VIDEO: ‘Waliotumwa na afande’ kutetewa na mawakili wanne, wafunguka

Dodoma. Mawakili wanne wanaowatetea watuhumiwa wanne wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza wamesema wanaimani haki itatendeka na itaonekana dhidi ya wateja wao.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ya ubakaji kwa kikundi na ulawiti kwa binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam ni askari wa JWTZ MT.140105 Clinton Damas, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Lord Lema na Nickson Jackson.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo Jumanne, Agosti 20, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma mbele ya Hakimu Mkuu Zabibu Mpangule na inatarajiwa kuendelea mfululizo hadi Ijumaa ya Agosti 23, 2024.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kubaka kwa kikundi na kumlawiti binti huyo ambaye katika kesi hiyo atajulikana kwa jina la XY ili kutomsababishia fedheha kwa jamii.


‘Waliotumwa na afande’ walivyotoka mahakamani, kutetewa na mawakili wanne

Leo Jumanne, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo asubuhi na ilitarajiwa kesi yao ianze kusikilizwa saa nane mchana lakini waliingia kwenye chumba cha mahakama ya faragha saa 10:20 jioni.

Ilipofika saa moja kasoro, Mahakama ilisimama kwa muda ili kutoa nafasi kwa watuhumiwa hao wanaodaiwa ‘kutumwa na afande’ kutekeleza tukio hilo kupata chakula kwa kuwa tangu walipofikishwa asubuhi hawakuwa wamekula; na ilitarajiwa kesi ingerejea tena saa 1:30 usiku.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kula, haikuwezekana kurejea bali walirejeshwa mahabusu hadi kesho Jumatano saa 4:00 asubuhi kesi hiyo itakapoendelea.

Watuhumiwa wa kesi ya ubakaji na ulawiti kwa binti mkazi wa Yombo Dovya wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza wakiwa kwenye karandinga baada ya kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma.

Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wanne wakiongozwa na Godfrey Wasonga. Wengine ni Sadiki Omari, Boniventura Njeru na Meshaki Ngamando.

Akizungumza na waandishi wa habari walioweka kambi mahakamani hapo usiku wa leo Jumanne, mahakamani hapo, Ngamando amesema upande wa Serikali imepeleka mashahidi watano lakini kutokana na muda wamemsikiliza shahidi mmoja.

Pia, amesema hawakumaliza kusikiliza na kumhoji baada ya askari magereza kueleza muda umeisha na walitaka kuwarudisha watuhumiwa mahabusu.

Ngamando amewatoa hofu Watanzania kuwa haki itatendeka na itaonekana kutendeka hivyo wasiwe na wasiwasi kuhusu hilo.

Watuhumiwa wa kesi ya ubakaji na ulawiti kwa binti mkazi wa Yombo Dovya wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Magereza wakati wakipanda kwenye karandinga baada ya kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma.

“Kesi kama hizi mara nyingi huwa zinasikilizwa in camera hasa kwa kesi kama hii ambayo ni ya udhalilishaji, hata sisi wenyewe mawakili hatupaswi kutoa wala kueleza kitu chochote ambacho tumekisikia mahakamani kwa sababu kesi hii inatakiwa kusikilizwa in camera,” amesema.

‘In camera’ inamaa hairuhusiwi kuingia watu wengine zaidi ya wale wahusika kutoa ushahidi na wale mawakili wa upande wa utetezi na wa mashtaka.

“Wananchi na waandishi wa habari tuwe na utulivu tusikilize kesi…naimani kwamba haki itatendeka na siyo tu kutendekea bali itaonekana kuwa imetendeka,” amesema Ngamando

Upande wa Jamhuri unawakilishwa na mawakili watatu.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts