DP World kuokoa Sh1.6 trilioni hadi Desemba

Dar es Salaam. Imeelezwa kutokana na kuanza kazi kwa Kampuni ya DP World katika Bandari ya Dar es Salaam huenda Dola za Marekani 600 milioni (Sh1.62 trilioni) zikaokolewa katika uchumi wa Tanzania, kutokana na kuondolewa kwa tozo ya uchelewaji wa meli.

Fedha hizo zitakazookolewa ni zile Dola za Marekani 1,000 zilizokuwa zikitozwa kwa kila kontena lililokuwa likishushwa katika bandari ya Dar es salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa akizungumza leo Jumanne, Agosti 20, 2024 na Mwananchi amesema kwa kawaida meli zilizokuwa zinakuja Dar es Salaam zilikuwa zikitozwa gharama ya msongamano (Peak season) ambayo ilikuwa Dola 1,000 (Sh2.7 milioni) katika kila kontena kwa sababu ya kusubiri kwa muda mrefu mzigo kupakuliwa, lakini sasa imeondolewa.

“Sasa hivi muda wa meli kukaa umepungua sasa kutokana na hilo, wameondoa hiyo tozo mfano wakati unaagiza kontena badala ya kulipa Dola 4,500 sasa hivi utalipa Dola 3,500,” amesema Mbossa.

Mbossa amesema kampuni ya meli ya MSC ndiyo ya kwanza kuondoa tozo hizo na kufanya gharama za meli kwa bandari za Mombasa na Dar es Salaam kuwa sawa: “Hatua hiyo imesababisha kampuni nyingine za meli kuwa katika presha ya kuondoa hiyo Dola 1,000 kama ilivyofanywa na MSC.”

“Ukiangalia kwa mwaka tunahudumia kontena milioni 1.2, sasa ukichukua nusu ya mwaka uliobakia na kuondoa Dola 1,000. Tumeokoa kama nchi kwa sababu leo ukitaka kuagiza mzigo, ili kupata dola lazima ukanunue kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambao wanazinunua Benki Kuu ya Tanzania (BoT).”

“Kwa hiyo tunachukua akiba yetu ya dola tunakwenda kulipa kampuni za meli, ndiyo maana tunasema fedha iliyookolewa itakuwa Dola milioni 600, lakini pia meli ilikuwa ikisubiria kwa siku 28 sasa imeshuka hadi siku 10,” amesema.

Mbossa amesema hivi sasa meli ya makasha inaaka katika gati siku moja hadi tatu kulingana na mzigo, kisha kuondoka, akisema hatua hiyo imeleta maendeleo makubwa katika utoaji huduma katika bandari ya Dar es Salaam.

Aidha kupungua kwa gharama hizo ni kicheko kwa wafanyabiashara, walaji na Taifa kwa ujumla kwani kupungua kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kunachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi, ikiiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa lango kuu la kiuchumi Afrika Mashariki.

Mbossa amesema mafanikio hayo yanaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati, na yanaonyesha uthabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa ya Watanzania.

Miongoni mwa masuala ambayo TPA imeyataja kuwa ni mafanikio ya uwepo wa DPW tangu kuanza kazi Mei mwaka huu ni kupungua kwa muda wa kusubiri kwa meli, meli za mizigo ya Kontena na RORO sasa zinaweza kutia nanga mara tu zinapowasili, kuboresha muda wa mzunguko na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.

Mbossa amesema uendeshaji wa kreni umeboreshwa, na uzalishaji umekuwa ukiongezeka kwa kasi kutoka Mei hadi Julai 2024, na bandari hiyo kufanikiwa kushughulikia meli yake kubwa zaidi.

Vilevile amesema ufanisi huo unaimarisha ushindani wa kianda kwani bandari ya Dar es Salaam sasa inalingana na Mombasa katika ushughulikiaji wa mizigo.

Kuhusu ufanisi wa bandari kwa sasa Wakala wa Usafirishaji wa Mizigo ya Kimataifa wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) ulisema ndani ya muda mfupi DPW imefanya mabadiliko makubwa na kuongeza ufanisi wa bandari ikiwa ni pamoja na kudhibiti eneo la bandari.

“Udhibiti wa eneo la bandari unawafanya wafanyakazi kujikita katika kazi yao hivyo kuokoa muda. Tumeshuhudia. Kuongezeka kwa mashine za kushusha na kupakia mizigo kila mtu sasa amejikita na kazi kongole nyingi sana kwa DP, punde bandari ya Dar es Salaam itakuwa miongoni mwa bandari bora duniani,” ilieleza taarifa yao ya mrejesho.
 

Related Posts