Kundi la Wahafidhina wa Ulaya na Wanamageuzi, ECR, kambi ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Meloni, lilifanikiwa kupata nafasi 13 katika kamati 20 na kamati ndogo nne za bunge la Umoja wa Ulaya zikiwemo nafasi tatu za wenyeviti na 10 za makamu wenyeviti.
Nafasi saba kati ya hizo, ambazo ni kamati zinazoshughulikia masuala muhimu kama vile masuala ya kigeni, usalama, mazingira na afya ya umma, zimepewa wanachama wa chama cha Meloni cha siasa kali za mrengo wa kulia Brothers of Italy, kutoka nafasi moja kwenye muhula uliopita wa bunge.
Soma zaidi:Von der Leyen asema yuko tayari kupambana na misimamo mikali ya kisiasa
Carlo Fidanza kutoka chama cha Brothers of Italy, ameiambia DW kuwa chama chake kinajivunia ukuaji huo.
Akizungumzia taarifa hizo mnamo Julai 23, Nicola Procaccini, mwenyekiti mwenza wa kundi la ECR na pia mbunge wa chama cha Brothers of Italy, alipongeza kukuwa kwa nafasi ya muungano huo katika masuala ya bunge la Umoja wa Ulaya.
Soma zaidi: Macron ataka wanasiasa kuungana dhidi ya misimamo mikali
Procaccini amesema licha ya jaribio la kundi la siasa za mrengo wa kushoto kususia katika kamati zote, matokeo mazuri ya uchaguzi huo yanaonesha kuwa wengi wamehama na kwamba kundi la Wahafidhina linaweza kufanya maamuzi katika bunge hilo miaka mitano ijayo.
Kuimarika kwa ECR ‘kutatishia maadili ya kidemokrasia
Hata hivyo, baadhi ya waangalizi wana wasiwasi kwamba kuwepo kwa wawakilishi wa ECR katika nafasi hizo za uongozi wa kamati zenye nguvu kama hizo, hakuwezi tu kushawishi ajenda za bunge, lakini pia kusababisha kuhalalisha siasa kali za mrengo wa kulia ndani ya Bunge la Ulaya na kudhoofisha maadili ya kidemokrasia hatua kwa hatua.
Zsuzsanna Vegh, afisa programu katika Wakfu wa Ujerumani wa Marshall, taasisi inayohusika na sera ya umma ya Marekani, anasema kuhalalisha siasa kali za mrengo wa kulia kama inavyoonyeshwa na kundi la ECR, kunatishia maadili ya demokrasia ya kiliberali. Kwa mujibu wa Zsuzsanna, hali hiyo inaweza kuwa changamoto kwa mafanikio ya ushirikiano wa Ulaya.
Sio vyama vyote ndani ya ECR vinachukuliwa kama vya siasa kali za mrengo wa kulia, lakini nguvu na ushawishi wa Brothers of Italy una baadhi ya wabunge na wachambuzi wa kisiasa wanaohusika.
Julien Hoez, mhariri wa jarida la siasa, na mshauri wa masuala ya Umoja wa Ulaya, anasema umaarufu wa ECR unaokuwa ndani ya Umoja wa Ulaya, hasa wanachama wa Brothers of Italy, unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa haki za wanawake, uhuru wa vyombo vya habari na usimamizi mzuri wa masuala ya uhamiaji. Hoez anasema wanaweza kujaribu kushinikiza sera inayowazuia wanaotafuta hifadhi na wafanyakazi wa kigeni kuingia Ulaya.
Zsuzsanna Vegh anasema wenyeviti wa kamati, makamu wenyeviti wana jukumu muhimu katika kupanga na kutekeleza kazi ya kutunga sheria ya Bunge la Ulaya.
Hawahakikishi tu majadiliano kuhusu miswada mbalimbali, lakini wanaandaa ajenda, wanaendesha mikutano na kusimamia nani anayeshughulikia nyaraka muhimu za miswada maalum.
Mchambuzi Hoez anasema wote, Meloni na Marine Le Pen wa chama cha National Rally cha Ufaransa, wamesimamia sera kali za vyama vyao katika miaka ya hivi karibuni, katika jaribio la kuongeza kukubalika kwao miongoni mwa wapiga kura.
Katarina Barley, mwanasiasa mkuu wa chama cha Wanasoshalisti na Wanademokrasia, mapema mwezi Julai, alisema kuwa wazalendo lazima watengwe ndani ya Bunge la Ulaya, na wazuiwe kuhujumu siasa za kujenga, barani Ulaya.
Maoni kama hayo yaliungwa mkono pia na Terry Reintke rais mwenza wa muungano wa vyama vya Kijani ambao ni watetezi wa mazingira, EFA. Reintke aliviambia vyombo vya Habari vya Ujerumani kuwa kundi la mrengo wa kulia linaweza kuharibu na kuvuruga sera za kundi la Kijani.
Ripoti ya hivi karibuni ya Wakfu wa German Marshall, ilieleza kuwa, wakati mielekeo ya kiitikadi ya makundi ya kisiasa yasiyofuata siasa kali za mrengo wa kulia itaendelea katika siasa za Umoja wa Ulaya, mchakato wa kuhalalisha sehemu za mrengo wa kulia unaendelea taratibu.
Sikiliza: