Vitongoji 3,060 Tanzania Bara kupelekwa umeme, Dk Biteko aonya

Dodoma. Serikali imetia saini mradi mpya wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 ikiwa ni vitongoji 15 kwa kila jimbo katika majimbo 204 ya uchaguzi yaliyopo katika mikoa 25 ya Tanzania Bara isipokuwa  Dar es Salaam.

Mradi wa umeme kwenye vitongoji unaanza baada ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), kukamilisha uwekaji wa umeme vijijini huku vilivyobakia ni 151 ambavyo upelekaji umeme utakamilika mwezi ujao.

Rea na makandarasi walitia saini kuanza ujenzi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 3,060 kati ya 64, 359 nchini, huku baadhi ya vitongoji vikiwa tayari na umeme uliowekwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini.

Utiajia saini huo ulishuhudiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliyehimiza utekelezaji wa mradi kwa wakati bila kuchelewesha malipo ya makandarasi.

Akizungumza wakati wa utiaji saini leo Jumanne, Agosti 20, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Saidy amesema mradi uliotiwa saini utahusisha ujenzi wa njia za msongo wa kati wa umeme zenye urefu wa kilomita 258 na ujenzi wa njia za msongo mdogo wa umeme zenye urefu wa kilomita 6118.

Saidy amesema utahusisha ufungaji transfoma 3,059 pamoja na kuunganisha wateja takribani laki moja, hatua itakayoongeza uunganishwaji wa wananchi na huduma za umeme.

“Utekelezaji wa mradi huu utakuwa katika mafungu 25 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, kutokana na sababu za kimanunuzi mafungu 23 yalipata makandarasi isipokuwa mikoa ya Singida na Tanga, ambayo zabuni yake itatangazwa Agosti 22, 2024.

“Utekelezaji wa mradi huu utaongeza mtandao wa njia za umeme kwenye vitongoji na hivyo kuwezesha upatikanaji wa umeme kwenye maeneo yenye shughuli za kijamii zikiwemo shule, zahanati na maeneo ya biashara,” amesema Saidy.

Amesema hatua hiyo ya Serikali itachochea maendeleo kwa kupunguza uhamiaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini, matumizi ya vifaa vya kisasa kwenye vituo vya afya, matumizi ya vifaa vya Tehama na vya maabara kwenye shule pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo.

“Utekelezaji wa mradi huu utachochea maendeleo katika vitongoji vilivyolengwa na hivyo kuboresha hali ya uchumi, huduma za jamii na usalama katika maeneo hayo,” amesema.

Amesema mbali na utekelezaji wa mradi huu, mpango wa Rea ni kufikisha umeme katika vitongoji 10,000 katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara ndani ya miaka mitatu ijayo na hivyo kufanya idadi ya vitongoji 13,000 kufikiwa na umeme ndani ya muda huo. Gharama za mradi huu zinakadiriwa kuwa Sh1.5 trilioni.

Saidy amesema mpango huu utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu wa fedha 2024/25 na Rea itatangaza zabuni ya kupeleka umeme katika vitongoji 4,000 hivi karibuni.

Amesema tangu kuanzishwa Rea, takribani vijiji 12,167 kati ya 12,318 sawa na asilimia 98.8 vimeshapatiwa umeme, na kwamba hadi kufikia Desemba 2024, vijiji vyote vya Tanzania Bara 12,318 vitakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme, hatua ambayo imeongeza hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

“Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa ya kupeleka umeme katika vijiji vyote nchi nzima, bado takribani vitongoji 31,532 sawa na asilimia 49 havijafikiwa na huduma ya umeme,” amesema.

Dk Biteko amewaonya makandarasi wenye tabia ya kwenda kwa wananchi kuchukua fedha wakati wamelipwa na Serikali.

“Jana tukiwa kwenye kamati (Kamati ya Bunge ya Nishati) hoja iliyoibuka ni wananchi kudaiwa fedha na makandarasi. Mimi sitahangaika na mkandarasi nitadai kwa Rea,” amesema.

“Ziko taarifa baadhi ya makandarasi wanaomba fedha kwa wananchi ili wawawekee nguzo ya umeme.”

Dk Biteko amewataka makandarasi wanapokwenda kutekeleza miradi hiyo kwanza wajitambulishe kwa viongozi wa maeneo husika wakiwamo viongozi wa vitongoji.

Related Posts