Dar es Salaam. Kutokana na mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea katika sekta mbalimbali, Benki ya NCBA Tanzania imezindua programu mpya ya kibenki iitwayo ‘NCBA Now’ kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya kibiashara ya benki kwa mwaka wa fedha uliomalizika Desemba 31, 2023. Katika kipindi hicho NCBA ilipata faida ya Sh20.16 bilioni baada ya kodi.
Uzinduzi wa programu ya NCBA Now unaelezwa unaenda sambamba na matokeo mazuri ya kifedha, ukidhihirisha dhamira ya benki kutoa suluhisho za ubunifu kwa wateja.
“Tumekuwa tukisikiliza maoni yenu na sasa tunafurahi kuzindua aplikesheni ya NCBA Now. Wateja wetu sasa watakuwa na uwezo wa kuangalia akaunti zao kwa wakati, kusimamia kadi zao, na kufanya miamala ya hadi Sh5 milioni,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Group, John Gachora wakati wa uzinduzi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Amewashukuru wadau kwa kuwaongoza kupitia mapungufu yaliyokuwapo ambayo yalifanyiwa kazi na kutatuliwa, hivyo sasa wanajivunia matokeo chanya ya mwaka 2023.
Ameongeza kuwa, “Ahadi yetu kwa wateja ni kuendelea kutoa huduma bora, na kuongeza uelewa na ufanisi wa wafanyakazi. Benki inafungua milango katika sekta kuu mbili za ujenzi na utalii,” alisema.
“Zaidi ya hayo, programu hiyo inawezesha uhamisho wa fedha kwenda kwenye akaunti mbalimbali kwa wakati mmoja na malipo ya bili. Mteja atanufaika na huduma hizi na nyingine nyingi, huku mfumo huu ukiwa wenye ulinzi madhubuti,” amesema.
Benki ya NCBA Tanzania inajivunia kuwa ya kwanza kati ya nchi tano inakofanya kazi, hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kutoa suluhisho za kibenki za kibunifu zinazovuka mipaka ya kijiografia, kuwawezesha wateja kote Afrika Mashariki na zaidi kunufaika na huduma za kibenki.
“Leo ni muhimu kusisitiza dhamira yetu kwa kuzingatia mipango ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG). Benki imechukua hatua mbalimbali zinazochangia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti. Zaidi programu ya NCBA Now, itapunguza matumizi ya karatasi,” amesema.
Benki hiyo imekuwa katika mfumo wa kidijitali kwa mikopo mtandaoni.
Imekuwa katika biashara ya kidijitali na bidhaa kama M-Pawa, ambayo kwa sasa iko katika daraja la pili katika huduma za kukopesha zinazopatikana kwenye simu za mkononi nchini Tanzania.
M-Pawa ni miongoni mwa huduma za mwanzo za mikopo ya kidijitali iliyochangia katika ukuaji wa NCBA Tanzania, kwa kusambaza mikopo zaidi ya Sh100 bilioni mwaka jana na kuipatia benki mapato ya takribani Sh25 bilioni.
Mgeni rasmi katika uzinduzi NCBA Now, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliipongeza benki hiyo kwa ubunifu, uwazi, na kwa kuwa na idadi kubwa ya wateja, ambao ni zaidi ya milioni 60 katika nchi zote inakofanya biashara.
Amesema uzinduzi wa programu hiyo utasaidia upatikanaji wa huduma za benki katika kila kona ya Tanzania, mijini na vijijini.