NYOTA chipukizi wa Vijana ‘City Bulls’, Fotius Ngaiza anaendelea kuwakimbiza wakongwe wa mchezo huo katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwenye udakaji wa mipira maarufu rebound.
Rebound ni mipira inayokosa kuingia katika golini na kudundia ndani ya uwanjani, ambapo mchezaji anayeiwahi mipira hiyo inapogusa ardhi kabla ya mtu mwingine kuichukua ndiye anayehesabiwa kuwa rebounder.
Ngaiza anaongoza katika udakaji huo wa mipira akifanya hivyo mara 267, huku nafasi ya pili ikienda kwa Jimmy Brown wa UDSM Outsiders aliyedaka 203.
Wachezaji wengine waliofuatia kwa udakaji ni Elias Nshishi (ABC mara 190), Amin Mkosa (169) na Jordan Jordan (165) wote Mchenga Star, Cornelius Mgaza (Savio 164), Adam Lutungo (Mgulani JKT 158), Isaya Aswile (Chui 156) na Mwalimu Heri mara 152.
Fotius aliliambia Mwanaspoti kuwa kuongoza kwake kumechangiwa na mazoezi anayofanya mara kwa mara katika uwanja wa Sekondari ya Zanaki.
Kwa upande wa uzuiaji (blocks) mchezaji Victor Michael wa Vijana ‘City Bulls’ anaongoza akifanya hiyo mara 44, akifuatiwa na Fotius anayechezea timu hiyo aliyezuia mara 41.
Wachezaji wengine ni Jimmy Brown (UDSM Outsiders mara 37), Englibert Machumu (KIUT 28), Jordan Jordan (Mchenga Star 28), Bramwel Mwombe (Dar City 24), Emmanuel Chacha (JKT 23), Isaya Aswile (Chui 20) na Charly Kasseng (Srelio) mara 20.