Rais Samia: Kizimkazi imekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tamasha la Kizimkazi limeendelea kujipambanua kuwa la kimaendeleo na chachu ya utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi.

Ametoa kauli hiyo, leo Jumanne Agosti 20, 2024 wakati akizindua Shule ya Maandalizi ya Tasani kwa sasa inaitwa Dk Samia Suluhu Hassan iliyopo Makunduchi mkoani wa Kusini Unguja. Shule hiyo ya kisasa imejengwa kwa ufadhili wa Benki ya NMB.

Kizimkazi ni tamasha lililoanza mwaka 2015 na lilikuwa sherehe ya kumuaga Samia baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa hayati John Magufuli lililojulikana kama Samia Day na ilipofika mwaka 2017 lilibadilishwa jina kuwa Kizimkazi Day.

Tamasha hilo linaloadhimishwa kila mwaka, limekuwa likijihusisha maonyesho ya vyakula vya asili, michezo na ujenzi wa miradi ya maendeleo ya huduma za kijamii zikiwamo shule.

Katika maelezo ya Rais Samia, Tamasha la Kizimkazi litagusa kila eneo ndani ya Wilaya ya Kusini Unguja, akisema taasisi za fedha na mashirika yameonyesha nia ya kuunga mkono jitihada hizo. Amewataka wadau kujitokeza zaidi kushika mkono kufanikisha malengo ya Kizimkazi.

Rais Samia amesema ana matumaini hata la tamasha la mwaka 2024, visiwani Zanzibar limechochea maendeleo kwa sababu kuna miradi mingi imeanza kuzinduliwa huku mingine ikisubiri kuzinduliwa pia.

Kuhusu shule hiyo, Rais Samia amesema sera ya afya na uzazi bora, inaeleza siku 1,000 baada ya mtoto kuzaliwa sawa na miaka mitatu ni muhimu, hivyo shule hiyo itakuwa kituo chao.

“Siku hizi ni muhimu kwanza mtoto apate chakula bora kitakachomjenga na afya, mwili na akili, sasa watoto watakaoletwa hapa wenye umri wa miaka miwili, mitatu na kuendelea watatunzwa na kupata makuzi ya kimwili yatakayowawezesha kuijenga akili yao kwa ajili ya masomo ya baadaye.

Amewataka wazazi kuchangia matunzo ya shule hiyo ili kuendelea kuwa ubora wake akisema shule hiyo itawalea watoto kimaadili ya namna tabia za maisha zinavyotakiwa kuwa ikiwamo kula, kusalimia na kujisaidia.

“Mtoto akitoka hapa kwenda shule ya msingi anajua kila kitu kwa sababu atafunzwa maadili na kujitambua yeye ni nani, anatakiwa kufanya nini. Wosia wangu wazazi leteni watoto hapa, lakini tusaidie michango ili kuitunza shule hii,”amesema Rais Samia.

Mbali na hilo, Rais Samia ameishukuru NMB kwa kufadhili ujenzi wa shule hiyo pamoja na miradi mingine ya maendeleo ikiwamo inayohusisha Tamasha la Kizimkazi. Pia ameipongeza NMB kwa kutambulika duniani kutokana na kujali mazingira, utawala bora na jamii.

“Hili la jamii ndilo hili, wanafanya hivi kwa sababu jamii ndiyo inayowapa uwezo, hivyo lazima warudishe hisani. Nashukuru kwa ubora wa ujenzi wa shule hii, hii ni shule ya mfano jamani katika zile zinazojengwa za maandalizi,”amesema Rais Samia.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna amesema uzinduzi wa shule hiyo unaashiria mwanzo mzuri wa watoto wa Makunduchi kupata elimu yao katika mazingira ya awali na itakuwa msingi mzuri kwa wanafunzi wanoazunguka Kijiji cha Tasani.

“Mwaka 2023 tulikutana hapa wakati unaweka jiwe la msingi na tulikuahidi tutakukabidhi shule hii kabla ya mwaka 2024, ninayo furaha kuwa ndoto imetimia na tunakukabidhi shule hii iliyopewa jina la Dk Samia Suluhu Hassan.

“Shule hii imejengwa na kuwekwa miundombinu ya kisasa ikiwamo maeneo ya kucheza ili kuwapa watoto wetu mazingira mazuri ya kujifunza pamoja na kujenga afya zao. Shule hii ina madarasa matano, kila moja linachukua wanafunzi 40.”

Zaipuna amesema wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, makadirio ya ujenzi wa shule hiyo ilikuwa Sh600 milioni, lakini hadi kukamilika kwake imetumika Sh800milioni ikiwa ni pamoja na eneo bwalo la chakula, samani za walimu na wanafunzi na viyoyozi kwenye ofisi za walimu.

“Hii ni alama ya matumaini na ndoto mpya kwa watoto wetu watakaojengewa msingi imara wa elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye,” amesema Zaipuna.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa amezipongeza Serikali za Tanzania na Zanzibar kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Waziri Lela amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha Tamasha la Kizimkazi lililojikita katika maendeleo yanayogusa maisha ya watu.

“Kisera elimu ya maandalizi Zanzibar ni ya lazima, ndiyo maana kila mwaka Serikali tunaongeza bajeti katika miundombinu ikiwamo shule za msingi ili kutoa elimu bora kwa watoto wetu,” amesema Waziri Lela.

Related Posts