Mgulani yatishia kushusha timu BDL

BAADA ya Mgulani (JKT) kuifunga Savio kwa pointi 66-62, timu hiyo ina nafasi ya kubwa ya kucheza hatua ya nane bora ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).

Nafasi ya kucheza hatua hiyo itakuja endapo timu hiyo itashinda michezo minne iliyosalia ya mzunguko wa pili wa mashindano hayo.

Kupanda kwa Mgulani kutoka nafasi ya 13 hadi ya 10  kumetokana na ushindi ilioupata dhidi ya Vijana ‘City Bulls’, Crows na Savio.

Mgulani ambayo ni timu ya pili ya JKT katika michezo  iliifunga Vijana kwa pointi 65-54, Crows 65-55 na Savio  66-62.

Timu ya Savio katika mchezo wake dhidi ya Mgulani ilianza vizuri katika robo ya kwanza ikiongoza kwa pointi 28-15  na robo ya pili matokeo yalikuwa 15-15, ilhali ile ya tatu Mgulani ilipata pointi 18-13 na 18-13.

Katika mchezo huo Sixto Ngomeni wa Mgulani aliongoza kwa kufunga pointi 16, akifuatiwa na Clavin Bwabwetega na Adam Lutungo waliofunga pointi 14 na 12 mtawalia.

Kwa upande wa Savio alikuwa Joshua Hamoud aliyefunga pointi 15 akifuatiwa na Godfrey Swai aliyetupia 12.

Wakati mambo yakianza kuwa mazuri kwa upande wa Mgulani huku nane bora ikikaribia, kamishina wa Ufundi na Mashindano wa BDL, Haleluya Kavalambi amesema hatua ya nane bora itakuwa ni ngumu.

Kavalambi ameliambia Mwanaspoti kuwa ugumu wake utatokana na uwezo mkubwa wa timu zitakazoingia kucheza hatua hiyo.

“Kwa mfano hatua ya nane bora unafikiri itakuaje. Unajua hata kupata nafasi ya kucheza hatua ya nane bora timu zinatakiwa zifanye kazi kubwa,” alisema Kavalambi.

Kamishna huyo ambaye pia ni kocha wa timu ya ABC na timu ya wanawake ya Jeshi Stars, alisema anavyoiona ligi hiyo  timu yoyote inaweza kuwa bingwa.

Naye kocha mkuu wa Dar City, Mohamed Mbwana alisema upinzani umeanza kuongezeka tofauti na miaka nyuma, ambapo baadhi ya timu ndizo zilikuwa zikifanya vizuri uwanjani tofauti na sasa kila moja inaonyesha ushindani wa kiwango cha juu.

Related Posts