Wawili kortini wakidaiwa kujifanya mawakili, kuajiri watu bila kibali

Dar es Salaam. Mkazi wa Ukonga, Mohamed Bakari(40) na Rahma Mnyamike (27) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu mashtaka 11 yakiwamo ya kujitambulisha kama mawakili na kufanya biashara za kuajiri watu bila kuwa na kibali kutoka kwa kamishna wa kazi.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Jumanne, Agosti 20, 2024 na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Asiat Mzamiru mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.

Kati ya mashtaka hayo kumi na moja, mashtaka matano ni kufanya biashara za kuajiri watu bila kuwa na kibali au leseni kutoka kwa kamishna wa kazi nchini, mawili ya kughushi, mawili ya kuwasilisha nyaraka za uongo ofisi za Uhamijia, moja kujitambulisha kama wakili na lingine ni kujaribu kutenda kosa la kusafirisha binadamu.

Akiwasoma mashtaka hayo, Wakili Mzamiru amedai shtaka la kwanza ni kujaribu kutenda kosa linalomkabili Bakari pekee yake.

Mzamiru amedai Februari 22, 2024 eneo la Ukonga Banana, mshtakiwa alijaribu kutenda kosa la kusafirisha binadamu wakati akijua ni kosa kisheria.

Shtaka la pili hadi la sita ni kufanya biashara za kuajiri bila kusajiliwa na kuwa na leseni, linalomkabili Bakari pekee yake.

Bakari anadaiwa Februari Mosi, 2022 hadi Februari 22, 2024 katika eneo la Ukonga, mshtakiwa alifanya biashara ya kuajiri Tedy Kimaro, Asia  Shabani Shamte, Fatuma Nyangasa, Mwajuma Said na Anainah Fredrick bila kuwa na leseni.

Shtaka la saba na la nane ni kughushi linalowakabili washtakiwa wote, ambapo Februari 2024 Ukonga Banana, washtakiwa kwa pamoja walighushi cheti cha kuzaliwa cha Fatuma Nyangasa na Ananaih Fredrick kwa kuonyesha kuwa vimetolewa na Rita wakati wakijua kuwa ni uongo.

Shtaka tisa na kumi ni kuwasilisha nyaraka za uongo, ofisi za Uhamiaji linalowakabili washtakiwa wote.

Wakili Mzamiru amedai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Oktoba 23, 2023 katika ofisi za Uhamiaji zilizopo Temeke, waliwasilisha vyeti vya kughushi vya Nyangasa na Fredrick wakionyesha kuwa ni halali na vimetolewa na Rita.

Shtaka la kumi na moja ni kujiwakilisha kama wakili au kujitambulisha kama wakili, linalomkabili Bakari pekee yake.

Katika shtaka hilo, Bakari anadaiwa kati ya Oktoba 2023 na Februari 22, 2024, eneo la Ukonga, kwa makusudi, alitumia mhuri wenye jina la Wakili Peter Msanjila katika uthibitisho wa nyaraka mbalimbali akionyesha kuwa yeye ana sifa za kuwa wakili, wakati akijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, walikana kutenda kosa hilo.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Swallo amesema mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao yanadhaminika na kutoa masharti manne.

Amesema kila mshtakiwa anatakiwa kusaini fungu la dhamana la Sh5 milioni

Pia, kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao saini bondi ya Sh5 milioni.

Masharti mengine, washtakiwa hao wanatakiwa kuwasilisha hati za kusafiria mahakamani hapo.

Vile vile, washtakiwa hao hawaruhusiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama.

Hata hivyo, mshtakiwa Mnyamike alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru kwa dhamana.

Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 2, 2024 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa Bakari amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutumiza masharti ya dhamana.

Related Posts