MARA kadhaa Mwanaspoti limekuwa likimtafuta mwigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Irene Uwoya ili afunguke kuhusu maisha yake mapya baada ya kuokoka, aliyopitia na sababu kubwa iliyomfanya amrudie Mungu.
Kama yalivyo maisha mengine ya wanadamu, haikosi misukosuko, hofu, ndoto za kutisha na hatimaye kupata maono na kuamua kuokoka.
Irene anafunguka mengi na aliwahi kusema ipo siku atafunguka yote kwenye Ukurasa wake wa You Tube kutokana na maswali ya mashabiki juu ya maisha yake kubadilika kuwa mengi.
Huyu hapa anasimulia kilichomfanya aamue kuokoka na maisha yake baada ya kuokoka.
MAPITO YAMRUDISHA KWA MUNGU
Anasema alikuwa anasali kwa kipindi kirefu lakini akifanya na mambo mengine kabla ya kuamua kuwa na Mungu moja kwa moja.
““Unajua kuna watu wengi sana wanajiuliza maswali, kuhusu maisha yangu ya sasa hivi, nilikuwa nasali siku nyingi ila sikuwa na sali sana, kwani ilikuwa kuna muda na sali na muda si sali nakuwa kwenye vitu vingine, kwa hiyo sikuwa nimekaa kwa Mungu mia kwa mia. Hadi naamua kubadilika na kuwa kwa Mungu, mtoto wangu na mimi mwenyewe ni kutokana na mapito niliyopitia kwenye maisha yangu.”
Aliwahi kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram picha yenye maneno ‘Friends and God’, na hapa anafunguka maana yake.
‘Friends and God’ ni mapito ya Mungu na ni kitu nilichokianzisha sio kwa kupanga wala kukiandaa, ni kitu ambacho Mungu mwenyewe ametaka nikifanye kwa hiyo, maana yake ni marafiki wa Mungu ambao ni mimi na wewe.”
“Kwa sasa siwezi kuliongelea kwa sababu sina hicho kitu na nasikia watu wanasema nina kanisa. Niwaambie tu bado sina kanisa Mungu hajanionyesha wala kunipa hicho kibali, lakini watu wanaongea wanasema labda inaweza ikawa hivyo kwa sababu Mungu wakati mwingine anaweza kutumia watu, kwa hiyo inawezekana labda ikaja kuwa hivyo.”
“Siku moja wakati nipo nyumbani naomba, nilisikia sauti ndani yangu ikiniambia ‘niende milimani kufunga siku tatu’, kuna kitu Mungu anataka kuongea na mimi, baada ya kupata hayo maono nilitafakari sana hadi nikawa najiuliza, ni kitu nimekisikia au ni mimi tu mwenyewe najiwekea vitu kichwani,” anasimulia Uwoya ambaye baada ya kupata uhakika na maswali hayo kutoka kwa mtumishi wake, alifunga safari hadi arusha akisindikizwa na madairekta wake Majag na John Elisha ‘Boneka’.
Anasema baada ya kufunga siku hizo tatu, Mungu alinimwambia vitu vingi sana, na moja ya vitu hivyo ni amtumikie, ingawa alikaidi licha ya kuambiwa kila mara. “Na nilijaribu kuwaza na kujiuliza nitamtumikia kinamna gani sababu mimi sioni kama nitaweza kuwa mchungaji sababu sio kitu ambacho nilikuwa nakitamani, kwa hiyo nilimwomba Mungu anipe muongozo kitu gani natakiwa kukifanya.” “Nilivyonamaliza niliona natakiwa nianze na mabinti kwa kuwahubiria au niongee nao kuhusu mambo ya Mungu, kuna mabinti wengi sana ambao wamepotea na pengine walikuwa na maisha kama yangu, hivyo natakiwa kuwaongoza wamjue Mungu na warudi kwenye njia sahihi na kuwawezesha kimaisha.”
