Mahakama yaipa ushindi Serikali, ikiruhusu Sheria ya Fedha 2023

Nairobi. Mahakama ya Juu nchini Kenya imesitisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa uliobatilisha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023.

Uamuzi huo umetajwa na Mahakama ya Juu kuwa utasaidia ufanisi wa kutimiza bajeti ya nchi hiyo kwa kuzingatia masilahi ya umma.

“Kwa kuzingatia masilahi ya umma katika suala hili, tunaagiza rufaa iliyojumuishwa hapa isikilizwe ndani ya muda mfupi iwezekanavyo baada ya uamuzi huu kutolewa,” umeeleza uamuzi wa majaji Martha Koome, Philomena Mwilu, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u. , Isaac Lenaola, William Ouko na Mohammed Ibrahim.

Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya watu nchini humo huku wengi wakisema ilipitishwa bila ushirikishwaji wa wananchi ipasavyo.

Novemba 2023, Mahakama Kuu ilitangaza baadhi ya vifungu vya sheria hiyo kuwa kinyume na katiba.

Hilo lilisababisha kuwasilishwa kwa rufaa sita katika Mahakama ya Rufaa, na katika hukumu iliyotolewa Julai 31, 2024, Mahakama hiyo ilitangaza sheria hiyo yote kuwa kinyume na katiba.

Serikali ikiongozwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Hazina, Mwanasheria Mkuu, Bunge la Kitaifa na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya- iliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Juu ya Kenya na leo imeshinda kesi hiyo.

Katika notisi ya hoja iliyowasilishwa mbele ya Mahakama Kuu, Serikali iliomba kusitishwa kwa utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama ya Rufani kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa hiyo.

Serikali iliiambia Mahakama ya Juu kuwa uamuzi wa Mahakama ya Rufani unasababisha hali matatizo katika kukusanya mapato ambapo Serikali inategemea Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 kwani Muswada wa Sheria ya Fedha, 2024 uliondolewa.

Pia, Serikali ilisema kufutwa kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 kutasababisha upungufu wa mapato ya Sh240 bilioni.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Juu unamaanisha kuwa Wakenya wataendelea kulipa ushuru wote uliomo katika sheria inayopingwa, ikiwa ni pamoja na asilimia 16 ya ushuru wa ongezeko la thamani kwenye mafuta.

Related Posts