SERIKALI YAUNDA VIKUNDI 3,963 VYA MALEZI CHANYA NCHINI – MWANAHARAKATI MZALENDO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeanzisha vikundi 3,963 vya malezi chanya kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii ili kukabiliana na changamoto za malezi nchini. Hatua hii inakuja wakati changamoto za malezi na makuzi ya watoto zikiwa ni moja ya masuala yanayopewa kipaumbele na serikali na wadau wa maendeleo.

Hayo yalibainishwa tarehe 19 Agosti 2024, mkoani Songwe, na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Asha Shame, wakati akifungua mafunzo kuhusu wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya familia. Mafunzo hayo yamewalenga Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, na Maafisa Elimu kutoka Ofisi ya Mkoa wa Songwe na Halmashauri za Ileje, Mbozi, na Tunduma.

Asha Shame alieleza kuwa serikali inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali, yakiwemo ya viongozi wa dini na waandishi wa habari, kutoa elimu ya wajibu wa wazazi na walezi katika malezi ya watoto. Hadi sasa, viongozi wa dini 109 kutoka madhehebu ya Kikristo na Kiislamu (TEC, CCT, BAKWATA, CPCT, na SDA) wamefikiwa na elimu hii, na jumla ya waumini 35,520 wamepata mafundisho hayo.

Asha Shame aliongeza kuwa, kwa kushirikiana na wadau kama Tanzania Interfaith Partnership (TIP) na UNICEF, serikali imeanzisha vituo vya kulelea watoto mchana vya kijamii, ambapo tayari vituo 255 vimeshaanzishwa nchini. Juhudi hizi zinalenga kuhakikisha kuwa wazazi na walezi wanajua wajibu wao katika malezi bora ya watoto, kuanzia lishe bora, afya, hadi ulinzi na usalama wa mtoto.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Songwe, Menrad Dimoso, alisisitiza kuwa Ofisi ya Mkoa wa Songwe itaendelea kusimamia utekelezaji wa mafunzo haya kwa maafisa wake, ili kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi ya malezi na matunzo ya familia kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Katika salaam zake, Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Interfaith Partnership (TIP), Asina Shenduli, alieleza kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kama UNICEF katika kutoa elimu ya malezi chanya kwa watoto na familia, hususan katika ngazi za chini.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwasaidia washiriki kuandaa mpango kazi wa Mkoa wa Songwe kuhusu utekelezaji wa Mwongozo wa Wajibu wa Wazazi na Walezi katika malezi na matunzo ya familia, na hivyo kuchangia katika kuimarisha malezi na makuzi ya watoto nchini.

 

#KonceptTvUpdates

Related Posts