Anasema alitafakari nini afanye ili kuwasaidia mabinti ndipo likaja wazo la kuanzisha Friends of God kutoka kwa Majag;
“Niliwashirikisha wenzangu na Majag akasema, ni kitu kizuri, sasa tunafanyaje?
“Tukaanza kutafuta mabinti wachache na jinsi ya kuifanya, kama ni kanisa au iitwaje. Ndipo Majag akasema kwa nini isiitwe ‘Friends of God’ maana yake ni ‘Marafiki wa Mungu’, jina likaja ghafla na tukalipeleka kwenye maombi na ndipo jina hilo lilipoanzia.”
“Miaka kama 10 iliyopita niliwahi kupokea simu na mtu akajitambulisha kama mchungaji. Simkumbuki jina ila aliniuliza naongea na Ray? Nikamuuliza Ray yupi? Akajibu Ray Kigosi?
“Nikamjibu hapana mie naitwa Irene, akasema aliota yupo stendi ya basi na Ray akamwambia Mungu anasema anatakiwa amtumikie, kwa hiyo akamuomba Ray namba yake ya simu Ray akampa, alipoamka Mungu akamkumbusha huyu mtu anatakiwa amtumikie hivyo mpigie simu (yaani mimi), anasimulia Uwoya na kuongeza mtu huyo alimpigia simu na kuongea naye;
“Aliniambia Mungu anataka umtumikie na ni vyema ukafanya mapema, kisha akakata simu,” anasema Uwoya ambaye anakumbuka usiku huo alikuwa anatoka Leaders na alirudi nyumbani na kuwasimulia Chopa Mchopanga na Miriam Ismail na walitaka mtu huyo apigiwe simu ila namba ikawa haipatikani na hakumtafuta tena kuendelea na maisha yake.
Anasema baada ya kuachana na mchungaji huyo, kuna siku alienda kanisani na kuambiwa tena yeye ni mchungaji wa Mungu, hayta hivyo aliishia kucheka na maisha yakaendelea kabla ya baadaye kuanza kupata ndoto za mambo hayo hayo.
“Baadae nikawa napata ndoto, naota nipo sehemu nimekaa mtu ananiambia vitu vya Mungu au kuota mtu fulani anaweza kesho akafanya kitu hiki mara nashtuka, nikiamka naona kile kitu kimetokea kweli, lakini nikawa naendelea kupuuza,” anasema alipuuza kwa sababu alikuwa bado mtu wa starehe na pombe na alikuwa anatumia hadi Sh10 milioni kwa siku au wiki na ilikuwa kawaida na mtu akimwambia kuhusu Mungu haelewi ingawa alikuwa akienda kanisani na yeye ni Mkatoliki na kumtumikia Mungu aliona ni ushamba.
AUGUA GHAFLA, SAFARI IKAANZIA HAPO
Anasema maisha yakaendelea na hakuona kama anatakiwa kumtumikia Mungu hadi alipougua na kupelekwa hospitali lakini huko hawakukuta ugonjwa wowote na zaidi alihisi moyo wake akienda mbio.
“Mungu aliamua safari ianzie hapo, maana niliumwa sana na watu wangu wa karibu wanajua hili, nilienda hospitali nikaonekana sina shida yoyote nilipofanya vipimo, ila Moyo wangu ulikuwa unaenda mbio sana nasikia sina amani, situlii na hakuna kitu nakifanya kikaenda yaani siwezi hata kuelezea.”
AITWA NA BIBI, AMTAFUTA MWAKASEGE
Anasema alipata wakati mgumu sana na aliamua kufunga safari hadi kwa bibi yake aliyekuwa anaumwa na aliambiwa alitaka kuongea naye kabla hajafariki dunia.
“Unajua bibi yangu tumezaliwa tarehe na mwezi mmoja (Novemba 18), Nilienda kwake na nilipofika walishangaa kuniona. Alikuwa hawezi hata kuonea nikamnunulia dawa, baada ya hapo niliondoka lakini kesho yake nikapigiwa simu ameshafariki dunia. Niliogopa sana, tukazika msiba ukaisha.”
