Mbeya. Hofu imetanda miongoni mwa madereva, abiria na watembea kwa miguu wanaotumia Barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) baada ya taa za kuongoza magari katika eneo la Mafiati, Jijini Mbeya kupata hitilafu na kuzima kwa siku tatu mfululizo.
Hali hii imezua hofu kwa madereva na wananchi, huku Jeshi la Polisi kupitia kitengo chake cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, likieleza kuwa tatizo hilo linaathiri utendaji wa kazi wa askari.
Baadhi ya madereva waliozungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Agosti 20, 2024, wamesema tatizo hili sio la mara ya kwanza, bali limekuwa likijirudia mara kwa mara.
Dereva Alex Mwaipopo amesema kuchelewa kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kufanya marekebisho kunasababisha askari wa usalama barabarani kutumia ishara za mikono kuongoza magari, jambo analodai kuwa limepitwa na wakati.
“Hii ni mara ya tatu au nne kwa mfumo wa taa katika eneo la Mafiati kuzima, hali hii inaathiri utendaji kazi na usalama wa abiria kwa sababu baadhi ya madereva wanakiuka sheria za usalama, hivyo kuleta changamoto wakati wa kuvuka barabara,” amesema Mwaipopo.
Ameomba Serikali ya mkoa kuboresha miundombinu hiyo ili kuepusha ajali zisizo za lazima na kupunguza mzigo kwa askari wa usalama barabarani, hasa wanapolazimika kuongoza magari ya mizigo.
“Askari nao ni binadamu, wanahitaji kupumzika. Serikali imeweka taa ili kurahisisha madereva kujiongoza, lakini sasa inawalazimu kufanya kazi usiku na mchana bila msaada wa taa hizo,” amesema.
Dereva bajaji, Emmanuel Miamba amesema madereva wengi walizoea kufuata mwongozo wa taa za barabarani na kutii sheria, lakini sasa wanakabiliwa na changamoto ya kufanya kazi katika mazingira magumu.
“Serikali yetu inapaswa kuiga mifano ya mataifa mengine, eneo la taa za barabarani linapewa umuhimu mkubwa. Wapo wageni wanaoshangaa kuona uwekezaji mkubwa kwenye taa lakini hazifanyi kazi ipasavyo,” amesema Miamba.
“Tunaomba Serikali itafute njia mbadala kuhakikisha taa zinafanya kazi saa 24 ili kuepuka usumbufu na kurahisisha kazi ya askari wa usalama barabarani.”
Mtumiaji wa barabara hiyo, Selina Joela amesema wanapata shida kubwa wanapovuka barabara kutokana na kukosa mwongozo, hali inayosababisha ajali mara kwa mara, hasa usiku.
“Tunaomba mamlaka husika litazame hili kwa uzito, ikizingatiwa kuwa barabara hii ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa ndani na nje ya nchi,” amesema Selina.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mbeya na Kaimu, Ansigar Komba amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo akisema ukosefu wa taa za kuongoza magari unaathiri utendaji kazi wa askari na shughuli za kiuchumi.
“Tulitoa taarifa kwa mamlaka husika hivi karibuni na marekebisho yalifanyika, lakini tatizo limejirudia tena. Tunaendelea kushirikiana na uongozi wa Tanroads ili kuhakikisha marekebisho yanafanyika haraka iwezekanavyo ili kuepusha ajali na msongamano wa magari,” amesema Komba.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(Tanroad) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Masige Matari alipozungumza na Mwananchi kwa simu, amesema wanalifahamu tatizo hilo na linashughulikiwa kwa haraka.
“Nashukuru kwa taarifa. Niko nje kikazi lakini naliwasilisha ofisini ili lifanyiwe kazi mara moja,” amesema Matari.
Barabara ya Tanzam imekuwa kiungo muhimu cha usafirishaji wa bidhaa kwenda mataifa mbalimbali kupitia mpaka wa Tunduma, Mkoa wa Songwe, huku magari zaidi ya 2,000 yakiripotiwa kutumia barabara hiyo kila siku.