Arusha. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshtushwa na madai ya madereva wa Serikali kulogana ili wapate magari ya kufanyia kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Juma Mtanda kwenye kongamano la tatu la madereva wa Serikali la mwaka 2024 linaloendelea jijini Arusha kwa siku nne mfululizo.
Mtanda amesema baadhi ya madereva wamekuwa wakilogana ili wapate magari ya kuendesha kutokana na vyombo vyao kuharibika na kuishia kukaa kwenye ajira wakilipwa mishahara bila kupangiwa majukumu, hivyo baadhi hufanya mambo hayo wapangiwe kazi.
Akizungumzia leo Agosti 20, 2024, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakuu wote wa taasisi na waajiri kuhakikisha wanafanya tathimini ya magari yote ya Serikali yaliyoharibika na yatengenezwe, kuhakikisha madereva wote walioajiriwa wanapata vyombo vya kufanyia kazi.
“Mmh! hili la kulogana limenishtua sana, sijawahi kujua kwamba madereva mnafikia hatua ya kulogana ili mpate vyombo vya kufanyia kazi.”
“Hivyo sasa nitumie nafasi hii, kuwaagiza wakuu wote wa taasisi na waajiri waanze kufanya tathimini mapema sana ya kufufua magari ya Serikali yaliyoharibika ili madereva wapangiwe kazi wasilogane kugombea machache yaliyopo,” amesema.
Mbali na hilo, amewataka waajiri kubainisha madereva waliopo kwenye taasisi zao ambao hawana vyombo vya kufanyia kazi au hawajapangiwa majukumu, ili Serikali iwatambue na kuwapangia kazi.
Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini ambazo hazijawasilisha michango ya madereva wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii wafanye hivyo haraka, kuepuka ukiukwaji wa haki za madereva wanapostaafu.
Amewataka wakuu wa taasisi kujali masilahi ya madereva hasa ya kupata mafunzo ya mara kwa mara ya mabadiliko ya teknolojia ya magari ya Serikali yanayoingia, pia kuwalipa posho na kuwapa mapema ratiba za safari kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza dereva asipojipanga vema.
Majaliwa amewataka madereva wanawake kuchangamkia fursa ya nafasi za ajira za kada hiyo zinazotangazwa na Serikali.
“Nimeambiwa hapa wanawake kwenye kada hii ni 50 tu, wakati wanaume ni zaidi ya 7,000, sasa niwaambie, Serikali inatoa upendeleo na kipaumbele kwenu wanawake wenye sifa ya udereva, ombeni haraka mpate ajira hizi,” amesema.
Amesema mwaka huu wa fedha 2024/2025 Serikali inatarajia kutangaza nafasi za ajira 745 za udereva.
Mbali ya hilo, amewaonya madereva wa Serikali ambao wanatumia nafasi zao vibaya ikiwemo kukiuka maadili ya kazi, kulewa kazini, kuvujisha siri za kazi wanazozisikia kutoka kwenye simu wanazozungumza viongozi.
“Maadili ninayozungumza hapa ni marufuku kulewa kazini, kuendesha gari kwa mkono mmoja huku ukiwa na kiongozi, au kusikiliza simu anayozungumza bosi wako unachangia bila kuulizwa na hata baadaye unavujisha siri anazozungumza au nyaraka mnazobeba,” amesema.
Amewataka madereva kuhakikisha wanatunza vyombo vyao vya kazi viwe endelevu na kutimiza malengo yaliyotarajiwa ya usafirishaji, pia kuzingatia sheria za usalama barabarani kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo kusababisha ajali na kugharimu viungo au maisha ya watu.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha masilahi ya kada za madereva wake ikiwemo mifumo ya ajira na upandishwaji wa vyeo.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST), Flora Mnyandavile amesema mkutano huo wa tatu umejumuisha wanachama 1,300 kwa lengo la kuona mambo wanayokumbana nayo kujadili namna ya kuyakabili na kuainisha mengine yatatuliwe na Serikali.
Amesema chama hicho huru, kina wanachama 7,241 kati yao wanawake ni 50 pekee, hivyo kuiomba Serikali kuona namna ya kuwapa kipaumbele wanawake wenye sifa kupata ajira za kada hiyo.
Amefafanua kuwa changamoto kubwa ni kutowasilishwa kwa wakati makato kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kusababisha kucheleweshewa mafao wanapostaafu lakini pia kutotolewa kwa malimbikizo ya mishahara kwa baadhi ya madereva, baada ya kupewa barua za kubadilishiwa muundo.
Mkuu wa Huduma Saidizi kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Josephine Matiro amemuomba waziri mkuu kuwashurutisha wakuu wa taasisi kulipa madeni yao kusaidia ufanisi wa kazi kufanyika.
“Kwa mwaka 2023 pekee tunazidai taasisi zako zaidi ya Sh39 bilioni na mwaka huu zaidi ya Sh14 bilioni kwa kuwatengenezea magari na mitambo, hali ambayo inapunguzia kazi na ufanisi taasisi yetu,” amesema.
Katika hilo, Majaliwa amewataka Temesa kuandika barua ofisini kwake na kuainisha taasisi zote zinazodaiwa ili waandikiwe barua ya amri ya kulipa.
“Kuna wakati tulifikiria kuifuta Temesa kwa kulegalega lakini tukawapa muda, ila kwa sasa mnafanya kazi nzuri, leteni barua haraka tuwatumie taasisi mnazowadai walipe madeni maana hivi sasa hela wanazo kutokana na kuingiziwa katika mwaka huu wa fedha,” amesema.