyesha hadharani kutokuwa na majuto hata kidogo baada ya kumuua baba yake.
Wakili huyo aliwasihi majaji hao waruhusu rufaa kufuta hukumu ya mauaji na badala yake wamhukumu kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Kwa upande wake, Wakili Nokoren hakuwa na la kuongeza katika mawasilisho na maombi ya Wakili Alice na badala yake aliwasihi majaji kuzingatia msimamo wa pande zote juu ya rufaa hiyo na kumhukumu kwa kuua bila kukusudia na adhabu isizidi kifungo cha miaka 30 jela.
Jaji Kente bila alisema kama Kalisto alikuwa akiugua aina fulani ya ugonjwa fulani wa akili ni jambo la kufikiria, chini ya uchunguzi wa Mahakama.
“Kuhusiana na hili, tumejiuliza iwapo Jaji alitekeleza kikamilifu wajibu wake wa kuendesha kesi ya mrufani bila kujiridhisha na hali yake ya akili wakati wa kutenda kosa aliloshtakiwa,” alisema Jaji Kente.
“Ni lazima tuseme kwamba, tunakubaliana na Wakili Nokoren na Alice kwamba yamkini, huenda kukawa na baadhi ya vipengele vya uthibitisho ambavyo vingeweza kudokeza kwamba huenda mrufani alimuua marehemu kwa sababu ya kukosa akili timamu au sivyo kwa sababu ya utetezi.”
Jaji Kente alisema ingawa wanakumbuka mara kadhaa mawazo yakitegemea ushahidi wa kimazingira yanaweza kusaidia katika kufanya uamuzi, katika hali ya kesi hiyo, wanapitia kanuni ya jumla kwamba wanatakiwa kufanya uamuzi kwa kuzingatia ukweli na ushahidi na si mawazo.
“Kwa maana tunafikiri ni akili ya kawaida, kile ofisa wa Mahakama anachoamini, huenda si lazima kiwe kweli, kwa kuangalia suala hili kwa mtazamo wa sheria zetu, juhudi zilipaswa kufanywa na utaratibu unaohitajika kufuatwa kupata maoni ya mtaalamu ili kubaini kama mrufani alikuwa na tatizo la akili,” alisema.
Pia, alisema suala kubwa litakaloamuliwa katika hatua hii ni kwa kuzingatia mawasilisho ya wakili Alice.
“Tunapenda kuanza kwa kuzingatia kwamba,Mahakama Kuu ambapo mrufani aliwakilishwa na wakili ambaye hata hivyo hatukuweza kubainisha jina lake mara moja kwa sababu, katika kipindi chote cha shauri la mahakama hiyo, alikuwa akitajwa tu kama wakili wa utetezi,” amesema.
Jaji Kente amesema kifungu cha 219 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambacho kinazungumzia kinga ya ulemavu wa akili chini ya sheria na kuwa inashangaza katika kesi hiyo licha ya tabia ya Kalisto kuwa ya ajabu na kupitia maelezo yake ya onyo, wakili wa utetezi hakuonyesha mrufani angetoa utetezi wa tatizo la akili.
“Vile vile ni bahati mbaya sana kwamba hata Jaji wa kesi hiyo hakuona haja ya kuitisha ushahidi wa kimatibabu juu ya akili timamu ya mrufani,” amesema.
Huku akinukuu rufaa ya jinai namba 203/2014 ya Mathias Tangawizi dhidi ya Jamhuri ambayo iliamriwa kutokana na tabia ya mrufani inayotia shaka kama inavyoonyeshwa na ushahidi wa shahidi wa kwanza.
Ilikuwa ni wajibu wa Jaji wa mahakama hiyo kuahirisha shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 220 (1) na kuamuru mshtakiwa awekwe mahabusu katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa uchunguzi wa kiafya,” amesema.
Jaji Kente alisema kwa mujibu wa mamlaka yao ya marekebisho waliyokabidhiwa Mahakama hiyo na kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, wanabatilisha shauri, kufuta hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya Kalisto.
“Tukiingia kwenye viatu vya Mahakama Kuu ili kufanya kile kilichopaswa kufanya, tunaamuru mrufani apelekwe katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili ili kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na baada ya kupokea ripoti ya Mganga Mkuu kuhusu afya ya akili ya mrufani, kesi yake itaanza upya mbele ya Jaji mwingine,” amesema.