Dar es Salaam. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema demokrasia ni zaidi ya kupiga kura siku ya uchaguzi na kwamba wengi wanaposikia neno demokrasia wanahusisha na upigaji kura licha ya kwamba ina mambo mengi ndani yake.
Kikwete alibainisha hayo Jumatatu Agosti 19, 2024 jijini Abuja, Nigeria wakati akitoa mhadhara kwenye Chuo cha Ulinzi wa Taifa cha Nigeria ambapo alizungumzia kuhusu mapito ya demokrasia barani Afrika.
Alisema demokrasia inapaswa kwenda mbali zaidi ya kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mine, mitano au saba kwa kuwa ndani yake kuna mambo mengine mengi.
“Tafsiri hii ya demokrasia kwenye uchaguzi ina matatizo kwa namna tofauti. Inapuuza ukweli kwamba demokrasia inajumuisha mambo mengi mbali na upigaji kura. Namna uchaguzi unavyopangwa, kutekelezwa kabla, wakati na baada ya upigaji kura inaeleza mengi kuhusu hali ilivyo katika nchi.
“Kwa hakika, migogoro mingi ya kisiasa katika mataifa ya Afrika inahusiana na uchaguzi. Nimepata fursa ya kutazama uchaguzi katika mataifa kadhaa ya Afrika. Ninachoweza kusema kwa ujumla ni kwamba, michakato ya uchaguzi inapokuwa wazi na watu hawajazuiwa kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kupigakura na uchaguzi wao ukiheshimiwa, uchaguzi unakuwa wa amani.
Kikwete ameongeza kwamba Waafrika wanapaswa kuzingatia zaidi namna bora ya kuhakikisha demokrasia, kwa namna yoyote au jina lolote, inajibu mahitaji yao ya umoja na maendeleo pamoja na amani na utulivu.
Kiongozi huyo mstaafu ameeleza kwamba Waafrika wanapaswa kuhakikisha wanakumbatia demokrasia kama nyenzo na matokeo katika mlinganyo wa maendeleo, na sio matokeo wala mchezo wa mwisho.
Alisisitiza kwamba wanapaswa kutafuta njia za kuifanya demokrasia ichangie katika kuikomboa sekta binafsi, kufungua fursa kwa vijana na wanawake, kuongeza uwajibikaji wa Serikali kwa raia wake (na kinyume chake), kuongeza uhuru na kudumisha amani, usalama na utulivu.
“Demokrasia inaweza kuwa haikutajwa vilivyo katika matarajio saba ya Ajenda 2063 lakini imejumuishwa katika kila mojawapo.
Ukosefu wa demokrasia katika taifa la Kiafrika utafanya iwe vigumu kwa nchi hiyo kufikia malengo ya ‘Afrika Tunayoitaka’,” amesema.
Rais huyo wa awamu ya nne amesema migogoro mingi ya kisiasa katika mataifa ya Afrika inahusiana na uchaguzi na amebaini hilo kutokana na uzoefu alioupata kutokana na fursa ya kuwa mwangalizi wa uchaguzi kwenye mataifa kadhaa ya Afrika.
“Ninachoweza kusema kwa ujumla ni kwamba, pale michakato ya uchaguzi inapokuwa wazi na watu hawazuiwi kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura na uchaguzi wao ukiheshimiwa, uchaguzi unakuwa wa amani.
“Kukiwa na uwazi katika kila hatua kama vile uandikishaji wa wapigakura, kupanga vituo vya kupigia kura, kuhesabu kura katika vituo vya kupigia kura na vituo vya kukusanyia kura kunakuwa na amani.
Lakini, alisema ikiwa hakuna uadilifu, rushwa na udanganyifu, demokrasia inakuwa shida.
Kuhusu demokrasia na maendeleo, Kikwete alieleza kwamba utafiti mmoja kwamba demokrasia na maendeleo vinakamilishana, kwa maana kwamba demokrasia inaweza kuzalisha mazingira yanayofaa kama vile ushiriki, uwajibikaji na ushirikishwaji kwenye maendeleo.
Alisema maendeleo yanatoa masharti ya awali kama vile utajiri, elimu na maendeleo ya viwanda ambayo yote ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia.
Alisema utafiti mwingine unaonyesha kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya demokrasia na maendeleo. China inatajwa kuwa mfano bora unaounga mkono hoja hii, kwamba licha ya kutokuwa na alama za kuvutia katika cheo cha kidemokrasia duniani, nchi hiyo, katika miongo michache iliyopita, imepata maendeleo ya kuvutia ya kiuchumi kwa kasi zaidi kuliko nchi nyingi za kidemokrasia duniani.
“Licha ya mjadala unaoendelea kuhusu demokrasia na maendeleo, kupitishwa kwa Ubia Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD) kulisisitiza utawala bora kama sharti muhimu kwa maendeleo endelevu. Utawala bora ambao ni kielelezo cha demokrasia, ni alama mahususi ya Ajenda ya Afrika ya 2063,” alisema.