“Baada ya hapo nililala usiku nikaota niko kanisani, nilikuwa nimekaa mwisho na kuna watu wengi. Mchungaji alikuwa akihubiri na alipomaliza akawa anaondoka, aligeuka na tukakutana macho tunaangaliana. Akanifuata akaniambia, yaani wewe utaumwa utapelekwa hadi India hutapona na utakufa na sina hata miezi sita, nikabaki namwangalia, akaondoka,” anasema Uwoya na kuongeza wakati anaondoka yule mchungaji alisikia watu wanamuita, Mwakasege, Mwakasege, akashtuka na kujiuliza Mwakasege ni nani, akakumbuka hilo jina na kuamua kumtafuta mchungaji (Christopher Mwakasege).
MWAKASEGE YUKO BIZE, AZIDI KUCHANGANYIKIWA
Anasema baada ya hapo hakuwa vizuri na watu wake wa karibu mmoja akamwambia waende kanisani na mwingine kwa mganga.
Hata hivyo, anasema aliamua kumtafuta Mwakasege lakini alipoongea na mtoto wake aliambiwa yuko bize.
“Nikamwambia naomba sana kuongea naye, sababu kuna kitu nahitaji kujua na nikaelezea kitu nilichokiona, akanijibu atafikisha ujumbe, baadae alinipigia simu akasema waniambie nifanye maombi sana sababu nilimuweka Mungu kama zima moto, nilichanganyikiwa sana,” anasema Uwoya na kuongeza alikosa raha na amani na hata watu wake walijua atakufa hadi alipopata msukumo wa kwenda kanisani.
“Rafiki yangu mmoja anaitwa Debora akaniambia twende kanisani, hapo tulikuwa Moshi kwenye msiba, tukaenda Arusha hadi kanisani, akaja mtumishi sikumwambia nilichokiota wala nini, akawa ameniangalia kama dakika 10, hiyo siku nililia sana. Akaniambia nitaumwa sana na wazazi wangu watahangaika na sitapona watanipeleka hadi India, nitakufa.”
“Niliogopa maana sikumuhadithia, akaniuliza nimeemda kanisani pale mwenyewe au nimelazimishwa? Nikamjibu mwenyewe, ndiyo akaniambia natakiwa kumtumikia Mungu,” anasema Uwoya na kuongeza alipomwambia hajawahi kuamini hayo aliambiwa wataongea siku nyingine na kama yuko tayari kumpokea Yesu.
“Nikamwambia niko tayari, akaniambia simama, akanisomea sala ya toba, akaanza kunifanyia maombi na aliniombea kwa saa tano, baada ya hapo nilikuwa mwepesi sana na kwa mara ya kwanza niliweza kula, cha kushangaza kuna baa tulienda kula, wakati tunaenda hawakuniona kabisa wahudumu walikuwa wananipita tu, hadi meneja alinifuata kuniambia asante kwa kuja leo kututembelea baa yetu yaani jana yake nilikuwepo hawakuniona kabisa hadi muhudumu alikataa hakunihudumia jana ndio ameniona ile siku ya pili, yaani ni kitu ambacho nilikishangaa sana na sikuwahi kukuiona maisha yangu.”
Anasema kipindi anapitia misukosuko hiyo alikuwa na pesa nyingi na alikula sana bata lakini hakuwa na amani ya moyo.
“Yaani nilikuwa na hela nyingi kwenye pochi lakini amani hakuna, hadi nilikuwa nawaambia watu natamani niwape hizi pesa ili nipate amani, lakini walikuwa hawanielewi.
“Ndipo nilipogundua pesa siyo kila kitu na kuna muda haifanyi kazi, baada ya hapo nilipata amani na kugundua Mungu yupo kweli na nilifurahi sana na nilirudi kama zamani, japo haikuwa rahisi sababu kuanzia pale vitu vyangu vikawa vinaenda tofauti.”