TFF yakubali yaishe, kuilipa mamilioni kampuni ya Romario Sports

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefikia makubaliano nje ya mahakama katika shauri la madai lililokuwa limefunguliwa na kampuni ya Romario Sports 2010 Limited, kwa kuilipa kampuni hiyo deni pamoja na fidia.

Kulingana na hukumu ya makubaliano (consent judgement) iliyotolewa na Jaji Isaya Arufani wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, TFF itailipa kampuni hiyo jumla ya Sh1.69 bilioni kama deni pamoja na fidia mbalimbali.

Kiini cha mgogoro huo ni hatua ya TFF kutolipa deni la Sh843 milioni lililotokana na kampuni ya Romario Sports 2010 Limited, kuiuzia TFF vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya Sh 893 milioni na hivyo kuingia katika mgogoro.

Baada ya TFF kushindwa kulipa deni hilo, kampuni hiyo iliwasiliana na TFF ili kujaribu kumaliza suala hilo kwa njia ya amani na wakakubaliana na TFF kuwa wangelipa fedha hizo kwa awamu 18 kuanzia Januari 31, 2023 hadi Juni 30,2024.

Hata hivyo, makubaliano hayo ya kumaliza deni hilo kwa njia ya amani hayakuzaa matunda na kusababisha kampuni hiyo kuamua kufungua shauri la madai namba 9792 la 2024 katika mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, kampuni hiyo ilikuwa inaiomba mahakama itamke kuwa TFF imevunja makubaliano waliyoingia Februari 2,2023, walipe deni lote wanalodaiwa, kulipa fidia ya jumla ya Sh200 milioni na kulipa fidia ya hasara ya Sh300 milioni.

Pia mahakama iamuru TFF kulipa riba ambayo mahakama itaamuru kama fidia ya uharibifu na fidia ya jumla ambayo jumla yake ni Sh500 milioni na riba hiyo italipwa katika viwango vya kibiashara vinavyotozwa na mabenki.

Halikadhalika waliomba TFF iamriwe kulipa riba ya asilimia 12 ya kiwango ambacho mahakama itaamua kuanzia siku ya hukumu hadi anapokuwa amemaliza kulipa, alipe gharama za kesi na nafuu nyingine ambayo mahakama itaona inafaa.

Hata hivyo, katika kikao cha kwanza cha usikilizwaji (pre-trial conference), suala hilo lilipelekwa kwa msuluhishi ambaye ni Jaji Isaya Arufani ambapo Agosti 6,2024, pande mbili zilikubali kusuluhisha suala hilo na kusaini hati ya makubaliano.

Hati hiyo, ilisajiliwa mahakamani kama ndio hukumu rasmi ya mahakama lakini kwa kuwa kituo cha usuluhishi hakina mamlaka ya kurekodi maafikiano hayo, TFF na kampuni hiyo walilirejesha tena suala hilo Mahakama Kuu ya Tanzania.

Katika hukumu yake aliyoitoa Agosti 19,2024 na kupatikana katika mtandao wa mahakama leo Agosti 20,2024, Jaji Arufani alisema makubaliano hayo yamesajiliwa na kuchukuliwa kuwa ndio tuzo itakayotekelezwa kama hukumu.

Katika makubaliano hayo, TFF ambao walikuwa wadaiwa katika kesi hiyo watailipa kampuni hiyo Sh843 milioni kama kiasi ambacho hakijalipwa na watalipa Sh50 milioni kila mwezi kuanzia mwishoni mwa Septemba, na Oktoba.

Mbali na kulipa Sh150 milioni kwa miezi hiyo mitatu, TFF itailipa kampuni hiyo Sh100 milioni kila mwezi kwa miezi saba kuanzia Novemba 2024 hadi Mei 2025 na pande mbili zinakubaliana kama makubaliano hayo ndio hukumu na tuzo.

Kulingana na makubaliano hayo, kama TFF watashindwa kuilipa kampuni hiyo katika awamu yoyote kama walivyokubaliana, basi kampuni hiyo itaendelea kukazia hukumu ili kulipwa deni lolote ambalo wanadaiwa chini ya makubaliano.

Related Posts