WAZIRI wa Madini Anthony Peter Mavunde amempongeza mwekezaji mzawa God Mwanga kwa namna alivyowekeza kwenye madini ya kinywe hapa nchini.
Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha madini ya kinywe cha Permanent Minerals Ltd, kilichopo kijiji cha Kandasikira Kata ya Shambarai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Amesema God Mwanga ni miongoni mwa wawekezaji wazawa wanaosababisha Tanzania kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa madini kinywe Afrika.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza juu ya uongezaji thamani madini nchini na sasa tunaona wawekezaji na hasa wawekezaji wazawa wameanza kuitikia wito huo,” amesema Waziri Mavunde.
Amesema wataendelea kuongeza nguvu ya utafiti ili kuvutia uwekezaji mkubwa katika eneo hilo ambalo madini maarufu ni Tanzanite lakini kutokana na uhitaji mkubwa wa madini kinywe duniani naamini uwekezaji wa kutosha pia utafanyika katika kuchimba na kuchakata madini hayo.
“Tanzania kwa sasa ni ya tatu katika uzalishaji wa madini kinywe katika bara la Afrika, ikitanguliwa na Madagascar na Msumbiji.Tunaamini kwamba Leseni 10 zote za kati na kubwa za uchimbaji madini kinywe zikianza kufanya kazi nchi yetu itakuwa miongoni mwa nchi vinara wa uzalishaji madini kinywe Afrika,” amesema Mavunde.
Mwekezaji mzawa wa kiwanda hicho God Mwanga amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 108,000 kwa mwaka na kitatoa ajira 300 za moja kwa moja huku Halmashauri ya Simanjiro ikitegemewa kuongeza mapato kupitia uwekezaji huo.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro. Fakhi Raphael Lulandala amewahakikishia wawekezaji hao ushirikiano kutoka serikalini na kutoa wito kwa wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika wilaya hiyo yenye utajiri wa madini mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amepongeza uwekezaji huo mkubwa wa kiwanda na kuwasilisha kwa kiwanda maombi ya ajira kutoa kipaumbele kwa wana jamii wanaozunguka kiwanda na pia jamii kunufaika na CSR.
Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Lendauo Mamasita amesema jamii imetoa ushirikiano wa kutosha kwa mwekezaji mzawa God Mwanga na wachina waliowekeza katika eneo hilo.