Chumi atoa agizo kukamilisha ujenzi barabara za Mufindi

Mufindi. Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, umeagizwa kuhakikisha unawasimamia ipasavyo makandarasi wanaojenga  barabara katika Jimbo la Mafinga ili kuepusha kero kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Agosti 20, 2024 na mbunge wa Mafinga Mjini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi baada ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu barabara za vijiji vya Kikombo na Ugute, vilivyopo Kata ya Isalavanu.

Chumi amesema Tarura isifanye kazi kwa mazoea, mkandarasi kama hana uhakika wa kukamilisha kazi kwa viwango stahiki ni bora wasubiri badala ya kumpatia kazi ambayo hataimaliza kwa wakati hali itakayosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Kwa hali ilivyo sasa kwa baadhi ya barabara, ingekuwa bora kama wajenzi (bila kuwataja) wasingepitisha greda kwa ajili ya kutengeneza barabara, kwa sababu wameacha bila hata kumwaga maji na kushindilia, hali hii ya vumbi inasababisha kero kubwa kwa wananchi,” amesema Chumi.

Ameitaka sababu Tarura ijipange vema kwa kuwa hawezi kukubali wananchi wa Mafinga kuilalamikia Serikali kwa ya uzembe wa watu fulani katika utekelezaji wa kazi.

Mbunge huyo pia amemwagiza Meneja wa Tarura Wilaya ya Mufindi kufika katika vijiji vya Ugute na Kikombo kutatua changamoto hiyo ya barabara.

Amesema wananchi wanahitaji barabara hiyo ikamilike ili kuondoa adha ya vumbi wanayopata.

Akizungumzia kero ya vumbi, Oscar Sagalla mkazi wa Kijiji cha Ugute amesema ingekuwa bora mkandarasi huyo ‘asingeichambua’ barabara wangeepuka kero ya vumbi linalotimuka muda wote.

“Barabara imekuwa kero kubwa kwetu kwa namna ambavyo mkandarasi amefanya kazi, amepitisha greda na kuacha barabara hiyo bila hata kumwaga maji. Sasa ukitaka kwenda Mafinga, lazima ubebe nguo za ziada kwa sababu unafika mjini ukiwa umejaa vumbi,” amesema Sagalla.

Hata hivyo, akizungumza mbele ya mbunge Chumi, Meneja wa Tarura Wilaya ya Mufindi, Richard Sanga amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo akielezea hatua ambazo tayari wameshaanza kuzichukua.

Sanga amesema tayari wameshamuandikia barua mkandarasi huyo ili afanye marekebisho ya barabara hiyo haraka.

“Huyu mkandarasi bado anaendelea na kazi na hajaikabidhi rasmi, lakini tayari ameshaandikiwa barua kwa ajili ya kufanya marekebisho na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu,” amesema meneja huyo.

Katika ziara hiyo, mbunge Chumi pia alikabidhi vitanda vitatu kwa ajili ya Zahanati ya Kikombo ambayo bado inajengwa sambamba na mabati 81 kwa ajili ya ofisi ya Serikali ya kijiji hicho.

Aidha, alitembelea ujenzi wa mradi wa maji wa Ugute-Kitelelwasi, ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).

Related Posts