NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
CHUO Kikuu Cha Dar Es Salaam kimesaini mkataba wa Makubaliano na Kampuni ya Yulho kutoka Korea Kusini kwaajili ya ujenzi wa maabara ya kufanya tafiti aina za Madini.
Mradi huo utagharimu karibu kiasi cha shilingi bilioni 27 za kitanzania hadi kukamilika ikiwemo uwekwaji wa vifaa vya kisasa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 20,2024 wakati wa hafla hiyo Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu was Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema maabara hiyo itakuwa ni kichocheo kwa ufanyaji wa tafiti zaidi kuhusu madini na kuendana na malengo ya taifa letu.
Amesema Chuo kimekuwa kikijitahidi kuhakikisha kinaendelea kufanya vizuri kwenye mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake Kaimu Amidi wa Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dkt. Abubakary Salama amesema maabara hiyo itasaidia kufanya majaribio kwa madini aina zote ambapo kwa mwanzoni wataanza na aina mbili ya madini.
Amesema maabara hiyo itakuwa ni miongoni mwa maabara kubwa nchini ambayo itakuwa inafanya majaribio ya aina zote za madini.