Chadema yadai kushikiliwa viongozi wake, Polisi yakana

Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikidai kukamatwa na Jeshi la Polisi na kuendelea kushikiliwa kusikojulikana watu watatu wakiwamo viongozi wa wawili wa chama hicho wilayani Temeke kinyume cha sheria, Jeshi hilo limesema halina taarifa kuhusu madai hayo.

Kwa mujibu wa Chadema viongozi hao wana siku ya tatu sasa tangu wakamatwe maeneo ya Buza Agosti 18, 2024.

Chama hicho kimewataja watu hao kuwa ni Katibu wa Jimbo la Temeke Jacob Mlay, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke Deusdedith Soka na dereva wa bodaboda, Frank Mbisa.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Foka Dinya amesema jeshi hilo halina taarifa kuhusu madai hayo.

Dinya amesema kama Chadema wanalitaja jeshi hilo, itakuwa wanajua waliko.

“Jeshi la Polisi hatuna taarifa za kupotea kwa watu au kushikiliwa kwa watu hao wa Chadema,” amesema Dinya alipozungumza na Mwananchi leo Agosti 20, 2024.

Taarifa za madai ya kukamatwa viongozi hao zilianza kusambaa jana Agosti 19, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikionyesha picha za viongozi hao zikiambatana na maandishi yaliyoshapishwa kuwa wamekamatwa na polisi na hawajulikani walipo.

Taarifa kwa umma iliyotolewa Agosti 20, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema imelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja bila masharti na kama wametenda kosa lolote wafikishwe mahakamani.

“Tunalaani kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa viongozi wa chama Wilaya ya Temeke kinyume cha sheria, na tunalitaka Jeshi la Polisi liwaachie bila masharti na kama wametenda kosa wafikishwe mahakamani,” amesema.

Taarifa ya Chadema imesema jana Agosti 19, 2024 namba ya simu ya Soka inayodaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Septemba 2023 imetumika kutuma ujumbe kwa mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke wenye maudhui kuwa Soka ameamua kwenda nje ya nchi.

Taarifa hiyo ya Chadema inanukuu ujumbe huo ikisema: “Sababu ndani ya chama kuna migogoro hivyo anaondoka hadi baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakapokamilika na kuwa amesitisha ‘Maandamano’ ya Agosti 26, 2024.”

Kupitia taarifa hiyo Chadema imelitaka Jeshi la Polisi lieleze linakowashikilia viongozi hao ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria na mahitaji muhimu ya kibinadamu.

Related Posts