Arusha. Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Kujenga Kizazi Chenye Usawa Tanzania, Angellah Kairuki ametoa wito kwa wanawake kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na wadau katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Ametoa rai hiyo leo Jumatatu Agosti 20, 2024, jijini Arusha wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua jitihada zinazofanywa na wajumbe katika kuwawezesha wanawake na vijana.
Katika ziara hiyo, kamati ilifahamishwa baadhi ya walengwa wa sera ya uwezeshaji wa wanawake wamekuwa na tabia ya kutohudhuria mafunzo, maonyesho ya bidhaa na kazi zao kama hakuna malipo ya posho.
Kairuki amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto hiyo haraka huku akisema: “Jitihada zinazofanywa na sekta mbalimbali kuwawezesha wanawake zinapaswa kukutana na walengwa wanaotumia fursa hizo ili kujiletea maendeleo yao na jamii kwa ujumla.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) Tawi la Arusha, Alice Mzava amezungumzia changamoto na mafanikio katika jitihada za kukuza biashara za wanawake mkoani humo.
Mzava amesema changamoto kubwa ni wanawake wengi kutoshiriki mafunzo na mahudhurio hafifu kwenye fursa za kuonyesha bidhaa zao wanazozizalisha.
“Wanawake wengi hawashiriki mafunzo. Wengi wanauliza kama kuna chochote na kama hakuna posho hawaji. Lakini wanapokosa mafunzo hayo kwa sababu tu ya posho, wengi huwagharimu katika maendeleo ya kazi zao,” amesema Mzava.
Naye Said Kambi mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ameelezea umuhimu wa mafunzo ya uongozi na biashara kwa wanawake.
Amesema mafunzo ya uongozi ni muhimu na hulenga kuwapatia wanawake na walengwa programu za uwezeshaji stadi za kuongoza vikundi vyao, kampuni na taasisi wanazoanzisha.
“Yanapaswa kutiliwa mkazo sambamba na stadi za kuendesha biashara na kusimamia fedha,” amesema Kambi.
Hata hivyo, jitihada za kuwawezesha wanawake mkoani Arusha zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mercy Michael, kiongozi wa kitengo cha vijana cha TWCC amesema wanatumia mfumo huo wa kusaidiana kununuliana biashara wao kwa wao sambamba na kutafuta masoko ya nje ya nchi.
Raheli Shoo, ambaye amejiunga na jukwaa la uwezeshaji kiuchumi amesema kupitia mafunzo na mtandao aliyoyapata, ameweza kuanzisha biashara mbili zaidi.
“Pamoja na elimu niliyopata, nimejifunza namna ya kusimamia fedha na hiyo imeniwezesha kuanzisha biashara mbili zaidi baada ya kujiunga na jukwaa,” amesema Shoo.